Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Muleba kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza naomba nijue utaratibu ni dakika ngapi.
MWENYEKITI: Una dakika kumi.
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi muda huu, kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge hili kwa awamu hii kwa kikao hiki kwanza kabisa nianze na pongezi. Nawapongeza kwa dhati Wabunge wetu wapya wateule wa Mheshimiwa Rais ambao wameungana na sisi, uteuzi huo mimi mwenyewe umenifurahisha sana, natoa pongezi na nimefarijika sana kumuona Mwenyekiti wa Baraza la Wazazi wa CCM, Mheshimiwa Abdallah Bulembo akiwa na sisi. Hii ni waziwazi kwamba Mheshimiwa Rais anataka Bunge hili pia tuwe na weledi katika malezi ya vijana wetu, kwa hiyo hongereni sana. Pia nampongeza msomi mwenzangu, Mheshimiwa Profesa Kabudi ambaye na yeye ameungana na sisi na nitoe taarifa kwako Mheshimiwa Mwenyekiti kwamba jana sisi katika Bunge Readers’Club tayari tumeshaanza kumfaidi aliweza kutoa mada ya matumaini yake katika Bunge hili. Kwa hiyo, tunaona kwamba uzoefu wetu katika fani ya sheria ambazo tunatunga unaendelea kuongezeka. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mama Anne Kilango Malecela ambaye anarejea nyumbani, waswahili wanasema mwenda kwao siyo mtoro, hapa ni nyumbani kwake. Natoa pia pongezi zangu kwa Mheshimiwa Dkt. Possi ambaye amepangiwa kazi nyingine ambaye sasa hivi ni Balozi katika Diplomasia. Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nichukue nafasi hii kumpongeza Mkuu wetu mpya wa Majeshi aliyeteuliwa na kutoa pongezi zangu, ziwekwe on record, kwa Jenerali Mwamunyange ambaye amemaliza kipindi chake kwa utekelezaji uliotukuka, hapo hatuna budi kabisa kusema kwamba tulikuwa katika mikono salama na leo tunaangalia ulinzi na usalama wa Taifa hili. Naendelea pia kutoa pongezi zangu kwa….
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Ndiyo, kwa sababu ni sehemu ya ulinzi na usalama kama unashangaa ni conceptual framework, maana yake mambo haya huu ndiyo ulinzi na usalama wenyewe huu, kwa sababu watu wanafikiria kwamba ulinzi na usalama ni mitutu ya bunduki hapana, ni amani, ni maendeleo, ni upendo, ni kufahamiana ni kutambuana na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sina budi kuwapongeza waliokuwa kwenye uchaguzi mdogo, naipongeza CCM na mimi mwenyewe najipongeza kwa kushinda kwa kishindo na wenzetu nasema kwamba kujikwaa siyo kuanguka, lakini wapiga kura kwa kweli walikwenda vizuri kwa sababu ulikuwa ni uchaguzi wa amani. Kule kwangu Muleba ninapozungumza hili sina budi kuwatambua kabisa wananchi wa Muleba Kata ya Kimwani na kumpongeza Ndugu Daudi Kiruma aliyeibuka mshindi akaleta ushindi wa CCM. Niwashukuru sana watu wote walioshiriki katika zoezi hili ambalo lilikwenda katika hali ya ustaarabu na demokrasia ya kisasa, nawapongeza sana, ngazi ya Taifa hawakututupa, ngazi ya Mkoa, Wilaya mpaka kwenye Kata. Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Mkoa wa Kagera, mimi ni mwakilishi kutoka Mkoa wa Kagera na katika hali ya kuangalia hali ya ulinzi, usalama na ujirani mwema wetu mnajua kwamba tulipata tetemeko na kwa mara nyingine tena ninatoa shukrani kwa mchango wa Waheshimiwa Wabunge ambao mlitupa. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ziara ya Mheshimiwa Rais ambaye tarehe Mosi, mwaka huu alikuja akasali na Wanakagera, akatufariji na sisi tulifarijika. Nilishangaa sana kuona watu ambao wazungu wanasema watoa machozi ya mamba (crocodile tears) wakijaribu kubeza ziara hiyo iliyofanikiwa kwa kiwango kikubwa. Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wanakagera tulifarijika sana na hasa tuliweza kupata misaada mbalimbali. Mheshimiwa Rais alikuja amejipanga vizuri alikuja na Balozi wa Uingereza ambaye atasaidia katika kurekebisha miundombinu. Mambo haya siyo haba, tumeyashuhudia. Kwa hiyo, nataka kusema kwamba katika suala la kumshukuru Rais kuja kututembelea na hata Mheshimiwa Jenista aliandamana naye Mawaziri kadhaa walikuwepo pale nawashukuruni sana na changamoto waliziona. Sasa kitu kikubwa ambacho napenda kusema kinahusiana na mada ya sasa hivi ni kwamba makazi kwa wananchi wa Kagera yanaendelea kuwa ya wasiwasi kwa sababu watu ambao nyumba zao ziliporomoka wengi bado wako katika hali hatarishi kiulinzi na kiusalama. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba nichukue nafasi hii kuomba kwamba Kamati ya Ulinzi na Usalama pia iangalie jambo hili kwa mapana yake na kuangalia sasa tunapojipanga na Waheshimiwa Mawaziri Serikali mnapojipanga, mnawasaidiaje wananchi ambao sasa hivi bado wanaendelea kuwa nje kwa sababu hawana makazi. Mheshimiwa Rais alifafanua vizuri sana, mimi naweza nikasema kwamba nimeshughulikia mambo ya maafa kwa ngazi za Kimataifa, Serikali huwa haijengi nyumba hata na Japan hawajengi nyumba hiyo ni international standard, jambo hili linaonekana geni kwa watu wengi lakini ndivyo zilivyo sheria za kimataifa. Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi ambalo tunaweka mezani kuwasaidia wale wahanga sasa kupata vifaa vya ujenzi kwa bei nafuu, ni suala la kiusalama na kiulinzi na kimiundombinu kwamba sasa hivi mtu ambaye nyumba yake imeporomoka sasa analipa kodi ya VAT kwenye mabati, kwenye simenti, kitu hiki kina ukakasi na tukiangalie sasa kwa mapana marefu. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, dakika ngapi sasa hizi tano, bado ninazo tano, sawasawa. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dakika zangu tano ambazo sasa zimebaki, naomba nianze na suala la ulinzi na usalama kabisa ambalo limeongelewa sana na watu, na ninaomba nikabidhi kwa rekodi ya Hansard, naomba nikabidhi barua ya Makamu wa Rais wa nchi ya tarehe 30, Mei alipositisha zoezi la kufukuza mifugo kutoka kwenye Mapori ya Akiba na Hifadhi nyingine ndogo ndogo. Kuna barua hapa naomba ipokelewe, wahudumu nisaidie, iwe kwenye rekodi za Hansard, sasa hao watu ambao wanaendelea kukiuka maagizo ya Makamu wa Rais wa Nchi kwamba zoezi hili limesitishwa wakati Serikali inajipanga watuambie wenyewe mamlaka yao wanayapata wapi. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapozungumza sasa hivi, katika Wilaya ya Misenye kuna watu sasa hivi wanachomewa nyumba zao, kuna wafugaji ambao wanahangaishwa, kuna wafugaji wengine Wabunge wengine nimesikia mnasema watu wameuawa, ninaomba tusipopata maelezo ya kutosha basi Bunge hili liazimie kwamba tuwe na Judicial Enquiry katika vifo vinavyoendelea kwa wafugaji. Kwa sababu, haiwezi kukubalika, tuliona Operesheni Tokomeza ilipotufikisha, sasa inakuaje watu wanapigwa risasi na Maafisa Wanyamapori na inakuwa business as usual, jambo hili haliwezi kukubalika naomba barua ya Makamu iwe sehemu ya Hansard. Kama imefichwa iliandikwa kwa Wakuu wa Mikoa wa Tanzania Bara wote, ninayo hapa naiweka for the record.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nataka nisisitize, mimi kwangu Muleba tuna tatizo la usalama wa wavuvi, wavuvi wangu wanahangaishwa. Naomba Serikali itufafanulie, ulinzi wa wavuvi, wavuvi ni kama wametelekezwa inabidi walipe wao vituo vya Polisi, wajitafutie zana na mambo kama hayo. Kwa hiyo, naomba Kamati ya Ulinzi na Usalama ije itutembelee na akina mama katika Kamati ile na ninyi wawabebe kama wanavyonibeba mimi kuingia kwenye mitumbwi maana yake kule hakuna hata gatiza kuweza kupaki boti, ni suala la ulinzi na usalama ni suala nyeti, naomba lifanyiwe kazi kwa mtazamo huo. Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, ulinzi na usalama pia kuna suala la chakula. Kule kwangu Muleba sisi ni wakulima, tunafanya kazi kwa bidii lakini tulikuwa na ukame, kuna upungufu wa chakula, kwa hiyo chakula hakitoshi, na penyewe tuangaliwe kwa mtizamo huo. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.