Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Maswa Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na mimi kuchangia katika taarifa hii ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu utekelezaji wa shughuli zake katika kipindi cha kuanzia mwezi wa Januari, 2016 hadi Januari, 2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kwanza kupongeza Kamati kwa kazi nzuri waliyoifanya, tunawapongeza kwa ufuatiliaji mzuri na ukweli waliouzungumza katika ripoti yao. Na mimi nashukuru kwamba Serikali imefanya kazi nzuri ya kukusanya mapato. Naishukuru vilevile Serikali na kuipongeza kwa kuweza kulipa madeni kwa kiwango kikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza haya kwa sababu tumeona ripoti inaeleza wazi kabisa kwamba ulipaji wa madeni umelipwa kwa kiwango cha juu kabisa na hii ni dalili nzuri kwamba ulipaji huu wa madeni unaweza kutusaidia hata kwa wafadhili kuendelea kutuamini na kuweza kutupa pesa nyingi ili kuweza kuleta maendeleo katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa imeeleza vizuri japokuwa tu mimi nina wasiwasi kidogo kwa baadhi ya mambo ambayo nafikiri tungehitaji uangalizi wa ndani zaidi au wa macho makali zaidi mawili. Kwa maana ya kwamba tunapoandaa bajeti ni lazima tuzingatie mambo ambayo yanatokana na bajeti ile. Tunaona kabisa kwamba bajeti hii haikuweza kutekelezwa kwenye baadhi ya miradi ya maendeleo kwa sababu nchi ilikwenda kulipa madeni. Tunakubali kulipa madeni ni wajibu, lakini tuna wajibu wa kuangalia bajeti zetu tunavyozipanga ni lazima wataalam watusaidie ku-forecast yale madeni ambayo Serikali inatakiwa iyalipe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulitoka kwenye bajeti ya trilioni 22 tukaenda kwenye bajeti ya trilioni 29 kwa mwaka 2016/2017. Tulikwenda kwenye bajeti kubwa, kinachonishangaza ni kwamba, kumbe kulikuwa kuna madeni ambayo yako matured. Kama kungekuwa kuna madeni yako matured ambayo yamekuwa ni kikwazo cha Serikali kupeleka pesa kwenye miradi na kulipa madeni ya ndani na ya nje, basi inabidi wataalam wachunguze na waangalie wawe tayari kuisaidia Serikali, kutusaidia Wabunge tunapokwenda kupitisha bajeti basi tuweze ku-consider yale madeni ambayo Serikali inakwenda kuyalipa. Bila kufanya hivyo tutapanga bajeti, tutakutana na madeni katikati, tutalipa madeni, tutashindwa kupeleka pesa kwenye miradi ya maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitizama katika miradi ya maendeleo Serikali imepeleka fedha kwenye miradi ya maendeleo kidogo sana. Mfano mzuri ukiangalia kwenye kipaumbele cha Serikali ambayo tunasema Serikali ya viwanda, bajeti iliyopelekwa katika Wizara ya Biashara na Viwanda ni asilimia 10 tu ya bajeti iliyokusudiwa. Ukitizama kwenye Wizara inayohusiana na masuala ya mazingira chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais, pesa ya maendeleo ni asilimia sifuri, haijaenda pesa yoyote. Sasa hivi ni vikwazo vinatukwamisha, inabidi kweli Serikali tujizatiti tuhakikishe tunapeleka pesa za maendeleo kwa wakati kama ilivyopangwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuongelea vilevile masuala ya vyanzo vya mapato. Suala la kodi, kuna kodi hapa ambazo zililalamikiwa sana, mfano kodi ya VAT kwenye utalii. Mimi nafikiri Serikali ijipime, Wabunge tunapozungumza na yenyewe Serikali itusikilize, siyo kukaa mnasikiliza tunaandika halafu tunakwenda kutoza kodi kwenye utalii. Utaendaje kuwatoza watu kwenda kuangalia nyumbu na swala unawawekea VAT! Mtu anayekwenda kuangalia nyumbu na swala hakuna haja ya kumuwekea VAT. Tuondoe VAT tuweze ku-invites watalii wengi waweze kutembelea katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona pato linavyozidi kuongezeka kwenye utalii tukiwaondolea kodi ya VAT tutakaribisha watalii wengi, wata-flow kwa wingi. Tuangalie na nchi ambazo tunashindana nazo kama Kenya wao wanafanya nini? Tujifunze kutoka kule ili na sisi tuweze kufanya inavyostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kodi hiyo kuna suala la VAT kwenye capital investiment. Tunasisitiza watu tuondoe kodi kwenye kilimo, tunasisitiza tuondoe kodi kwenye vifaa vya kilimo kwa maana ya kwamba watu tulime zaidi tupate mazao mengi. Kwa mfano, mtu amelima akaenda kuuza mazao yale kwa wale watu ambao wanachakata mazao yetu, unakuta kwa mfano mtambo wa kutengeneza juice au mtambo wa kusaga unga, ile investiment anayoileta Mwekezaji, kwa mfano, Ndugu Bakhresa pale alitaka kuleta mtambo wa dola milioni 100, lakini akaukutana na VAT! Hebu piga asilimia 18 ya VAT ya milioni 100 ni shilingi ngapi! Ndipo alipoamua kuondoa mtambo huu na kuupeleka nchi jirani ambako hawana hiyo kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni lazima tu-harmonize hizi strategy zetu. Kama tumeamua kuondoa VAT kwenye vifaa vya kilimo basi tuondoe kodi kwenye msururu mzima ambao hadi kwenye uchakataji wa bidhaa zile. Sasa kama wewe umeondoa kodi umemu-encourage mtu alime akalima mahindi, unamuwekea kodi mtu anaye-invest anayeweza kwenda kusaga unga na ku-pack, maana yake ni nini? Tunapoamua kuondoa basi tuangalie flow nzima ili tuweze ku-encourage wawekezaji waweze ku-produce zaidi na kuweza kupata kipato cha kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kodi hiyo kuna kitu kinaitwa single customer territory, mikataba ya single custom, tumepigia kelele. Ni kweli Tanzania sisi ni wanachama wa East African na tumekubaliana nchi zote za East Africa kuwa na single customer territory kwa maana ya kutoza kodi, kwa niaba ya nchi nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu mkataba uko kwa nchi za East Africa, kwa nchi ya Kongo haupo, iIna maana Mkenya anaweza akafanya biashara na Mkongo bila kumtoza kodi. Ina maana sisi tunamtoza kodi mfanyabiashara wa Kongo Dar es Salaam, tukimtoza kodi ina maana kwamba huyu mfanyabiashara tunamu-encourage aende kwenye bandari za pembeni. Wamekwenda Beira, wamekwenda Durban, wanakwenda Mombasa, wametukwepa katika bandari yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya tuyatizame kwa kina, tunapoamua kutafuta vyanzo vya mapato tusione aibu. Tusiingie mikataba ambayo haina tija! Huu Mkataba wa single customer territory kati ya Tanzania na Kongo naomba muutizame upya, ikibidi muuondoe. Kwa nini tuwakusanyie Kongo zile pesa? Kuna malalamiko wameshaanza kusema kwamba, kumbe hata pesa zenyewe zinapokwenda kwenye mikono ya Serikali ya Kongo haifiki kwa wananchi! Sasa sisi tunawasaidia nini? Ina maana badala ya kuwasaidia Wakongo wote tunawasaidia Wakongo wachache!
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tuingie kwenye mkataba kama huo na unakimbiza wateja wetu wasije katika bandari yetu! Tuuondoe huo mkataba, ikiwezekana hata kesho tuuondoe ili kusudi tu-encourage biashara ya kongo na Tanzania ili bandari yetu irudishe uwezo wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naongelea kuhusu vyanzo vipya. Katika kuongelea vyanzo vipya vya kodi ni lazima tujali viwanda vyetu na viwanda vipo vikubwa na viwanda vidogo. Viwanda hivi haviwezi kufanya kazi kama hatuna umeme wa uhakika, hatuna umeme wenye bei nafuu. Umeme wetu bado ni tatizo kubwa katika uchumi wa nchi yetu. Tunauza umeme kwa bei kubwa mno na bado umeme wenyewe hauna quality nzuri, unakatika mara kwa mara. Umeme unapokatika ni hasara kubwa sana kwa wawekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulitembelea EPZA pale kuna jamaa wanatengeneza hizi smart card, kadi za benki na nini, wanatengeneza kwa ajili ya kuwauzia makampuni ya simu, wanauzia mabenki, hizi unaziona visa card zinatengenezwa pale EPZ Dar es Salaam. Wanatumia system kubwa ya computer and very sophisticated. Ukiukata umeme mara moja wana-recover ile system kwa siku saba. Kesho akiona kuna nchi nyingine ina umeme wenye quality nzuri huyu mtu atatuhama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni matatizo makubwa. Ilipeni TANESCO deni lake, walipeni waweze kuweka infrastructure nzuri. Tunaipongeza Serikali mmepeleka umeme hadi vijijini sawa kabisa mmepeleka umeme hadi vijijini, lakini quality ya umeme bado ni tatizo katika nchi yetu. Umeme kwa kweli ni tatizo, tusipo-improve umeme hii Serikali tunasema tunaenda kwenye viwanda, tutashindwa kwa sababu bila energy ya kutosha ni tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niende kwenye kilimo. Asilimia 70 ya Watanzania tumejiajiri kwenye kilimo, lakini kilimo chetu hakina tija, kilimo na ufugaji ndiko kwenye ajira kubwa katika nchi yetu. Hebu tuangalie namna gani ya kuwasaidia wakulima, sasa hivi bei ya mbegu ya mahindi inauzwa shilingi 13,000 mfuko wa kilo mbili! Shilingi 13,000 mwananchi wa kawaida mbegu kununua shilingi 5,000 kwa kilo, karibu shilingi 6,000 ni shida kununua, hawezi kununua. Ni bora Serikali mka-subsidize hizi mbegu mkatoa na mkawalipia wakulima wakanunua mbegu kwa bei nafuu ili waweze kupanda na kupata mazao mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachokifanya sisi kwetu kule Usukumani mtu akilima mwaka huu anahifadhi na madebe mawili/matatu ya mbegu, zile mbegu hazina ubora! Tunataka special mbegu ambazo mtu ukipanda unapata mavuno ya kutosha, sasa zile mbegu ni bei juu mno. Kama mnataka kweli wananchi waweze kulima wapate mazao ya kutosha punguzeni bei ya mbegu, Serikali iingilie kati i-intervene m-subsidize mzilipie kodi hizi mbegu. Wako watu wachache wanaozalisha hizi mbegu muwape mikataba wazalishe mbegu, muwasambazie wananchi kwa bei nafuu waweze kupata mazao mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kwa wanyama ng‟ombe tulionao hatuna ng‟ombe wa maziwa wala hatuna ng‟ombe wa nyama. Tuna indigenous ng‟ombe wetu ambao ukimwangalia amekondeana, tuna ng‟ombe wengi na ukame huu wengi wanakufa sasa hivi. Hatuna ng‟ombe ambao wana good quality kwa maana ya kula nyama, hatuna ng‟ombe kwa maana ya kupata maziwa bora. Tunaomba mbegu mpya, tunazungumza kila siku Serikali iingilie kati mlete mbegu za ng‟ombe wapya wenye kuweza kutoa nyama nyingi, ng‟ombe wapya wenye kuweza kutoa maziwa mengi ya kutosha ndipo tutaweza kuwainua wananchi wetu na kuweza kuwaingiza katika uchumi wa kati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kusema kwamba bado Serikali ina kazi kubwa ya kufanya. Nawashukuru kwa kazi kubwa mnayoifanya kwa kweli, tumeangalia kwenye elimu, elimu bure, pesa zinakwenda, hivyo vitu tunasema tunatoa pongezi za dhati kabisa, muendelee kufanya kazi nzuri. Tunaona miradi mingine inakwenda ya barabara, tunajengewa barabara, lakini miradi ya maendeleo tunaomba Serikali iwalipe watu wanaoidai ili kusudi mzunguko wa pesa urudi na tuweze kupata mzunguko wa kutosha na watu waweze kulipa kodi na Serikali iweze kupata mapato ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi.