Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MAHMOUD H. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Awali ya yote napenda kuwapongeza Wenyeviti wote waliowasilisha leo mada zao hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa majukumu makubwa ya Bunge letu Tukufu ni kuishauri na kuisimamia Serikali, lakini kumekuwa kuna tatizo hapa. Tutazungumza, tutasema, lakini hayo tutakayokuwa tumeyazungumza na kuyasema na kuwashauri wenzetu wa Serikali watakuwa hawayafanyii kazi kama siku za nyuma. Kwa mfano, katika bajeti iliyopita sisi Waheshimiwa Wabunge wote kwa kauli moja tulishauri tuongeze tozo ya maji kutoka sh. 50 kwenda kwenye sh.100 na Wabunge wanajua matatizo yaliyopo kwenye majimbo yao. Cha kusikitisha kabisa Serikali ilikataa hili jambo na hela ambayo inafanya kazi sasa hivi ni hela ya Mfuko wa Maji, hela iliyokuwa kwenye bajeti kuu haipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawashawishi Waheshimiwa Wabunge wenzangu ili hoja ambayo tulikuja nayo kwenye bajeti tuendelee nayo na yawe ndiyo maazimio ya Bunge ili hiyo sh. 50 iongezwe ili kwenye bajeti ya safari hii tusiume maneno; kwamba tozo ya maji imetoka kwenye sh.50 kwenda kwenye sh.100 ili tuendelee kupata maji katika maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ninalopenda kushauri katika Wizara hii ya Maji ni suala la mita; tuwe na mfumo wa prepaid kama ilivyokuwa umeme, kwa sababu miongoni mwa watu wanashindwa kulipa maji kwa wakati matokeo yake Sekta hii ya Maji inashindwa kujiendesha. Kwa masikitiko makubwa taasisi nyingi za Serikali zimeshindwa kulipa na ndizo zilizoweka mzigo mkubwa sana kwenye taasisi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sekta hii kutengeneza hifadhi, kuchimba mabwawa ya kutosha ili maji yawe ya uhakika kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la kilimo. Asilimia 67 mpaka 72 ya Watanzania ni wakulima na Serikali imesema kwamba inataka kwenda kwenye uchumi wa viwanda, tutaendaje kwenye uchumi wa viwanda kama hatujawekeza vya kutosha kwenye eneo la kilimo? Tuna matatizo kwenye eneo la pembejeo, naiomba Serikali katika eneo la pembejeo tuangalie kwa nafasi kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka ya nyuma tulikuwa tuna eneo kubwa la kutoa ruzuku katika eneo hili, lakini cha kusikitisha ruzuku inayotoka safari hii ni ndogo kuliko iliyokuwa siku za nyuma, mfuko wa ruzuku katika eneo hili umepungua. Kwa hiyo, waongeze mfuko wa ruzuku tofauti na uliokuwepo miaka iliyopita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko makubwa, Serikali imekuwa hailipi pesa za mawakala, kwa hiyo wametengeneza gap kubwa kati ya mawakala na wakulima wetu waliokuwa kijijini. Serikali inadaiwa zaidi ya bilioni 64, huu mwaka wa tatu na baadhi ya mawakala wameuziwa nyumba zao na baadhi ya mawakala wamekufa kutokana na shock walizokuwa nazo katika maeneo. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali ijiangalie na iwalipe hawa mawakala kusudi waweze kufanya kazi zao mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye eneo la ukame. Hapa kwenye eneo la ukame kuna tatizo. Naishauri Serikali ipeleke mbegu ambazo zinahimili ukame katika maeneo husika, lakini vilevile katika yale maeneo ambayo kwenye ripoti yetu tumeyasoma leo, zile halmashauri 55 ambazo zina matatizo ya chakula tunaiomba Serikali ipeleke chakula haraka iwezekanavyo. Kwa sababu tunaweza tukashindwa kupeleka chakula kwa wakati tukasababisha inflation, chakula kitakuwa kiko juu kwa sababu ya demand pullinflation katika maeneo yale,kwa hiyo hata ule mfumuko wa bei tunaouzungumzia kwamba tunaweza tukau-control, tatizo la chakula likiendelea kuwepo katika maeneo husika automatically inflation itaongezeka katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko makubwa tunaiomba Serikali iondoe kodi kwenye mbegu zinazozalishwa hapa nchini. Unakuta mbegu zinazotoka nje ya nchi hazina kodi lakini mbegu zinazozalishwa na Watanzania zina kodi. Haya ni masikitiko makubwa sana, waziondoe hizo kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunaomba Serikali iongeze mtaji kwenye Benki ya Kilimo, mtaji uliopo sasa hivi hautoshi. Kwa hiyo, wakulima wetu hata kama wanataka kufanya kazi kwa ajili ya kuisaidia hiyo sekta ya viwanda ambayo inataka kuja hatuwezi kupata kwa sababu benki katika sekta hii haipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie kidogo kuhusu ranchi. Tuna tatizo, kuna baadhi ya ranchi zilichukuliwa na watu binafsi na zinaendelea kumilikiwa na watu binafsi. Hatuna sababu ya zile ranchi kuendelea kumilikiwa na watu binafsi ikiwa hawazitumii kwa yale makusudi tuliyoyakusudia; matokeo yake mifugo mingi inazurura kwenye hifadhi za Taifa na kuleta kero ambazo hazina sababu. Kwa hiyo wale watu ambao wanatumia ranchi zile ambazo hazina sababu ya kutumiwa wanyang’anywe zirudishwe Serikalini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ninalotaka kuzungumzia kidogo ni suala la maliasili. Nataka kuzungumzia suala la VAT kwenye maliasili. VAT inapokuwepo automatically unaongeza gharama za utalii, kwa hiyo Serikali yetu badala ya kupata mapato tunayostahili kupata, hatuwezi kupata mapato yale kwa wakati, kwa hiyo Serikali iliangalie upya suala la VAT. Wenzetu wa Kenya tulikwenda nao kwa kauli moja, lakini ilipofika wakati wa utekelezaji Wakenya wakaji-withdraw kwenye hili jambo wakatuacha tukakaa peke yetu, kwa hiyo utalii wa hapa nchini ukawa gharama zaidi kuliko wa kwao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la miundombinu. Miundobinu ya utalii katika nchi yetu ni dhaifu, kwa hiyo tunatakiwa tujiangalie kwenye hili eneo, tuboreshe miundombinu katika maeneo ya utalii na tujenge nyumba za bei rahisi kwenye hifadhi zetu ili watu wa kawaida waweze kwenda kutalii. Kwa hiyo kuna haja ya kutunza utalii wa ndani katika nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ardhi. Maafisa wengi wa ardhi, hasa maafisa wa mipango miji wamekuwa wana matatizo makubwa sana katika maeneo yao, hawafanyi kazi zao ipasavyo matokeo yake watu wanaendelea katika ujenzi holela.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, naunga mkono hoja. Naomba yale maazimio yote ambayo yametolewa na Kamati zilizohusika tuyapigie kura na yaweze kutekelezwa na Serikali.