Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbulu Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kupata nafasi hii ya kuchangia Wizara hizi mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa kwanza nitauelekeza kwenye sehemu hii ya TASAF. Kwanza, nikubaliane na wachangiaji wenzangu kwamba TASAF inasaidia sana kwenye maeneo yetu hasa kwa kuziinua familia hizi ambazo zina hali duni. Changamoto ambayo tunapata kwenye maeneo yetu ni kwamba wanapoleta hizi fedha za TASAF mara nyingi watu hawa au familia hizi zinapata changamoto pale ambapo kunakuwa na michango ya vijiji. Fedha zinakuja kwa ajili ya kuwawezesha hawa wafaidika wa TASAF wenyewe wakati huo huo Wenyeviti na Watendaji wa Serikali wanawatoza michango kwa pesa hizi za TASAF.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niombe kidogo Wizara itoe maelekezo kwa sababu pia hawa ndugu zetu wengine wamesamehewa michango kwa hiyo wanapopata ule mwanya wa kupata hizi pesa za TASAF wakati huo huo wanakamatwa michango na wanatakiwa kuchanga tena kwa kutumia pesa ambazo Serikali imewapatia kwa ajili ya kujisaidia kwa maisha yao. Kwa hiyo, niombe Serikali itoe elimu katika Serikali zetu za Mitaa hasa vijiji ili Watendaji waweze kuwasamehe watu hawa ambao pia Serikali imeona wana haki ya kupata hii pesa ambayo inasaidia kuwainua hasa hizi familia ambazo zina tatizo la kipato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tena kujielekeza kwenye sehemu nyingine hasa hii ya ajira. Namshukuru kwanza Mheshimiwa Kairuki ameeleza jinsi ambavyo ajira zinategemea kuachiwa kwenye kada mbili za afya na elimu. Kwenye Halmashauri yangu ya Mbulu Vijijini tuna shida kubwa sana ya watumishi hawa hasa kwenye kada ya VEO na WEO. Sasa hivi watumishi hasa Walimu ndio wanakaimu nafasi za Maafisa Watendaji. Hebu niambie leo hii tuna tatizo la Walimu, tena Walimu wa sayansi wanakaimishwa nafasi hizi ili kusaidia mpango mzima wa governance huku chini. Pamoja na nafasi hizi ambazo Waziri amezitangaza leo wanazotegemea kutoa ajira za afya na elimu, wajitahidi kufungua ajira kwenye nafasi za Watendaji wa Vijiji na Kata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nataka nitoe mchango mwingine katika suala la property tax, hii kodi ya majengo ambayo kimsingi ukiangalia sheria sasa inakwenda kukusanywa na TRA. Kwa sababu sheria hii bado haijatungwa na Bunge na tunategemea iletwe baadaye tuone jinsi tutakavyosaidia kwa sababu TAMISEMI wametoa maelekezo ambayo siyo mazuri sana kwenye Halmashauri zetu. Kwa mfano, Halmashauri yangu imepewa waraka ambapo inatakiwa ikusanye kodi ukiangalia wameweka viwango vya kukusanya kodi kwenye maeneo ambayo hayafai. Wamepanga pia kukusanya kodi kwenye nyumba za tembe na kwenye nyumba za majani. Mimi sikatai kodi inakusanywa na ni sheria na inatakiwa kukusanywa lakini siyo sahihi sana kukusanya kodi kwenye nyumba za tembe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya kule nina wapiga kura wangu wananchi wanaoitwa Wahadzabe wao wamezoea kukaa porini, lakini sasa tunawaomba tuwajengee nyumba ili wakae kwenye nyumba. Wakisikia sasa Halmashauri inakusanya kodi inayoitwa kodi ya majengo hasa kwa nyumba za nyasi na tembe wanapata maswali makubwa na kutaka kuendelea kukaa porini. Mheshimiwa Waziri naomba uangalie suala hili na lipo kwenye Jimbo langu la Mbulu Vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuchangia pia suala zime la upandishaji wa madaraja. Wako watumishi mwaka jana walipandishwa madaraja na wengine baada ya waraka kutoka wamesimamishwa kupandishwa madaraja. Niiombe TAMISEMI iangalie namna gani nzuri ya kuwapa pia motisha watumishi hawa ambao kimsingi wenzao wameshapandishwa madaraja baada ya waraka kutoka wamesimamishwa na hawezi kupandishwa madaraja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ukija kwenye Halmashauri yangu ya Mbulu Vijijini specific asilimia 90 ya Wakuu wa Idara wanakaimu. Sasa basi niombe kwa sababu Halmashauri tumeshaleta mapendekezo ya kuwapandisha hao Wakuu wa Idara, Serikali iweze kutoa mwanya wakuu hawa wapandishwe. Mtu ameshakaimu miaka mitano unategemea nini? Naomba Serikali iangalie namna gani ya kuwapandisha na kuwarasimisha hawa Wakuu wa Idara ambao wamekaimu kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala la asilimia tano za wanawake na vijana kwa habari hii tunayosema mikopo ya vijana. Ni vigumu kwa Halmashauri zetu za vijijini kuweza kutoa hizi hela kwa sababu gani? Hela za OC hazikwenda na Wakurugenzi wengi wanatumia pesa hizi hizi ili kuendeshea shughuli zao. Kwa hiyo, ni vizuri basi hizi fedha za OC ambazo kimsingi ziko kwenye kila bajeti ya Halmashauri za Wilaya ni vyema zikapelekwa kwa wakati ili Watendaji au Wakurugenzi waweze kuzitumia na hatimaye basi wasiende kwenye hela za vijana na wanawake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakwenda kwenye utawala bora. Mimi kwanza nishukuru sana, nina Mkurugenzi mzuri naamini hakupata semina au amepata semina lakini anafanya kazi yake vizuri, nampongeza sana. Pia nimeona wenzangu wengi wamelalamika sana habari ya Watendaji yaani Ma-DC. Mimi nampongeza DC wa kwangu anafanya kazi nzuri na nashukuru Mungu kama hajapata semina mimi naona kwa kweli anafanya kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vibaya sana kila mtu kusema hapa Ma-DC wanafanya kazi mbaya, hapana, mimi nafikiri sio wote. Wapo wa kupongezwa na mimi nampongeza wa kwangu kwa sababu naona anafanya kazi nzuri. Pia nampongeza Mkuu wa Mkoa wangu naona kabisa anafanya kazi nzuri ambayo kimsingi ana-operate ile human right ambayo naiona mwenyewe. Pia namshukuru sana Mungu labda mimi inawezekana nimepangiwa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niunge mkono wenzangu waliosema wanahitaji semina elekezi. Ni vizuri basi Serikali ikaona, kama wenzangu na wengine wamepata tatizo hili la utawala bora ni vizuri hizi semina elekezi zikawekwa na zikapangiliwa kuliko kuwafanya wananchi, watendaji na Wabunge wenzetu wakawa na hali ya sintofahamu katika maendeleo, haiko vizuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze pia Mawaziri wanaofanya kazi na nashukuru sana wamefika kwenye eneo langu. Nawapongeza sana kwa sababu wanafanya kazi kubwa. Nimpongeze Mheshimiwa Rais wetu kwa kuwateua pia hawa Wakuu wa Wilaya, ndugu zangu Wabunge kama wasingeteuliwa Wakuu wa Wilaya wapya ingekuwa biashara kama ilivyo. Sasa hivi ukiangalia Serikali imeanza kukaa katika line yake. Leo hii watumishi wamekuwa na nidhamu. Ukienda kwenye Halmashauri zetu na maeneo mengi ya kazi hakika utaona wananchi wanatekelezewa na wanasikilizwa katika maeneo mengi. Kwa hiyo, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kweli kwanza kwa kuangalia na kuiweka Serikali vizuri kwani sasa hivi Serikalini kuna nidhamu na wananchi wanasikilizwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka nichangie haya tu, ahsante sana.