Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Joram Ismael Hongoli

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa uamuzi wa kutoa elimu bure toka shule ya msingi mpaka kidato cha nne. Hii imesaidia kuongezeka kwa udahili wa wanafunzi wa darasa la kwanza na kidato cha kwanza. Ufaulu wa watahiniwa wa darasa la saba na wale wa kidato cha sita unaendelea kupanda wakati ngazi ya chini, yaani sekondari, umeshuka.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto hapa ni Walimu. Walimu wa masomo ya sayansi ni wachache sana. Kuna baadhi ya shule hazina kabisa Walimu wa masomo ya Hisabati, Fizikia, Biolojia na Kemia. Shule ambazo hazina Walimu wa masomo haya bado ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya kidato cha nne ni mbaya sana. Hivyo, ni muhimu katika mipango ya Serikali tuwekeze vya kutosha katika kuzalisha Walimu wa masomo ya sayansi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nyumba za Walimu katika shule nyingi zimekuwa chache sana. Walimu wengi bado wanakaa mbali na shule, kuna baadhi wanatembea umbali wa kilometa tano mpaka saba kwenda shuleni, hasa maeneo ya vijijini; hivyo, hufika shuleni wakiwa wamechoka na wakati mwingine kushindwa kutekeleza majukumu yao ya kuwasaidia wanafunzi. Serikali iweke utaratibu madhubuti wa kujenga nyumba za Walimu, hasa kwa shule zilizopo vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa hatua inayochukua ya kuanzisha Vyuo vya Ufundi (VETA) kwenye baadhi ya maeneo. Kwa kuwa, tunaelekea kwenye uchumi wa viwanda, hasa viwanda vya kati, tuhitaji zaidi mafundi mchundo ambao ndio watafanya kwenye viwanda hivi. Hivyo ni muhimu kuweka utaratibu wa kujenga vyuo hivi kwa kila Wilaya. Kuendelea kuongeza Vyuo Vikuu haitusaidii sana kutatua tatizo la ajira na nguvukazi, kwani wahitimu wa Vyuo Vikuu ni Maafisa ambao wanatarajiwa kwenda kusimamia kazi katika sekta mbalimbali. Je, ni nani atafanya kazi katika viwanda hivi kama hatuna watu hawa wenye elimu ya kati?
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada za Serikali katika kuendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu, bado vijana wengi wamekuwa wakikosa mikopo hiyo. Vijana wengi, hususan watoto wa maskini wanaotokea vijijini ndio ambao wamekuwa wakikosa mikopo. Serikali ipitie upya vigezo vinavyotumika katika utoaji wa mikopo. Vigezo hivyo viwe wazi na ikiwezekana Wakuu wa Shule za Sekondari wapewe hayo maelekezo ya jinsi Bodi ya Mikopo inavyotoa tathmini ya kukopesha wanufaika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iwe na utaratibu wa kufanya projection/forecast mapema ili kujipanga na kujua mahitaji ya kiasi cha fedha kitakachohitajika kwa mwaka husika ili tuingize kwenye bajeti ya Serikali. Hii inaweza kufanyika kwa kujua ni vijana wangapi watahitimu kidato cha sita kwa mwaka huo wa fedha? Tunatarajia watafaulu wangapi? Hii itatusaidia kupunguza baadhi usumbufu na matatizo yanayowapata kwa kukosa mikopo hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Naipongeza Serikali kwa kuweka mpango wa kuendeleza utafiti katika kilimo kwa mazao mbalimbali. Serikali sasa ijikite kwenye utafiti wa masoko ya mazao haya. Wakulima wetu, hususan vijijini, wamekuwa wakijituma katika kuzalisha mazao mbalimbali. Tatizo kubwa limekuwa ni kupata soko la mazao hayo. Kuna baadhi ya maeneo, mfano, Lupembe; mazao ya matunda kama vile nanasi, maembe, parachichi, yamekuwa yakiozea shambani kwa kukosa soko la uhakika. Pia, barabara mbovu au zisizopitika wakati wa kifuku zimekuwa zikiathiri soko la mazao haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri Serikali ikaweka utaratibu wa kutengeneza barabara zinazoenda kwenye maeneo ya uzalishaji ili kuokoa mamilioni ya fedha yanayopotea au hasara wanayopata wakulima kutokana na ubovu wa barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nampongeza Waziri wa Fedha na Watendaji waliopo chini ya Wizara hii kwa kuunda mpango huu. Naunga mkono hoja.