Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nkasi Kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii namshukuru pia Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima, naungana na wenzangu kuchangia katika taarifa za Kamati hizi mbili. Mimi ni mmoja kati ya Mjumbe wa Kamati ya Nishati na
Madini. Nianze na taarifa hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Waziri na watendaji wake wote pamoja na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanayoifanya na kwa hakika inaonekana kwa Watanzania, isipokuwa kitu kinachokwamisha ni pesa zinazotolewa zinawafanya majukumu yaliyopangwa yasifikiwe kwa
wakati, lakini juhudi tunaiona. Kwa hiyo, niishauri Serikali kuhakikisha kwamba katika eneo la usambazaji umeme na kwa vile tumejitangazia kila mahali umeme ufike pawepo nidhamu ya utoaji wa fedha kuendana na utaratibu wa kibajeti kwa mwaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu wananchi tulishakubaliana kwamba tunatoa tozo kwenye mafuta, pesa ambayo ingeenda kwa mwananchi, tunamkamua ili pesa iende kwenye usambazaji wa umeme. Kwa hiyo, hatuna sababu ya kukosa pesa kwa jukumu hili. Lakini nisifie kwamba katika usambazaji wa umeme sisi Wilayani Nkasi tumepata umeme katika vijiji vya Kundi, Kibande, vijiji vyote mpaka kufika Namanyere kwa barabara hiyo, lakini bado tatizo la usambazaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukifika pale Nkundi, Kipande, Katawa, Milundikwa, Chala, Kasu, Kacheche na Kanondokazi, wapo wananchi wengi wanahitaji umeme na wanagombana leo haujawafikia. Umefika kijijini, lakini haujafika angle ile pale na ile pale.
Pawepo utaratibu maalum wa usambazaji, ili wote wanaohitaji umeme waweze kupata, hilo la kwanza. Na wengine hapa wanaingiza siasa, yupo Mwenyekiti wangu mmoja wa Nkundi pale anasema aliyezuwia tusipate umeme upande huu hapa ni Mheshimiwa Mipata, lakini ana
sababu zake. Naomba tugawane, ni sungura mdogo lakini tugawane wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yapo maeneo pia ya kupeleka umeme ambayo bado katika eneo langu, kama Kata ya Sintali, Kata ya Ntuchi, Wampembe, Ninde, Kizumbi, Kala na vijiji ambavyo vilisahauluka katika Awamu ya Pili, vijiji hivyo ni Katani, Malongwe, Komolo IIpamoja
na Kisura. Ni vijiji ambavyo viko jirani sana na maeneo umeme unapita kwa hiyo, wanauangalia tu hivi. Jambo hili si jema sana, linawatia simanzi na wanaona wakati mwingine ni kama tumewafanyia jambo ambalo sio lenyewe, kumbe sio kwa nia mbaya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri alipotutembelea niliweza kumfikisha kijiji cha Wampembe na njiani kote huko aliona jinsi watu wanavyohitaji umeme. Na wamebaki na matumaini na kila mara tukiwaambia Awamu ya Tatu inafuta machozi yenu wote, wote
wamekuwa hawaamini. Kwa hiyo, naomba awamu hii ianze mara moja ili maeneo haya niliyoyataja yote yaweze kupata umeme, hasa njia ndefu ya kupeleka mwambao wa Ziwa Tanganyika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipo Kitengo cha Utafutaji wa Madini, mimi kama Mjumbe wa Kamati hii tumekuwa tukizunguka huku na kule tunaangalia jinsi wananchi wanavyopata ajira katika uchimbaji wa madini mdogo mdogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, wachimbaji wadogo wadogo inaonekana ni ajira ambayo kwa kweli, fursa hiyo sehemu nyingine hatuna, naomba kitengo hiki kije kitafute Mkoani Rukwa, tuna madini yakutosha, lakini hawajatafuta. Tumemuomba Waziri kwenye Kamati kwamba watupe potentials zilizopo ili wananchi wenyewe waangalie na kama kuna mashirika mengine ambayo yanaweza yaka-chip in waweze kuangalia katika maeneo haya kwa sababu tumeona ni muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni barabara. Naungana na wote wanaosema kuna kazi nzuri ya barabara inayofanyika na sisi tuna barabara ya lami kutoka Sumbawanga kwenda Kibaoni inajengwa vizuri sana kwa kiwango cha lami na kasi imeongezeka. Sasa hivi
barabara inasogea pale Kichala na nyingine inatoka Kibaoni, imeshafika Namanyere tayari kwa hiyo, bado kipande kidogo sana. Naomba wasisimame, kasi hii iliyopo sasa iendelee ili wakamilishe hiyo barabara tuweze kunufaika na wananchi waweze kunufaika na matunda ya
Chama cha Mapinduzi, wasisimame, watusaidie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hizi pia zipo za Halmashauri ambazo zinatusumbua. Kuna barabara ya Kitosi - Wampembe, ambayo Mheshimiwa Rais kabla hajawa Rais aliweza kunipa shilingi milioni 500, nayo inaanza kusuasua na wataalam wameanza kuitengea hela
kidogo kidogo, naomba waendelee kuitengea. Alipokuwa kwenye Wizara walitenga hela ya kutosha, sasa hivi hawatengi, nitawashitaki kwake. Hakikisheni kwamba mnatenga ya kutosha. Iko Barabara ya Ninde - Namanyere na Barabara ya kutoka Kasu kwenda Myula, bado
inasuasua sana hii, mtusaidie bila kuacha ile ya kupeleka Chamiku pamoja na maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lipo suala la mtandao wa simu. Suala la mtandao wa simu kwa kweli limekuwa ni huduma muhimu. Kata yangu moja ya Kala imekuwa haina kwa kipindi kirefu na sasa hivi wanaonekana kama wametengwa na wanajimbo wengine na Watanzania kwa
ujumla.
Naomba nitumie nafasi hii kumuomba Waziri, amekuwa akitoa ahadi kila wakati, lakini wananchi hawajapata eneo la Kala, hata wale wa eneo la Wampembe na Ninde wamekuwa wakipata on and off; on and off! Wakati mwingine unasimama wakati mwingine unapatikana!
Sasa haitusaidii sana, tunaomba huduma hii imekuwa muhimu kibiashara, katika huduma za jamii, katika kuhimiza mambo ya kiafya kwa hiyo, ni muhimu iende kila mahali sawia itatusaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba nimalizie kwa kusema kero moja, kijiji changu, kijiji cha Kasapa wananchi wake wamelima mashamba, yale mashamba yamefyekwa na wahifadhi wa Msitu wa TFS. Jambo hili limekuwa kero sana na nilipojaribu kufuatilia sana wale jamaa ni wakatili sana, wameshindwa hata kuwaruhusu wananchi wakatunze mazao zaidi ya hekta 2000 ambazo wameshalima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wanakijiji wote wanashinda kijijini hawaendi kutunza mazao yao, jambo ambalo ni kero kubwa sana na kwetu kwa kweli mvua zinanyesha vizuri, naomba sauti hii ifike kwa wahusika wote, waruhusiwe tu wakatunze saa hizi mazao yao ili
wasife njaa, hawana kimbilio lingine lolote zaidi ya kilimo ambacho wanatumia jasho lao. Zaidi ya kaya 395 na watu 2,500 wanakaa hawaendi shamba kwa sababu msitu umezunguka. Na sababu ni kwamba, msitu wenyewe walikuwa hawajaweka vibao. Juzi ndio wanatuwekea
vibao mpaka mlangoni, jambo ambalo wananchi hawapati nafasi hata ya kutoka mlangoni kwenda kulima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hii ni kero na kijiji hiki kwa kweli kilifanya vizuri hata kwenye uchaguzi. Mimi nilipata kura zote, Mheshimiwa Rais alipata kura zote. Leo hii wanapoona matendo kama haya yanayofanywa na watendaji wao wanakuwa wanasema kwa kweli,
labda Serikali imetuchukia, kumbe Serikali hii ni ya wanyonge, inasikia sauti, nafikiri sauti hii ataisikia Mheshimiwa Rais na atatoa maelekezo. Nimeenda kumuona Mkuu wa Mkoa hajanisaidia katika hili. Naomba maelekezo yatolewe ili waweze kusaidiwa angalau wakavune mazao yao. Sisemi wakae siku zote, hii ni masika na ajira yao ni hiyo, kwa hiyo, mashamba zaidi ya hekta 2000 yamekaa bila kutunzwa tutegemee kutakuwa na njaa ya ajabu Mkoa wa Rukwa ambayo sio stahili yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru sana kunipa nafasi hii, Mungu akujalie sana. Ahsante sana.