Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia machache.
Kwanza kabisa nianze na pongezi, natoa pongezi kwa Waziri wa Nishati na Madini, pamoja na Naibu Waziri wamefanya kazi nzuri sana. Naibu Waziri alikuja mpaka kwenye jimbo langu akieleza mpango mzima wa Serikali wa umeme vijijjini. Ukweli katika ziara yake ilikuwa
nzuri sana na wanachi wanakupongeza sana walikuelewa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikinukuu speech za Naibu Waziri ambazo zilieleweka kwa kila mtu. Nilipenda sana usemi wake, alisema masuala ya umeme sio kwamba unapelekwa umeme halafu wananchi wanaanza kuangalia nguzo, kwa sababu tumeona kuna vijiji vingi sana
vinakuwa umeme umepita hasa huu umeme wa Gridi ya Taifa, vijiji vingi sana vinakuwa havijapewa umeme umepita tu pale. Lakini akasema kwamba Serikali itaangalia kwamba vijiji vinapewa umeme, umeme unaenda kwenye nyumba za watu, hiyo niliipemda sana na
akasema kwamba, vitongoji vyote vinapewa umeme, akasema kata zote zitapewa umeme, bahati nzuri sana alisema tarehe 15 Desemba, makandarasi wanaanza kusaini mikataba halafu wanaanza kazi ya Awamu ya III, umeme wa REA vijijini unaanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, hizi speech ni nzuri sana, naifurahia sana Serikali kwa mpango mzuri na bahati nzuri katika quotation yake ni kwamba zahanati zote zitapewa umeme, shule za msingi zote zitapewa umeme, vituo vya afya, pamoja na hospitali, hilo ni jambo zuri sana. Sasa niiombe tu Serikali kwa ushauri wangu kama tumepanga mpango umekamilika na tumeshawaambia wananchi, kwa mwaka huu wa fedha ambao tunaingia mwaka 2017/2018 basi tufanye utekelezaji ambao unaonekana kwa wananchi, isionekane tumepiga speech nzuri
halafu hazitekelezeki. Hii itatusaidia sana na wapiga kura wetu watatusaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, kwenye jimbo langu nina kata 16, katika kata 16 ni kata sita tu zina umeme, ina maana kata 10 hazina umeme. Nina vijiji vingi sana, nikianza kuorodhesha hapa naweza nikachukua muda wote kwa kutaja vijiji tu. Sasa kwa sababu Naibu
Waziri alikuja kule aliahidi wananchi, naendelea kuiomba Serikali kwamba vile vijiji vyote vya Jimbo la Mufindi Kusini, ambavyo havijapatiwa umeme kwenye mwaka huu wa fedha angalau katika kata 10 tufikie hata nusu. Wakipata kama kata tano kwa mwaka 2017/2018 kwa kweli
nitaishukuru sana Serikali. Hiyo naomba sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile leo tulikuwa tunajadili kwenye semina vifo vya mama na mtoto, na ni kweli sababu kubwa inaonekana kwenye zahanati na vituo vya afya hakuna umeme. Na unaweza ukaona mtoto amezaliwa labda hajafikia umri wake, mtoto anatakiwa
aongezewe labda oxygen kijijini hauweze kuongezewa oxygen kama hakuna umeme. Imekuwa ni tatizo kubwa sana. Kuna zahanati nyingine wanatumia kule zile taa tunaita koroboi, sasa hilo Serikali lazima iangalie vizuri sana ni tatizo kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili nakuja kwenye masuala ya miundombinu. Kwenye Jimbo la Mufindi Kusini kila siku huwa ninasema, sisi maeneo yetu ni maeneo ya mvua sana, bahati nzuri sana namuomba Waziri wa Ujenzi aangalie sana ahadi ambazo zilitolewa na Rais
na aangalie zile ahadi ambazo ziko kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Kuna barabara ambazo, upembuzi yakinifu ulishakamilika tayari. Hazihitaji kwamba tunaanza kuandaa upembuzi yakinifu, upembuzi yakinifu ulishakamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa mfano kuna barabara hii ya Nyororo mpaka Mtwango pale kwenye Jimbo langu la Mufindi Kusini, kuna barabara kutoka Mafinga mpaka Mgololo, kuna barabara ya kutoka Kasanga mpaka Mtambula. Hizi barabara zimeandikwa mpaka
kwenya Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwamba watatengeneza kwa kiwango cha lami, na kuna sababu sio suala la kutengeneza kiwango cha lami lazima kuwe na sababu kwa nini upeleke barabara kule? Kwenye Jimbo langu la Wilaya ya Mufindi kuna viwanda vingi sana, na
vile viwanda siku zote nasema, Pato la Taifa tunategemea katika viwanda vile.
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri Tanzania tumesema Tanzania ya viwanda, kuna viwanda vingine inabidi vifufuliwe au vijengwe vipya. Sisi kule hatufufui viwanda, viwanda viko tayari lakini tuna matatizo ya barabara. Na ninavyoongea saa hizi, mvua kule inanyesha sana, sisi hatuna uhaba wa mvua. Tumepewa neema na Mwenyezi Mungu, lakini zile barabara pamoja kwamba; tumeimarisha kwa kiwango cha kokoto inatakiwa tuweke kiwango cha lami. Bahati nzuri, kwenye Mpango wa Mwaka 2014/2015 upembuzi yakinifu mimi walishakamilisha
barabara ya Nyororo kilometa 40. Sasa naomba kwenye mwaka huu wa fedha ambao ni 2017 tunaounza kesho kutwa, kwenye bajeti ninaposoma nione kwamba tayari Wizara imejipanga kwa ajili ya kujenga ile barabara kiwango cha lami kama ilivyoahidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine nije kwenye masuala ya mawasiliano. Mawasiliano ndio yanayounganisha nchi, mawasiliano ndio inayounganisha vijiji, kata, na vitongoji. Nakumbuka mwaka 2013/2014 kipindi kile Waziri wa Mawasiliano alitoa taarifa alitupatia na barua kwamba minara ya simu itajengwa kwenye vijiji vile ambavyo hakuna minara ya simu, bahati nzuri na mimi nilipewa. Kuna kata moja ya Idete, ile kata kutoka Mafinga Mjini mpaka uikute hiyo kata ni kilometa 160. Kata ile ina vijiji vikubwa tatu, kuna Idete, Holo na Itika, ni vijiji vikubwa, yaani kijiji hadi kijiji sio chini ya kilometa 40 lakini hakuna mnara hata mmoja, hakuna mawasiliano.
Naomba vijiji vile vipewe mawasiliano kama waziri alivyoahidi wa nyuma; kwa sababu Waziri hata ukibadilishwa wizara, ofisi inakuwepo naomba vijiji vile vya Idete, Holo na Itika viweze kujengewa minara. Na kuna kata nyingine, hii kata ya Ihoanza ambayo hiyo kata tunapakana
na Mkoa wa Mbeya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Kuna vijiji vingine kule kwa mfano kijiji cha Katangwa, Iyai hawana mawasiliano kabisa na makao makuu ya wilaya kwa sababu hakuna minara ya simu.
Naomba na ile sehemu yote ambayo Waziri niliwahi kumpa majina basi apelike huduma hii ya mawasiliano kama alivyoahidi. Hii itatusaidia sana kuhakikisha kwamba huduma kwa wananchi tunafikia kwa urahisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna watu wanaweza kuugua kijijini kule hakuna mawasiliano hata ya hospitali, wakinamama wengine, wanajifungulia porini au wanajifungulia nyumbani kwa sababu hakuna mawasiliano hata wakipiga simu tukajua kwamba kuna gari inabidi
ipelekwe kule ambulance kutoka Mjini Mafinga ni kilometa karibu 120 na kama hakuna mawasiliano basi tunampoteza mama huyu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali iwekee mkakati kuhakikisha kwamba sehemu zote nilizotaja zinaweza kujengewa minara ya simu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga hoja mkono ila naomba Serikali ifanye utekelezaji, ahsante sana.