Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Dr. Charles John Tizeba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buchosa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nami kwa kuanzia niishukuru sana Kamati yetu ya Kilimo, Mifugo na Maji, kwa taarifa nzuri ambayo kwa ukweli imegusa maeneo yote muhimu ambayo wao wana wajibu wa kuyasimamia na kutoa ushauri kwa Serikali. Nawashukuru sana tumefanya kazi vizuri na niseme tu mapema kwamba yote ambayo wamependekeza na kutolea ushauri tumeyachukua, mengine tutayafanyia kazi mara moja na mengine ambayo yanahitaji muda tutaendelea kuyafanyia kazi kadri muda utakavyokuwa unakuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wamezungumza mambo mengi na kwa hisia sana. Hisia hizo zinaonesha ni kwa kiasi gani wanaguswa wao na wananchi wanaowawakilisha na haya mambo ambayo wameyazungumzia. Kilimo katika tafsiri yake pana kinamgusa kila mtu na kwa hivyo haishangazi na kwa kweli lazima utegemee mjadala utakaokuwa unahusu kilimo uwe na sura hii. Mimi mwenyewe ningeshangaa kama mjadala wa Kamati hii ungekuwa na sura tofauti na hii niliyoiona hapa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, niombe nizungumzie tu mambo machache ambayo mwenzangu Mheshimiwa Ole-Nasha hakuyagusa. Nianze na suala la tozo. Suala la tozo limekwishatolewa kauli na Mkuu wa nchi kwamba zote zile ambazo ni za hovyo hovyo na zenye usumbufu Serikali izifanyie kazi na iziondoe. Ziko tozo ambazo hazikuwa na madhara ya kibajeti katika mazao tumeziondoa, kwenye korosho, tumbaku, pamba tumezifuta. Ziko tozo ambazo zilikuwa na madhara ya kibajeti kama tungezifuta mara moja.
Kwa hivyo, hizi zinafanyiwa kazi iko Kamati ya Serikali ya Makatibu Wakuu wanaendelea kufanyia kazi na kwa kweli tutakapoingia katika bajeti hii ya mwaka huu tozo nyingi mtaona zitakuwa zimeondolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tozo hizi haziathiri tu bei za mazao na mambo mengine lakini ziko tozo pia zinazoathiri kilimo ambazo haziko kwenye mazao. Waheshimiwa hapa wamezungumzia gharama kubwa ya pembejeo, mbolea tu inazo tozo 14 mbalimbali. Kwa hiyo, tunavyozungumzia kushusha gharama ya pembejeo pamoja na hatua zingine ambazo tumejipanga kuzichukua, lakini itabidi pia tuangalie katika hizi tozo zilizopo kwenye mbolea ili mjumuiko wa hatua hizo utuhakikishie kwamba mbolea itashuka bei kiasi kwamba wakulima na watumiaji wengine wa pembejeo wataweza kumudu bei bila wakati mwingine kulazimika kuweka ruzuku katika pembejeo hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Haonga analiona hilo, kwamba tunao uwezekano wa kufika mahali tukaondoa ruzuku kwenye pembejeo kama tutaweza kushusha bei zake katika levels ambazo mkulima wa kawaida anaweza kuzimudu. Hatua kadhaa zinachukuliwa, moja, ni kama alivyosema kununua moja kwa moja kwa wazalishaji wa hizi pembejeo. Tumefanya hivi mwaka huu na kwa kweli mbolea imeshuka bei kwa wastani wa asilimia karibu 28. Tutaendelea kuchukua hatua zingine za kupunguza kodi hizi, lakini pia kuna mazungumzo mazuri sasa hivi ya ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza sulphur hapa hapa nchini. Tukifanikiwa kufanya hivyo maana yake ni kwamba hata bei ya sulphur tunayoinunua sasa hivi kwa bei kubwa huko nje na yenyewe itashuka bei. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie haraka haraka suala la mbegu. Mbegu ni tatizo kweli, bado utoshelevu wetu wa mbegu bora uko kwenye asilimia 40 Kitaifa, kwa hivyo asilimia 60 bado tunaagiza nje. Mbegu inayozalishwa hapa ndani ina changamoto moja kubwa kwamba inatozwa kodi wakati mbegu zinazoagizwa nje ya nchi hazitozwi kodi. Hata mimi haiingii akilini, ni kwa sababu kwa kufanya hivyo, mbegu inayozalishwa Tanzania inakosa ushindani lakini inakuwa inakatisha tamaa kwa wazalishaji wa ndani kuzalisha zaidi kwa sababu hata wakizalisha mbegu inayotoka nje inakuwa na ushindani zaidi kuliko ya hapa ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo tutalitazama katika Serikali na kwa kweli nadhani ni jambo ambalo tunaweza tukaliondoa tu mara moja ili kuwapa motisha wazalishaji wa ndani wa mbegu tuweze kujitosheleza. Wakala wetu wa Mbegu wa Taifa nimekwishawapa maelekezo, mashamba yote ambayo wameyatunza yamekuwa mapori, wawape watu wenye uwezo wa kutuzalishia mbegu waingie nao mikataba kwa masharti ambayo yatakuwa yanawawezesha wale watu kuzalisha bila kupata hasara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la fedha katika Wizara ya Kilimo. Kamati imeona kweli kwamba bajeti iliyokwishatolewa mpaka sasa ni kidogo, labda nitoe taarifa kwamba kilimo kinapata fedha nyingi nje ya mfumo wa bajeti ya Serikali. Leo tunavyozungumza, fedha iliyoingia katika kilimo kupitia vyanzo tofauti na bajeti ya Serikali iko kwenye tune ya shilingi trilioni 1.7, hii si hela kidogo katika kilimo cha nchi hii. Tunapata fedha nyingi kwenye kilimo nje ya mfumo wa bajeti kupitia mashirika mbalimbali kwenye SAGCOT na kadhalika. Bill & Melinda Gates Foundation peke yake imeingiza Tanzania dola milioni 700 ambazo zimeelekezwa kwenye kilimo, wacha World Bank, AGRA na wengine. Kwa hiyo, kilimo kwa maana ya bajeti ambayo inapita kwenye Wizara ni fedha inayoonekana si nyingi sana lakini fedha nyingine inakwenda kwenye Halmashauri lakini wafadhili wengi wanapeleka moja kwa moja kwenye programu na miradi mbalimbali ya kilimo inayotekelezwa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza na taasisi za fedha, zimekubali pia sasa kuanza kukopesha, kutoa fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali ya kilimo. NMB peke yake wametenga mwaka huu wa fedha shilingi bilioni 500 kwa ajili ya kukopesha miradi ya kilimo na shughuli zingine zinazohusiana na kilimo. Kwa hiyo, tukitumia hizi fursa vizuri kilimo chetu kitasonga mbele.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)