Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, nianze kuunga mkono hoja kwa kuipongeza Serikali ya CCM chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli, kwa kazi kubwa wanayofanya ya kurejesha nidhamu na uwajibikaji katika nchi yetu. Japokuwa hali hii kwa kuwa ni ngeni kwa wengine na kinyume cha matazamio yao wameitafsiri katika namna hasi. Ombi langu, tuendelee hivi hivi huku tukibaki katika lengo letu la kumkomboa Mtanzania kutoka kwenye lindi la umaskini, ujinga na maradhi na kuwapeleka kwenye nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2030.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba sasa nijikite kwenye hoja yangu. Bila kusahau naomba ku-declare interest kwamba mimi ni mdau wa elimu wa shule binafsi. Naomba nielekeze mchango wangu kwenye ushirikiano kati ya Umma na Binafsi (PPP) katika uwekezaji kwenye sekta zote muhimu nchini ikiwemo elimu, afya, viwanda, miundombinu na kadhalika. Nafahamu kuwa Serikali yetu sikivu ya CCM ina nia njema sana katika hili hivyo naomba nitoe ushauri ufuatao:-
(i) Kubainisha wazi na bayana majukumu ya kila upande katika utekelezaji wa sera ya PPP katika sekta ya elimu (utungaji wa sera, sheria, miongozo, uchangiaji wa gharama za elimu, usimamizi wa taasisi za elimu, upimaji na udhibiti ubora);
(ii) Kuwa na mifumo imara na endelevu ya mawasiliano (dialogue structure) baina ya pande zote mbili ili kupeana taarifa za mara kwa mara na uzoefu mbalimbali wenye tija kwa maendeleo ya nchi; na
(iii) Kuwe na mifumo imara yenye kujengeana uwezo baina ya pande zote mbili kwa vile kila upande unacho cha kujifunza kutoka kwa mwenzake.
Mheshimiwa Naibu Spika, pale Serikali itakapofungua milango katika PPP ni hakika tutaona mafanikio na mabadiliko makubwa ya kiuchumi ndani ya muda mfupi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, niishauri pia Serikali kuweka vipaumbele vinavyotekelezeka. Mpango huu ni mzuri lakini umekuja na vipaumbele vingi sana. Tukiendelea hivi tutabaki kupapasa tu na hatutafika tuendako.
Mheshimiwa Naibu Spika, mifumo yetu ya kodi si rafiki hali inayopelekea kutishia kuongezeka hali ya rushwa hasa katika chombo chetu cha kodi (TRA). Kuwe na mazingira rafiki na dialogue structure baina ya TRA na mlipa kodi badala ya vitisho na kuuza kwa mnada mali za wafanyabiashara kwani kwa kufanya hivyo Serikali inakosa pesa na wale wafanyabiashara wanakuwa wamefilisika na mwisho tunaishia kuumia kama nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu ina mpango wa kutupelekea kwenye Tanzania ya viwanda, basi niishauri Serikali iweke nguvu kubwa kwenye kilimo cha umwagiliaji ili viwanda vyetu viweze kufanya kazi kwa kipindi chote cha mwaka. Endapo hatutawekeza kwenye kilimo cha kisasa ambapo asilimia 80 ya Watanzania ndiyo wahusika wakuu katika hili, ni bayana hatutaweza kumwondoa huyu Mtanzania maskini kwenye lindi la umaskini.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nitoe ushauri wangu kwa Wizara ya Afya. Ni dhahiri kwamba ni pale tu watu wetu watakapokuwa na afya njema ndipo tutakapoweza kufanikiwa katika mambo yote. Mtu mgonjwa asiyeweza kutibiwa kwa wakati hawezi kamwe kufanya uzalishaji wa aina yoyote ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nigusie suala la ukosefu wa dawa MSD. Suala hili linaipeleka Serikali yetu pabaya sana. Naomba hili suala la dawa lifanyiwe kazi kwa gharama yoyote ile ili kulinusuru Taifa na vifo vya watoto na kizazi kijacho kwa kukosa chanjo za muhimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mapendekezo haya ya Mpango bado hayajaweka bayana ni jinsi gani huduma ya maji zitafika vijijini ili kumtua ndoo mama wa Kitanzania. Asilimia zaidi ya 80 ya muda wa wanawake hawa wazalishaji inapotea kwenye kusaka maji usiku na mchana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nipende tena kupongeza juhudi za Serikali kwa jinsi pia inavyoshughulikia suala zima la mikopo ya elimu ya juu inayotishia amani ya wapiga kura wetu. Busara ya hali ya juu itumike ili kumaliza tatizo hili na kila mhusika abaki akiwa ameridhika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, niunge mkono hoja, ahsante sana.