Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa Mpango huu ambao ametuletea, Mpango wa Pili wa Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 mpaka 2020/2021.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli nimefurahishwa sana na Mpango huu ambao umeletwa mbele yetu. Mpango huu umeeleza bayana vipaumbele ambavyo Serikali inategemea kutekeleza katika kipindi hiki cha miaka mitano.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika vipaumbele hivyo ambavyo ni msingi mkubwa sana wa maendeleo ya nchi yetu mambo yako mengi lakini suala la kwanza ambalo ni la msingi sana ni kuendeleza kilimo. Suala la kilimo inabidi lipewe kipaumbele cha kutosha. Kilimo ndiyo uti wa mgongo wa maendeleo ya nchi yetu, kilimo ndiyo kinachotoa ajira kubwa kwa wananchi wengi katika nchi yetu, zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wanategemea kilimo. Pia tunapotaka kuipeleka nchi kuwa ya viwanda tunategemea zaidi kwamba malighafi nyingi na mazao mengi yatakuwa ni yale yanayotokana na kilimo na hivyo viwanda vingi ambavyo tunavianzisha vitakuwa vile vitakavyochakata mazao yanayotokana na kilimo. Naomba tuongeze jitihada kabisa za kuhakikisha tunakiimarisha hiki kilimo, pembejeo zile zinazohitajika katika kufufua kilimo hiki ziongezeke na bajeti ya kilimo iongezeke ili kwenda kujenga nchi ya uchumi safi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiofichika kwamba kama tukikifufua kilimo, tukiimarisha viwanda vinavyotokana na mazao ya kilimo, asilimia kubwa sana ya watu wetu wataajiriwa. Nashauri Serikali ihakikishe tunajenga viwanda vitakavyochakata mazao haya ya kilimo. Viwanda hivi vitasaidia sana kutoa ajira na msukumo mkubwa katika kuchangia pato la Taifa.
Kipaumbele cha pili ambacho kinaendana na hicho cha kilimo ni kuimarisha miundombinu mbalimbali ambayo ita-support hicho kilimo chetu. Miundombinu ya barabara, umeme na vitu vingine vinavyoendana na hivyo vitasaidia sana kuhakikisha nchi yetu inaendelea. Pia miundombinu hiyo itatoa ajira kwa vijana wetu wengi katika nchi yetu. Kwa hiyo, lazima tuweke nguvu zaidi katika kuimarisha hiyo miundombinu ya reli na vitu vinginevyo.
Nimefarijika sana na jitihada za Serikali za kuamua kufufua Shirika letu la Ndege. Katika ulimwengu huu kila nchi ina shirika lake na Shirika la Ndege ndiyo linatoa mchango mkubwa sana katika kuendeleza nchi. Tumeona nchi mbalimbali jinsi zinavyofanya. Kwa kweli inasikitisha sana kuona shirika letu limekuwa likisuasua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hizi jitihada ambazo Serikali ya Awamu ya Tano imeamua kuzichukua katika kulifufua shirika hili lazima tuziunge mkono kwa udi na uvumba ili kuhakikisha linakua na linatoa ajira nyingi kwa vijana wetu lakini pia tuweze kulitumia katika kuharakisha kuchochea maendeleo katika sehemu mbalimbali. Shirika letu sasa hivi lina ndege moja au mbili …
WABUNGE FULANI: Hamna.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri hizi ndege ambazo tumepanga kuzinunua zikinunuliwa naamini zitachochea sana maendeleo ya nchi yetu. Kwa hiyo, tuongeze hizo jitihada. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ili tuweze kuleta maendeleo ya kweli lazima huduma mbalimbali zikiwemo huduma za masuala ya fedha ziimarike. Hivi sasa mabenki mengi yamekuwa yakifanya biashara maeneo ya mijini hayakuweza kwenda vijijini. Sasa hivi Benki ya Wakulima imeanzishwa lakini bado iko Dar es Salaam. Nashauri kama ni Benki ya Wakulima ianzishwe mikoani ili wakulima wapate nafasi ya kwenda kukopa huko na tuweze kufufua kilimo chetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia mabenki yetu mengi yalikuwa yanafanya biashara kwa kutegemea fedha za Serikali. Kwa hiyo, naomba niunge mkono jitihada za Serikali, sasa hivi za kuhakikisha fedha zote za Serikali zinakuwa Benki Kuu ili mabenki haya yaende sasa kutafuta wateja huko vijijini na hii itasaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sambamba na hilo, wakati Serikali inachukua jitihada za kubana matumizi na hivyo kuondoa fedha nyingi za Serikali kwenye mabenki maana yake sasa mabenki nayo lazima yafanye jitihada za makusudi za kuhakikisha kwamba riba za mikopo zinashuka. Sasa hivi riba ziko juu sana, wananchi wakikopa baada ya miaka miwili, mitatu unakuta deni ni mara mbili ya kile ambacho alikuwa amechukua hali ambayo haisaidii kuchochea maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nadhani kwa kuangalia riba zile za kukopa na riba ambazo wanazitoa kuna spread kubwa ambayo nafikiri Serikali pamoja na mabenki yachukue hatua zinazostahili kuhakikisha kwamba yanarekebisha hiyo hali ili kusudi benki hizi zichochee maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mpango huu umejikita katika utoaji wa huduma za jamii hasa suala la elimu. Suala la elimu limepewa uzito mkubwa na naunga mkono kwani bila kuimarisha elimu hatuwezi kuwa nchi ya kipato cha kati. Elimu hii ndiyo itakayotuwezesha tupate watalaam wazuri, tupate watalaam wa kati wanaohitajika katika viwanda vyetu. Lazima mitaala ya elimu zetu kuanzia shule za msingi, sekondari, vyuo vya kati na vyuo vikuu ipitiwe upya ili iendane na mahitaji halisi ya wakati tulionao. Hilo naamini linawezekana kwa kutumia watalaam na uwezo uliopo tunaweza tukafanya kazi nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda vyetu vinahitaji wataalam, sasa hivi vijana wengi wamekuwa wakikimbilia sana kwenda kusoma kwenye vyuo vya elimu ya juu wanakuwa ni ma-engineer, lakini nadhani kuna haja ya kuimarisha elimu ya mafundi wale wa kati na hasa vyuo vyetu hivi vya VETA na vyuo vinginevyo. Hivi ndivyo vitakavyoweza kuchukuwa vijana wengi na kuwapa ujuzi unaohitajika katika viwanda vingi. Kwa hiyo, hizi jitihada lazima ziungwe mkono kwa hali na mali ili tuhakikishe kwamba tunafika kule tunakokusudia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kupongeza Serikali ya Awamu ya Tano ya kuhakikisha kwamba elimu yetu inakuwa bure kwenye shule za msingi na sekondari mpaka kidato cha kumi na mbili. Kwa kweli hili ni suala zuri sana lazima tuipongeze Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tumeanza kuitekeleza hii sera imeonyesha matumaini na matunda makubwa kwani watoto wengi wameweza kwenda shule na kuandikishwa. Sasa lazima tuhakikishe kwamba tunaunga mkono jitihada hizi na tunashirikiana na Serikali ya Awamu ya Tano ili kuhakikisha hii azma inatekelezeka. Zipo changamoto ambazo tutakabiliana nazo na ni kitu cha kawaida. Unapoamua kuanzisha kitu chochote lazima ukabiliane na changamoto ambazo naamini tutashinda na tutafika mahali pazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuzungumzia suala la afya. Jitahada za Serikali ya CCM sasa hivi ambazo tumejikita nazo na tumeiweka kwenye Ilani yetu ya Uchaguzi kwamba kila kijiji kuwe na zahanati na tunataka kila kata kuwe na kituo cha afya lakini vituo hivi vya afya vinahitaji pia viwe na wataalam. Jitihada ambazo wananchi wameanza kuonyesha kwa kujenga zahanati na vituo vya afya, Serikali iongeze mkakati wa kuhakikisha inawaunga mkono na pale ambapo wamekamilisha vianze kufanya kazi kama ambavyo inakusudiwa. Wananchi wamejitoa sana kuhakikisha wanajenga hivi vituo vya afya na zahanati, Serikali itekeleze wajibu wake pale ambapo tunaona kwamba panatakiwa kutekelezwa ili kusudi maendeleo yapatikane haraka kadri inavyowezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, Mpango huu ni mzuri, mpango wa kuimarisha reli ya kati, mpango wa kujenga reli kwa standard gauge ni wa muhimu sana kwani utatusaidia sana kuchochea maendeleo katika mikao yote. Hii ndiyo njia pekee itakayotusaidia nchi yetu kuweza kuunganishwa na hizo nchi zingine na kupunguza gharama za uendeshaji ambazo sasa hivi zimekuwa ni kubwa sana. Sasa hivi barabara zetu zinabeba malori makubwa ambayo yanasababisha barabara zetu zisidumu kwa muda mrefu. Kwa hiyo, tukiimarisha reli hii naamini itakuwa limesaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa na hayo machache, naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana kwa kunipa nafasi.