Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

Hon. Stephen Hillary Ngonyani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Korogwe Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru kwa kuniona. Vile vile naanza kwa kuwapongeza Wabunge wenzangu kwa kazi nzuri ya kutoa michango katika hii hoja ya Mipango. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilivyokuwa Dar es Salaam nilisema huu Mpango wa Serikali ni mzuri sana. Ni mzuri sana kwa Watanzania wote! Nilivyokuwa Dar es Salaam nilisema sitaunga mkono hoja. Ni kwa nini sitaunga mkono hoja?
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu Mpango umeelekeza kwa Tanzania nzima jinsi itakavyopanga Serikali yetu ambayo tunaipenda sana ya Awamu ya Tano. Nataka tu Mawaziri watakapokuja waniletee majibu ya sehemu hizi ninazotaka kujua. Maana ya viwanda, maana ya reli na maana ya bandari. Unaposema kwamba tutaimarisha Bandari za Tanzania, moja ya bandari ni bandari ya Tanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bandari ya Tanga toka nimeanza kuisikia kwenye vyombo vya habari na toka nimeanza kuisikia hapa ndani ya Bunge hili kwamba kutajengwa Bandari ya Mwambani, tutarekebisha bandari zilizopo sasa hivi, lakini cha kushangaza, inayong‟ang‟aniwa ni Bandari ya Dar es Salaam peke yake. Hizi bandari nyingine zina matatizo gani? Fedha inayotumika ni ya Serikali, siyo kwa ajili ya Bandari ya Dar es Salaam peke yake! Ni bandari zote za Tanzania zirekebishwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kukaa meli sana Dar es Salaam siyo faida! Kuna Bandari ya Mtwara ambayo unaweza kupeleka meli na ikatoa mizigo ya aina yoyote. Kuna Bandari ya Tanga unaweza kutoa meli ukatoa mizigo yote, lakini tunang‟ang‟ania tu Bandari ya Dar es Salaam, meli zinakaa pale mwezi, wakati kuna bandari nyingine zenye kina kirefu, hakuna chochote kinachoendelea! Hii hatutendewi haki! (Makofi)
Tunapozungumzia reli, reli zote ni kwa faida ya Watanzania, lakini unaponiambia kwamba barabara zitatengenezwa na zitaimarika; zitaimarika namna gani kama reli zenyewe ambazo tumeanza kuziongolea toka sijaingia Bunge hili mpaka leo hii hazitengenezwi? Hiyo barabara itakayokuwa nzuri ambayo mabasi yatakuwa yanapita na magari madogo bila kuumia ni ipi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali yangu Tukufu, sikivu, hebu jaribu kuiangalia na reli inayotoka Tanga, kupitia Kilimanjaro, kupitia Arusha na kwenda mpaka Musoma. Mwaka 2012 tumeijadili hii reli kwamba itajengwa lakini tunashangaa zinajengwa reli ya kati tu, lakini huku kwingine zikikorofisha kidogo zinarekebishwa. Reli hii ya Tanga mpaka Arusha mpaka Musoma, hata kuisikia kwenye vyombo vya habari, hatuisikii! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania haijengwi na reli ya kati peke yake, Tanzania haijengwi na mikoa ya kati pekee, Tanzania inajengwa na mikoa yote ya Tanzania ili mtutendee haki. Serikali hii ambayo ni sikivu inayoendelea kutumbua majipu, hebu angalieni na mikoa hii mingine ambayo mlituahidi wenyewe na tukaunga mkono kwa dhati kwamba tunachohitaji ni maendeleo. Maendeleo haya hayatapatikana kwa reli ya kati peke yake! Barabara zinazotoka Arusha kwenda Dar es Salaam, kila siku zinakarabatiwa, kwa nini? Kwa sababu reli ya Tanga haifanyi kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri katika mipango yake yote, hebu jaribuni kurekebisha hizi reli nyingine ambazo hamzipi kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye viwanda. Siku za nyuma, mikoa mitatu ndiyo ilikuwa na viwanda vingi sana hapa Tanzania; Mkoa wa Dar es Salaam, Morogoro na Tanga. Cha kushangaza, tunasema tutajenga viwanda vipya, hatukatai. Ni mambo mazuri ya Serikali kwa sababu ya kuwasaidia Watanzania ili wapate kazi. Je, viwanda ambavyo vimekufa mnaviweka wapi? Kwa mfano, kuna kiwanda cha General Tyre Arusha, Kiwanda cha Kahawa pale Moshi na viwanda vilivyoko katika Mkoa wa Tanga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Tanga kulikuwa kuna viwanda vyenye msimamo! Kuna Kiwanda cha Chuma, Kiwanda cha Mbolea, Kiwanda cha Foma, Kiwanda cha Mablanketi, Kiwanda cha Mashati, kulikuwa na Kiwanda vilevile cha kutengeneza Mbao, Sikh Saw Mills, kulikuwa na kiwanda pale Mkumbara cha kutengeneza chipboard, kulikuwa kuna Viwanda vya Chai ambavyo mpaka leo hii havijafunguliwa. Serikali imeahidi itavifungua, kwa mfano kiwanda cha Mponde, lakini hakuna! Sasa tukifanya haya mambo, tunafanya mambo tu, halafu sisi tukirudi huko nyuma ndiyo tunahukumiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu hapa leo tunaongea sana lakini Wabunge wakirudi nyuma watakiona chamoto. Naomba Serikali sikivu, mviangalie hivi viwanda. Leo hii tunaambiwa Kilimo Kwanza, nimekubali lakini nataka mniambie hawa wananchi wa Mkoa wa Tanga watalima wapi, wakulima wa Moshi watalima wapi, wakulima wa Morogoro watalima wapi; kwa sababu maeneo mengi yamehodhiwa na watu wachache na hao watu wachache waliohodhi hayo mashamba hawayaendelezi badala yake ni ya kukopea mikopo kwenda kununua magari ya kisasa! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama watu wanakopa mikopo kwa ajili ya kununua magari ya kisasa na wamekopa kwa ajili ya kuendeleza kilimo, kilimo hicho hakiendelezwi, wananchi wanaambiwa kilimo kwanza, wakati mashamba yale ambayo wangeyategemea wananchi wa chini kulima, yamehodhiwa. Ukilima pale, mtu anakuja nyuma yake, anakupeleka Polisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Fedha, ni rafiki yangu na nampenda, anafanya kazi kwa dhati. Bahati nzuri Mawaziri wote mlioingia safari hii, hakuna Waziri mwenye shida. Wote mmeamua kumsaidia Mheshimiwa Magufuli. Haya mambo tunayoyaongea ni ya msingi sana ili kuiona Tanzania siyo tegemezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunazungumzia masuala ya umeme, ni kitu muhimu sana kwa Watanzania, lakini nataka niulize, huu umeme wa mafuta wenye gharama kubwa tunaoukazania, kwa nini msiendeleze kituo cha Hale, Kihansi na pale Achemka ambapo ni umeme wa maji? Maji yapo! Ni lini mmesikia Mto Ruvu umekwisha maji? Kama tatizo ni maji, Mto Ruvu ni lini umekauka maji? Kwa sababu tunategemea tu kwamba tutumie mabilioni ya pesa! Hawa watu wa Symbion wanaokuja kutupa masharti magumu, tumshukuru Mheshimiwa amesema safari hii hatutegemei wafadhili, tunajitegemea sisi wenyewe. Sasa kama tunajitegemea sisi wenyewe tujaribu kupunguza gharama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hivi vituo vya nguvu za umeme ambavyo vinatoa nguvu za umeme kwa kutumia maji ambayo gharama yake ni nafuu. Tungeviongezea engine. Kama ni mashine, basi ziongezewe mashine kuliko kutumia umeme unaotokana na mafuta ambapo hao watu wanatupiga bei mara mbili. Watanzania wanakaa katika wakati mgumu kwa kuwalisha watu wachache ambao wanataka kuja kutuhukumu leo kwamba hawatatupa misaada. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, vitu muhimu sana ambavyo tunaweza kufanya; wananchi wa Tanzania wanategemea sana kilimo, lakini hivi leo ninavyokwambia, hakuna sehemu ambayo Watanzania wanaweza kulima. Siyo kwamba nchi hii haina ardhi, ipo; lakini ardhi hii inakuwa ya masharti kama tuko Kenya. Imehodhiwa na mtu kwa manufaa yake. Nashukuru safari hii Waziri wa Ardhi, unafanya kazi nzuri sana, lakini usiangalie mikoa ya huko tu, angalia na Mikoa ya Mashariki yako. Anza Morogoro, njoo Pwani, nenda Tanga, nenda Kilimanjaro, nenda mpaka Arusha, ili ukitoa maamuzi, utoe maamuzi! (Makofi)
Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, wengine wakati wa nyuma walikuwa hata ukiwapigia simu hawapokei, lakini wewe unapokea. Sasa kama unapokea, umefanya kazi nzuri kwa muda mfupi. Njoo uangalie mashamba, misitu ya kule Tanga ambayo wananchi wanalalamika sana kwamba, hawana mahali kwa kulima, lakini mashamba hayo yamekopewa fedha. Ukienda ukilima, kesho mtu anakuja kupanda zao lake, anakwambia hapa siyo kwako. Sasa kama siyo kwangu, nimekaa miaka 50 hapa siyo kwangu kivipi? Eti kwa sababu ni mtu ambaye ana uwezo. Sasa hawa waganga wa kienyeji wasiokuwa na uwezo watalima wapi? (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tuangalie, naamini kabisa Serikali ya safari hii ni sikivu. Mawaziri mnafanya kazi nzuri sana nami naendelea kuwapongeza. Ukimwona mtu anamsema vibaya Waziri ana matatizo ya akili, kwa sababu Mawaziri mko wachache na nchi ni kubwa, hamwezi kwenda kila kona kwa muda mfupi. Kwa hiyo, ninachoomba ni kwamba, tushirikiane nasi Wabunge hapa wote, usijali itikadi ya mtu; twendeni mkaone mazingira ya Majimbo yetu na mtoe maamuzi kama anavyotoa Mheshimiwa Lukuvi pale kwa pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona niliseme hili, kwa sababu sisi kule Tanga na Mikoa ya Mjini huku tunapata shida sana. Kama tunapata shida sana, hakuna mahali kwa kuongelea masuala haya ila ni hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu Mheshimiwa Waziri wa Barabara ajue kwamba Jimbo langu barabara zote zimefungika, watu wamekaa kwenye visiwa na maji yameingia kwenye nyumba za watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali Tukufu hii iende ikaangalie Mkoa wa Tanga ulivyopata mafuriko makubwa. Wabunge usione tumekaa hapa, tumekaa kwa ajili ya kuchangia hoja hii tusije tukaonekana Wabunge wa Mkoa wa Tanga ni watoro. Siyo watoro lakini kwetu huko kumeingiliwa, hakuna mahali kwa kuwatetea Waheshimiwa Wakulima wetu, pamoja na Wajumbe wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mungu awasaidie sana na amsaidie sana Spika wa Bunge hili kwa kazi nzuri aliyotufanyia safari hii. Meza tunayokaa utafikiri tupo Ulaya, kumbe tupo Tanzania. Ahsanteni sana.