Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Amb. Adadi Mohamed Rajabu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. BALOZI ADADI. M. RAJAB: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nashukuru sana kupata nafasi hii ya kuchangia taarifa za Kamati hii. Kwanza nawapongeza Wenyeviti wote wa Kamati kwa mchanganuo mzuri na mambo mazuri, mapendekezo na maoni ambayo wameyatoa kwenye Kamati zao. Nitajikita kwenye Kamati zote mbili kwa kifupi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Kamati ya Katiba nilitegemea sana wangeweka msisitizo pia pamoja na mambo mengine suala la msongamano na ucheleweshaji wa kesi Mahakamani. Kamati hii ya Katiba ina mwingiliano sana na Kamati yangu ya Mambo ya Nchi za Nje, Ulinzi na Usalama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yangu imetembelea sana Magereza na imeona namna ambavyo mahabusu pamoja na wafungwa walivyosongamana ndani ya Magereza, ni tatizo kubwa sana. Tatizo hili linatokana hasa na makosa mawili tu au matatu. Utaona makosa ya mauaji na makosa ya madawa ya kulevya ndiyo ambayo yanachukua muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mahabusu wako wengi sana wa makosa ya mauaji, madawa ya kulevya na Wahamiaji haramu. Sasa hawa watu wamekaa gerezani muda mrefu, mtu anakaa miaka miwili, mitatu, minne anasubiri apangiwe kesi Mahakama Kuu. Kwa hiyo unaona kwamba Kamati hii ilikuwa na uwezo wa ku-force Serikali hasa Mahakama Kuu kuangalia uwezekano wa kubadilisha taratibu zao, kanuni zao kuendana na wakati kwa sababu mahabusu wanakaa sana wakisubiri kesi zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kitu kinaitwa hiyo High Court Session. High Court Session inapangwa, inaweza kukaa miaka mitatu mahabusu wanasubiri High Court Session iweze kuitwa. Ni muhimu sasa hivi Kamati ipendekeze kwa Jaji Mkuu waangalie uwezekano wa kubadilisha kitu kinaitwa High Court session.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wafungwa kule ambao wamehukumiwa kunyongwa. Wamejaza Magereza na kama unavyojua ukihukumiwa kunyongwa hufanyi kazi yoyote, wanakula tu, wanasubiri kunyongwa. Kunyongwa kwenyewe hakujulikani watanyongwa lini. Sasa sijui mamlaka zinazohusika zinafikiria namna gani kwa sababu wanaendelea. Sasa hivi karibu miaka ishirini, thelathini kuna watu wamehukumiwa kunyongwa wako kule hawanyongwi, vifaa vya kunyongea vimekaa mpaka vimeota kutu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri kama sheria hiyo mamlaka inaona kwamba haitekelezeki basi iletwe Bungeni tuifute, maana hata kwenye kupunguziwa adhabu wafungwa ambao wanataka kupunguziwa adhabu wale waliohukumiwa kunyongwa hawapunguziwi adhabu hata siku moja sasa sijui ni kwa nini. Ni vizuri suala hilo Kamati pia ingeshauri ili tuibane Serikali ili mamlaka zinazohusika zifikie maamuzi ya hawa watu ambao wamehukumiwa kunyongwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mamlaka zinazohusika zinashindwa basi zirekebishe ziteremshe kwa Mwakyembe huenda atasaini watu wanyongwe, lakini vinginevyo kwa kweli wanajaa na wahamiaji haramu ambao wako mle wanajaa. Maafisa uhamiaji, mhamiaji haramu anakosa anamtupa jela hata bila kupelekwa Mahakamani. Ni vizuri Sheria hiyo pia iangaliwe na kuletwa hapa Bungeni tuweze kuiangalia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la ajali. Suala la ajali ni kubwa sana na zinaleta athari kubwa sana. Watu wanakufa sana kwa ajali, watu wanapata vilema kwa ajali. Nilitegemea pia tuungane na Kamati hii ya Katiba na Sheria tuweze kulazimisha Serikali ilete mapendekezo ya kubadilisha suala hilo, kwa sababu mambo mengi ambayo yanatokana na ajali ni mambo personal (mtu binafsi). Ajali ambazo zinatokea karibu asilimia 70 na ushee zinatokana na matatizo ya mtu binafsi. Ni vizuri Sheria hiyo tukaiangalia upya na iletwe Bungeni tuweze kuifanyia marekebisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye Kamati ya Utawala Bora na Serikali za Mitaa, hii kitu inaitwa TAMISEMI. TAMISEMI ni jalala, limechukua kila kitu. Kwenye Majimbo yetu huwezi ukazungumza chochote bila kuangalia TAMISEMI. Ukiangalia afya TAMISEMI, sijui shule TAMISEMI, barabara TAMISEMI, matatizo ya maji TAMISEMI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TAMISEMI ina mambo mengi sana na kwenye Halmashauri inakuwa ni tatizo, kwa sababu tuna mipango mizuri ya kutekeleza bajeti hii ya TAMISEMI lakini hela hakuna, hela zimeanza kuja juzi. Nashauri tu kwamba, tuilazimishe Serikali hizi fedha zilizopangwa kwenye Halmashauri zetu ziletwe kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Muheza tuna mipango mingi sana ambayo tumepanga kwenye bajeti, lakini mpaka sasa hivi sijui hata kama robo zimefika ambazo tumepokea kwenye mpango wa maendeleo. Kwa hiyo, naomba hela hizi ziletwe ili tuweze kukamilisha mambo ambayo yamepitishwa hapa Bungeni na mambo mengi ya maendeleo ambayo tumeamua kuyafanya katika kipindi hiki cha fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Madaraka ya Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa; suala hili sasa hivi linakwenda kubaya na nashauri Serikali iliangalie kwa kina. Hawa Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa wanaonekana hawajapata semina yoyote ya kuelewa madaraka ya ukamataji. Wao wanaelewa tu mtu mpeleke ndani. Mtu amekubishia kwenye mkutano unaamua akamatwe apelekwe ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, askari Polisi anachukua miezi sita kusomea namna ya kumkamata mtu, namna ya kuondoa haki ya mtu, sasa huwezi ukajibishana na mtu tu kwenye mkutano wewe Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa unaamua huyu mtu umweke ndani. Ni suala ambalo ni sensitive na ningeshauri Kamati suala hili tuwabane Serikali hawa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wapate semina, waelewe maana ya ukamataji, waelewe maana ya kuweka watu ndani vinginevyo itakuwa chaos hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa sana kupongeza suala la mradi wa mabasi wa DART, ni mradi ambao unatakiwa upongezwe. Kwa kweli huu mradi sijui kwa nini umechelewa, lakini haya mabasi yangeweza kuwa kwenye Jiji la Dar es Salaam sasa hivi naamini Dar es Salaam upungufu huu wa usafiri ungeweza kupungua kwa kiasi kikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala ambalo ndugu yangu aliyesema la kutoa matairi alilosema Mheshimiwa Rais, zile ni mbinu za Askari, Rais amewashauri tu Askari namna ya kufanya kazi zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti kwa hiyo, si kutoa matairi ni vielelezo mojawapo ambavyo vitatolewa Mahakamani kuthibitisha huyu mtu alikuwa anaingia kwenye barabara ya mwendokasi. Ile ni barabara ya mabasi ya mwendokasi na yanapokukuta wewe ni maiti. Sasa ni lazima askari wawe wakali na wahakikishe kwamba kweli wanatekeleza hizo sheria inavyopaswa. Kwa hiyo, Rais alifanya kuwashauri tu askari, hiyo ni mbinu mojawapo ya kuwakamata hao watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge ni suala ambalo tunatakiwa tulipongeze kwamba hawa wapanda bodaboda wanapoingilia haya mabasi kwa kweli waelewe kwamba ni kifo. Kwa hiyo, ni lazima kwamba Sheria iwe kali kwenye suala hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napongeza sana suala la TASAF, suala ambalo linatujengea imani sana kwa wananchi. Kuna matatizo madogo madogo ambayo wanatakiwa wayarekebishe lakini huu mpango wa TASAF uongezwe na tunaunga mkono sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono mapendekezo yote na ningeshukuru mapendekezo haya ambayo tumeyashauri, basi yachukuliwe ili tuwabane Serikali vizuri, nakushukuru sana.