Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalambo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE - MAKAMU MWENYEKITI WA KAMATI YA BAJETI: Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kukushukuru kwa fursa nyingine tena, naomba niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote ambao walipata fursa ya kuchangia kwa kuongea walikuwa jumla ya Wajumbe 19 na waliochangia kwa kuandika walikuwa jumla 17, jumla yake ilikuwa ni 36.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ulivyoanza kusema asubuhi, umuhimu wa hoja hii nzito, naamini na wewe mwenyewe ni shahidi leo siku ya Jumamosi nisingependa kupoteza muda mwingi wa Waheshimiwa Wabunge, lakini wewe mwenyewe unaona jinsi ambavyo wametoa msukumo wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla naomba nikumbushe, wewe ni shahidi jinsi ambavyo kulikuwa na kazi kubwa ya uanzishaji wa Kamati ya Bajeti na uanzishwaji wa Sheria ya Bajeti na misingi ambayo ilikuwa imewekwa ili tuondokane na ile hali ambayo Bunge lilikuwa linafanya kama rubber stamping waliita watu hivyo. Tukasema tuondoke hapo, tufike mahali ambapo Bunge litashiriki katika mchakato mzima wa kuandaa bajeti na utekelezaji wake. Ombi ambalo ni vizuri na Serikali bahati nzuri wanasikia, isingependeza tukarudi nyuma tulikokuwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, itakuwa ni vizuri kwanza tukajengea uwezo Ofisi ya Bajeti na sitarajii, maana hili limeanza kujitokeza pale ambapo Bunge linataka kuwa na uwezo wake mzuri sasa kumekuwa na tabia hata ule uwezo mzuri, wale watumishi wazuri ambao wanapikwa na Bunge wanaanza kuhamishwa wanapelekwa upande wa Serikali, haitapendeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri tukawa na uwezo mkubwa, twende na wengine ambao Mheshimiwa Mwenyekiti, ni shahidi ukienda nchi kama Uganda, Kenya inafika mahali ambapo Kamati ya Bajeti, inakuja na bajeti mbadala ili kulinganisha na ile bajeti ambayo inaletwa na Serikali, huko ndiko ambako tunatarajia kwenda. Kwa hiyo, itakuwa si vizuri kama Serikali watatumia fursa ya kuanza kuchukua vile vichwa vizuri ambavyo vinatengenezwa wakapeleka upande wa kwao. Hilo lilikuwa la jumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kulisema hilo na baada ya kutambua Wajumbe waliochangia, kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, naomba kwa uchache nishukuru Serikali kwa sababu iko hapa wamesikia na mengi kimsingi na wao wamekiri kwamba ni ya kwenda kuyafanyia kazi, nitaje machache na kwa ujumla Waheshimiwa Wabunge waliochangia kwa kuongea kama watapenda niwataje majina lakini kwa kuokoa muda, naomba nisitaje hata wale ambao walichangia kwa kuandika naomba nisitaje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya masuala ambayo yamesemwa kwa kiasi kikubwa ni vizuri nikasema. Kimsingi wajumbe wengi wamesisitiza juu ya suala zima la kulipa deni la TANESCO. Sisi sote ni mashahidi, uko umuhimu sana wa kuhakikisha kwamba deni hili linalipwa maana tunaamini Tanzania ya viwanda bila kuwa na uhakika wa umeme hatuwezi kufika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia kuhusiana na suala zima la ushiriki wa private sector (PPP). Si rahisi kwamba masuala yote ya maendeleo tutaiachia Serikali kwa maana ya ile miradi mikubwa. Kwa hiyo, ni vizuri kama ambavyo Waheshimiwa wengi wamechangia kwamba fursa iwepo na itumike kuhakikisha kwamba private sector inashiriki kama injini ya kukuza uchumi wa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe ni shahidi, tumekuwa tukiongea muda mrefu tangu ukiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, mapendekezo ambayo yaliletwa Serikalini juu ya kuanza ujenzi wa barabara, kutoka Dar es Salaam kufika Morogoro na kwa kuanzia Chalinze zile njia tatu. Taarifa ambazo zilikuwepo ni kwamba private sector walikuwa wako tayari. Sasa hadithi imekuwa ya muda mrefu ni vizuri sasa Serikali ikaenda kwanza kutenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, katika Wajumbe wengi waliochangia yamesemwa maneno kwamba kuna hizi kauli za kutoka kwa Mheshimiwa Rais, anatamka pesa inapatikana. Niombe Waheshimiwa pamoja na nia njema ni vizuri tukaenda kutazama budget frame kwa ujumla wake, hiki ambacho kinatamkwa na Mheshimiwa Rais ukienda kwenye bajeti utakuta kipo. Siyo kwamba anaamka tu anatamka halafu pesa inapatikana. Mifumo ya bajeti iko sahihi. Kwa hiyo, ni vizuri kwa nia njema kwa sababu haya ambayo yanafanywa ni kwa ajili ya Watanzania ni vizuri tukafuatilia utaratibu wa bajeti twende kwenye vitabu, turejee tujue hayo ambayo yanatamkwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wachangiaji wengi wameongelea kuhusiana na suala zima la kilimo ambalo na Kamati ya Bajeti kimsingi tumesisitiza kwamba ili twende kwenye Tanzania ya viwanda ni vizuri uwekezaji ukawekwa wa kutosha kuhusiana na suala zima la kilimo. Bahati nzuri Serikali imesikia, hii habari ya kwamba mvua zisiponyesha mara moja tu tunaanza kuwa na wasiwasi hatuwezi kwenda tukasema ni Taifa la kwenda kwenye uchumi wa kipato cha kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ziko nyingi, kama mtu hakuchangia hoja asitarajie kusikia hoja yake ikijibiwa, hayo ambayo nayajibu ni yale ambayo yamechangiwa kwa ujumla na yakapewa uzito na bahati nzuri, hiki ninachokisema nimekisomea. Kwa hiyo, sikukiokota mitaani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto za kibajeti, Wajumbe wengi wamechangia. Wabunge wameainisha kuwa katika taarifa ya Kamati hali ya uchumi kwa mujibu wa taarifa ya kutoka Benki Kuu na mwenendo wa mfumuko wa bei, Serikali inashauriwa kuhakikisha kwamba inakaa chini na kutathmini mwelekeo uliokuwa umetolewa awali na hali ya sasa. Ni vizuri tukaanisha ili tukapata namna ambavyo tunaenenda kama tuko kwenye right track. Hili niombe Serikali kujisahihisha si vibaya, tutazame wapi tuna-miss point ili isije ikafika mpaka dakika ya mwisho ndio tukajikuta tume-miss kile ambacho tulikitarajia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja kuhusiana na mafunzo kwa Bunge zima. Imechangiwa na Wabunge wengi ni hoja ya msingi ni vizuri Serikali mkajipanga maana exposure ni jambo la msingi sana. Pamoja na ufinyu wa bajeti lakini ni lazima tuhakikishe kwamba Wabunge wanajengewa uwezo ili wafanye kazi yao ya kikatiba ya kuhakikisha kwamba wanaisimamia na kuishauri Serikali kwa mujibu wa Katiba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, imeongelewa hoja kuhusiana na Serikali kukopa ndani na sisi Kamati tumeliona, tukaishauri Serikali. Serikali ina muscles za kutosha ina uwezo mkubwa wa kwenda kutafuta mikopo nje, ni vizuri hii mikopo ya ndani tukaiachia sekta binafsi ili wahangaike na hizi fedha ambazo watazipata kwa urahisi. Tumeiomba Serikali iharakishe zoezi la kufanya sovereign rate ili waende kutafuta mitaji huko nje kwa sababu inapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la shilingi milioni 50 ya kila kijiji, wewe ni shuhuda ulishiriki wakati tunajadili na tukakubaliana kwamba pesa hizi zinazotolewa si pesa ya ruzuku, ni pesa ambayo ni ya mkopo na pesa ya mkopo lazima ujihakikishie kwamba huyu unayemkopesha anaenda kuzirejesha vipi kwa sababu pesa hii ni revolving fund. Tunaiomba Serikali iharakishe mchakato ili pesa hizi zikitolewa zikifika kwa wananchi ziweze kurejeshwa ili wananchi walio wengi, Watanzania wengi waweze kupata fedha hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, muda hautoshi naomba sasa nijikite katika maazimio ambayo tunaomba Bunge lako liiitake Serikali kwenda kuyatekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Bunge lako Tukufu lipokee maoni na mapendekezo ya Kamati kuwa Azimio la Bunge kwa utekelezaji wa Serikali ili taarifa hiyo ije iletwe namna ambavyo Serikali imetekeleza na kwa kuzingatia ushauri mzuri ambao umetolewa na Waheshimiwa Wabunge kwa kuzingatia pande zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.