Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Dr. Philip Isdor Mpango

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kushukuru sana kwa kuongoza kikao hiki vizuri, lakini pia kwa kunipatia nafasi niweze kuchangia. Vile vile niruhusu niipongeze sana Kamati ya Bajeti chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia na Makamu Mwenyekiti, Mbunge wa Kalambo kwa kazi nzuri sana wanayofanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema kutoka moyoni kabisa, Kamati hii ni very pragmatic, very resourceful na wamekuwa wanatusaidia sana. Serikali nipende kuahidi kwamba itazingatia maoni na mapendekezo ambayo wametupatia katika uandaaji wa bajeti inayokuja na tutaendelea kuzifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nizungumzie mambo tu machache. Kwanza kulikuwa na hoja ya washirika wa maendeleo kutotoa fedha na kwamba sababu zake hazifahamiki. Sababu za washirika wetu wa maendeleo kutotoa fedha ni nyingi sana. Mojawapo kwa kweli ni yale masharti yenyewe ya kutoa fedha. Yako masharti ambayo hatukubaliani nayo na tunaendelea kuzungumza na wenzetu ili watuelewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ngoja nitoe tu mfano; kwa mfano tulikuwa tunaomba fedha kwa ajili ya kuboresha bandari yetu ya Dar es Salaam, lakini moja ya sharti tulilopewa ni kwamba ni lazima sasa TPA wajiondoe kwenye kuendesha Bandari badala yake aje mtu binafsi kuendesha bandari yetu. Hatukubali hilo Waheshimiwa Wabunge na sisi tunafanya kwa maslahi ya Taifa letu. Tumeshakuwa na uzoefu wa kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mengine ambayo pia wanatusukuma huko ambayo sio sawasawa, ni kinyume cha mila na desturi za Kitanzania na hatuwezi kuzikubali. Kwa hiyo, hiyo ni mojawapo. Pia kuna ukweli kwamba kuna mabadiliko katika mtazamo wa Serikali nyingi ambazo zimeingia madarakani hususan katika nchi za Ulaya. Tumekuwa na majadiliano sisi bado tunadhani kwamba general budget support ndiyo njia nzuri ya wabia wetu kutusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wao wamebadili msimamo, wanasema wapeleke fedha moja kwa moja kwenye miradi. Tulishakuwa huko, tunajua changamoto za wao kupeleka fedha kwenye miradi wanayochagua kwenye mikoa wanayochagua badala ya kutupa sisi kama Watanzania nafasi ya kusema tumepungukiwa zaidi huku sisi tupeleke kule. Hata hivyo, tunayajadili na tumeunda Kamati maalum ya wataalam kutoka nje na ndani ambao wanaangalia jinsi dialogue yetu inavyokwenda. Naamini kwamba mwezi huu tutakuwa na kikao cha pili, naamini tutafika mahali ambapo tutaelewana vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la msingi Waheshimiwa Wabunge, naomba tena kusisitiza, khanga ya kuazima ni tatizo. Lazima tuielekeze nchi yetu kujitegemea kama Baba wa Taifa alivyotufundisha. Hili ni jambo la msingi sana, mnaona tunapata wakimbizi tunahangaika miaka yote lakini wao wakipata wakimbizi kidogo wanakimbiza fedha zao kwa wakimbizi wa upande mwingine. Kwa hiyo, kwa kweli tujielekeze kujitegemea na ndiyo maana tukazanie zaidi kujenga mapato yetu ya ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme mengine haraka haraka. Kwa upande wa takwimu za mfumuko wa bei, wale ambao wana mazoea kuzitazama umegawanyika sehemu mbalimbali. Kuna mfumuko wa bei wa jumla lakini kuna mfumuko wa bei wa chakula lakini pia kuna non food inflation na ukizitazama hizi ziko bayana kabisa kwamba mfumuko wa bei ya chakula daima umekuwa ni mkubwa kuliko mfumuko wa bei wa jumla na sababu kubwa ni kwamba mfumuko wa bei wa Taifa letu unasukumwa zaidi na upatikanaji wa hali ya chakula lakini pia bei za mafuta. Kwa hiyo, hiyo iko wazi tu na nadhani ni mazoea kuziangalia zile takwimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa upande wa kuhusu makampuni ya mawasiliano kujisajili katika soko letu la hisa. Kwenye taarifa ambayo niliisoma humu Bungeni, muda haukuniruhusu lakini mkiisoma ile taarifa kuna kipengele nafikiri ni ukurasa wa 15 kinaeleza vizuri juu ya hatua iliyofikiwa kuyataka makampuni yetu ya mawasiliano kujisajili katika soko la hisa kwa mujibu wa sheria. Nitaomba wasome.
Mheshimiwa Mwenyekiti, limesemwa sana kuhusu Sekta yetu ya Kilimo. Ni kweli growth ya Sekta yetu ya Kilimo imekuwa hairidhishi na nimelisema hili mara kadhaa ndani ya Bunge, lakini ni muhimu tuwe clear. Ningependa kama ingewezekana kama ulivyosema wewe, suala hili la uchumi pengine tukapata muda kweli wa kulijadili labda hata kwenye semina au hivi na Wabunge wakaja wakashiriki kwelikweli kwa maslahi ya Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano; kilimo, tukisema bajeti pekee ya kilimo iongezwe tutabadilisha kilimo sio sawasawa. Najua Maputo Declaration inataka tupeleke 10% ya bajeti iende kwenye kilimo lakini kilimo kinachosemwa ni nini? Wataalam wanasema ili kilimo kiweze kufanya vizuri unahitaji pia sekta nyingine ambazo sio za kilimo nazo zifanye vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa mfano; tunapozungumzia mbolea, mbolea inazalishwa viwandani, unapozungumzia performance ya kilimo lazima uzungumzie upitikaji wa mazao kutoka shambani maana yake ni barabara. Unapozungumzia wataalam wa kilimo maana yake lazima uzungumzie Sekta ya Elimu. Kwa hiyo, ni lazima tuwe waangalifu, sio bajeti pekee ya kilimo. Kuna mambo mengi ambayo ndiyo yanakwenda kuamua performance ya kilimo iweje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa yako mengine ambayo ni ya msingi. Bajeti yetu ya umwagiliaji ikoje, bajeti yetu ya utaalam ikoje? Incentives, hata za kikodi kule kwenye kilimo zikoje? Lazima tuliangalie kwa upana wake ili kweli tuweze kuja na mkakati mzuri kwa ajili ya kuboresha Sekta ya Kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yalisemwa hapa najua Naibu Waziri amelisema kwamba ukuaji wa deni la Taifa, tumekazania zaidi kukopa ndani, kwa hiyo tuna–crowd out private sector. Nisisitize tu, Serikali haina maagizo maalum kwamba tulipe wadeni wetu wa nje peke yake. Nililieleza wakati natoa taarifa Bungeni, ni lazima tuwe makini sana na kuhakikisha kwamba hatuachi kulipa halafu madhara kwenye uchumi yakawa makubwa zaidi. Kwa hiyo, there is a delicate balance that we need to do na ndicho tunachojaribu kufanya. Madeni haya ndugu zangu, mengine tumewapa taarifa, madeni haya mengine tunayolipa yamekopwa toka uhuru, kwa hiyo, hilo ongezeko linaloonekana ni cumulative sio kwamba ni kwa sababu tu imeongezeka katika Awamu hii ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yalisemwa pia kuhusu kwamba tuangalie nchi ili iendelee inahitaji Sound Fiscal and Monetary Policies, Revenue Policies na Good Governance. Nafikiri niseme tena, inabidi tuwe waangalifu, country context na specificity ni muhimu sana. Tanzania yetu ya leo sio Malaysia, wala sio Botswana, wala Korea. Kwa hiyo, ni muhimu sana na wale ambao mnasoma hivi vitabu ni ukweli pia kwa mfano Dkt. Mahathir Mohammed was a dictator! Ndiyo ukweli wenyewe, angalieni South Korea, Park Chu Hi ambaye ndiye aliibadilisha Korea alikuwa dictator, kwa hiyo msiseme tu kwamba good governance and stability ndiyo msingi pekee wa ukuaji wa uchumi katika Taifa. Kwa hiyo, ni muhimu sana tuwe waangaifu na hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lilisemwa pia hapa kwamba pato la Mtanzania linapungua.
Pato la Mtanzania linapungua, si kweli! Pato la wastani la Mtanzania mliangalie vizuri, tumetoka kwenye dola 350 sasa tumefika dola 980, lakini ni vizuri kuzingatia volatility ya exchange rate, kama unatazama tu lile pato la Taifa kwa shilingi, halafu unagawa kwa exchange rate kuna miaka ambayo kwa wastani, exchange rate yetu imeporomoka na hivyo wastani unaonekana kushuka, lakini trend ya pato la Taifa inaongezeka kwa hakika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa mapitio ya mfumo wa kodi, naomba nitumie nafasi hii, kuwaomba sana Waheshimiwa Wabunge kwamba kuanzia mwezi huu sasa tutaanza kujadili pale Wizarani mapendekezo ya wadau wote wa kodi nchini, ambayo wamependekeza wengine wameleta. Hamjachelewa yeyote aliye na mapendekezo namna ya kuboresha mfumo wa kodi awasilishe mwezi huu tutaanza kufanya kikao cha kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vipaumbele, nilijaribu kulieleza kwenye moja ya vikao vilivyopita, naomba nisisitize sana kwamba kusema juu ya kuwa na vipaumbele vichache ni rahisi sana, lakini kuvitekeleza katika mazingira ya nchi maskini kama Tanzania ni jambo gumu kweli. Nakumbuka nilimtania Mheshimiwa Silinde hapa, nikasema nitaanza kupunguza vipaumbele vinavyogusa jimbo lake lakini ni ukweli tuna mahitaji makubwa kwenye maji, elimu, kila mahali. Kwa hiyo, kuweza kusema kwamba tujikite kwenye eneo moja tu la reli katika mazingira ya Tanzania haitawezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Naibu Waziri alieleza juu ya ukusanyaji wa kodi ya majengo, naomba tu niseme kama alivyoeleza kwamba tumeanza kukusanya. TRA imeanza kukusanya mwezi wa Kumi baada ya kukamilisha maandalizi na kuanzia mwezi wa Kumi mpaka Desemba mpaka sasa zimekusanywa sh. 4,762,369,261. Hata baadhi ya miji ambayo inasemekana hamna chochote si kweli, kwa mfano Kinondoni peke yake kwa hii miezi michache imeshakusanya sh. 1,229,821,142, niseme Arusha Sh. 462, 527, 906, Ilala Sh. 999,193, 088 na takwimu tayari zipo kwa kipindi hiki, kwa hiyo kazi imeanza. Ilikuwa ni muhimu sana kufanya maandalizi stahiki ambayo yanagusa vitu vingi ili tuhakikishe kwamba tunakwenda sawasawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MWENYEKITI: Malizia tu Waziri.
WAZIRI WA MIPANGO NA FEDHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, okay, labda niseme tu moja la mwisho kwamba, kwenye tathmini ya deni la Taifa, tazameni kidogo kwa uangalifu taarifa ambayo niliwaletea. Tuna vile viashiria vya uhimilivu wa deni, ni pamoja na deni la nje, uwiano wake na uuzaji wa bidhaa za nje kwa maana ya foreign exchange earnings lakini pia tunaangalia deni la nje uwiano wake na mapato ya ndani. Kwa hiyo, siyo kwamba tunaangalia tu uwiano relative to GDP. Ahsante.