Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa hii. Nianze kwanza kwa kuishukuru sana Kamati na kuunga mkono pengine na kusema kwamba tunapokea ushauri ambao wameutoa ikiwa ni pamoja na ile addendum ambayo imeletwa kama Serikali tumeipokea na tutakwenda kuifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wachangiaji wengi wamezungumzia masuala ya migogoro na kama mwenzangu wa kilimo alivyozungumza, suala hili la migogoro ni mtambuka. Nitapitia wachache ambao nimejaribu ku-note, ukiangalia suala la migogoro, zaidi ya Wabunge 15 wamezungumzia. Naomba nianze kwa kusema kwamba ushauri uliotolewa na Kamati tumeupokea kama ulivyo, wamezungumzia suala la National Housing kwamba nyumba ni za gharama nafuu, lakini ubora si mzuri sana. Hilo tumelipokea na tutakwenda kupitia tena kuona ni jinsi gani ambavyo watakwenda kuboresha. Sehemu kubwa pia hata ile size ya nyumba zinapoungwa mbili wengi wamesema hawazipendi sana katika kutembelea waliyazungumza hayo. Kwa hiyo, tutalifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nikija kwa hoja ya Mheshimiwa Sakaya ambayo alizungumzia habari ya Kamati iliyoundwa na Wizara tano ambazo hazijajulikana zinamaliza muda wake lini pamoja na Mheshimiwa Grace Kiwelu na Mheshimiwa Pauline Gekul wote walitaka kujua taarifa hizi zitakuja lini.
Mimi niseme tu kwamba tarehe 13 Februari, taarifa ya kwanza itatoka na wamepitia katika mikoa mitano, wamekwenda Tabora, Katavi, Morogoro, Geita na Kagera. Kwa hiyo, taarifa ya kwanza tutaipokea kutoka katika mikoa hiyo. Baada ya hapo awamu ya pili wanakwenda katika Mkoa wa Arusha, Manyara, Tanga na Pwani, kwa hiyo, tutawapa ratiba kamili watakapokuwa wanakwenda kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Sakaya pia alitaka kujua namna ambavyo tunaweza tukasaidia Halmashauri kuhakikisha kwamba viwanja vinapimwa na kuondoa hii migogoro. Niseme tulikuwa na ule mfuko na bado upo lakini haufanyi kazi vizuri sana kwa sababu Halmashauri zetu zinakopa na hazirudishi. Jumla ya Halmashauri 27 zilishakopeshwa kiasi cha shilingi 962,676,000 lakini kati ya hizo Halmashauri 11 hazijalipa, bado zinadaiwa. Kwa hiyo, pesa ambayo ilitakiwa irudi ni shilingi 1,155,211,224.
Kwa hiyo, niwaombe tu Halmashauri ambazo zinadaiwa mrejeshe ikiwemo Halmashauri ya Magu, Mji Mdogo wa Makambako, Kagera, Bunda kwa maana ya Chato lakini kuna Singida, Sengerema, Iringa, Tumalenga, Ruvuma, Songea na Tarime. Hizi ni Halmashauri zinazodaiwa, tuwaombe sana mrejeshe ile mikopo ili na wengine waweze kutumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa suala la kusaidia, tuseme tu kwamba kanda zetu tumejaribu kuziimarisha, lakini tatizo tulilonalo kwa nchi nzima tuna upungufu wa watumishi wa sekta ya ardhi kwa asilimia 64. Kwa hiyo, utaona kwamba kuna upungufu mkubwa ambapo kwa kweli kuweza kukidhi haja inakuwa ni ngumu. Pamoja na upungufu huo, tunazo Halmashauri kama saba ambazo hazina kabisa wataalam hao, kwa hiyo, unaweza ukaona changamoto jinsi ilivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ambavyo tunajaribu kuimarisha kanda zetu, niwaombe tu Waheshimiwa Wabunge pale mnapokuwa na ratiba za upimaji shirikisheni ofisi zetu za kanda, kwa sababu tunatarajia watakuwa tayari wamekamilika na timu nzima za wataalam lakini pia na vifaa vya upimaji. Kwa sababu unakuta kanda moja pengine inasimamia Halmashauri zaidi ya 18 mpaka 36, basi niombe tu ile ratiba iweze kwenda vizuri ili hawa nao wasaidie katika kupima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sehemu kubwa ni jukumu letu katika Halmashauri zetu kuona ni jinsi gani tunapanga mikakati yetu vizuri kuweza kuweka utaratibu wa kupima kila mwaka na kwenye mpango wa matumizi bora ya ardhi, tukiweka angalau vijiji vitatuau vinne kila mwaka tutasogea. Gharama siyo kubwa ni kati ya shilingi milioni sita mpaka 7 na kuna vijiji vingine vina uwezo basi tuwashirikishe wale waweze kuona ni jinsi gani wanaweza wakahudumiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ku-subsidized nyumba za National Housing hili tulichukue tu tulifanyie kazi, kwa sababu ni mashirika mengi yanayojenga, bado TBA, WatumishiHousing, NSSF kila mmoja atataka kunufaika na punguzo hilo. Kwa hiyo, niombe tulichukue tutaendelea kulifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la mashamba ambapo wamezungumzia kwamba kasi ni ndogo pengine na gharama ya kuweza kuyapima. Mimi niwaombe Waheshimiwa Wabunge kwenye maeneo yetu sisi ndiyo tuna mashamba hayo na tunatambua jinsi gani ambavyo hayajaendelezwa. Kazi ya Wizara ni kupokea kile ambacho mmeona hakifanyi kazi vizuri na kimekiuka taratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuwaombe wakati wanafanya kazi zao wale watumishi wa idara husika iwe ni sehemu ya kazi zao. Mmaana hapa mmesema hakuna pesa anahitaji pesa lakini akiweka kama ni sehemu ya kazi zake za kila siku, yule anayefanya kazi za uandani anapokwenda kufanya kazi kule basi afanye na kazi hii itasaidia sana katika kuona ni jinsi gani tunaweza tukapunguza au tukatoa taarifa za haya mashamba. Tusisubiri hela za kuja kupimiwa au kukaguliwa kutoka Wizarani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Njeza amezungumzia suala la mipango miji, naomba nikiri tu hili nalo ni kutokana na upungufu tulionao. Pia tunaomba sana kwa sababu wenzetu wa Mbeya wako katika mpango kabambe wa master plan basi hilo nalo liingie katika mpango huo, itasaidia sana katika kuona ni jinsi gani tunaweza tukaweka mpango mzuri katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la ile project ya Kawe, imezunguziwa kwamba amepewa mtu binafsi kwa US dollar milioni 6.5.
Naomba niseme tu kwamba tungeweza hata kuishukuru Serikali kwa namna ilivyoweza kuokoa, kwa sababu lile lilikuwa imewekwa chini ya PSRC na ndipo hapo Wizara ikaomba kupitia National Housing ili kuweza kuchukua ile fifty, fifty angalau eneo lingine lirudi Serikalini. Isingekuwa hivyo basi basi eneo lote lilikuwa limeshaondoka. Mimi nasema kwa kweli lile eneo na gharama yake ni kubwa kwa maana ya kwamba lina-appreciate kila siku. Kwa hiyo, kitendo cha kuchukua asilimia 50 ...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.