Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Nkasi Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami naunga mkono taarifa ya Kamati ya Sheria Ndogo na taarifa zote zilizowasilishwa. Siko mbali sana na wajumbe waliotangulia, kwanza nampongeza Mheshimiwa Goodluck kwa mara ya kwanza ameonesha ukomavu wa kisiasa kwamba msimamo wake unabaki pale pale. Kila mhimili unapaswa kuheshimiwa na lazima tulisimamie hilo, hatuwezi kukubali. Kuna kitu kimenishangaza sana, Maazimio ya juzi tu hapa lakini naona kuna watu wameanza kugeuka, Bunge hili hili, juzi tu hapa, kuna nini kimetokea?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bado tutaendelea kusema ukimtuhumu mtu ambaye ana watu wengine nyuma hujamtuhumu yeye, tunachokizungumzia sisi ni kwamba sheria zifuatwe. Kuna watu wanaohusika na hayo mambo wafuate utaratibu, sheria ziko wazi. Makonda hawezi kumwita mtu yeyote angeagiza Jeshi la Polisi lifuate utaratibu kuwaita hao watu. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, katika mazingira ya kawaida kama kuna Mbunge ametuhumiwa, sisi tulivyoambiwa tunalala msifikiri ni mtu mmoja alisikia, ni wananchi ambao wako nyuma yetu wamejua kwamba sisi tunalala usingizi. Sasa kama tunakubaliana na Makonda kwamba kweli tunalala usingizi, kiukweli mimi binafsi kama Aida, sisi Wafipa tuna misimamo yetu, mimi siwezi kukubaliana hata siku moja. Kama kuna mtu anajua amefanya vizuri kwa kusubiri uteuzi, sisi wengine hatusubiri uwaziri hata siku moja hatusubiri, tutasimamia ukweli. Kama kuna watu wanafanya hayo mambo hakuna mtu anafurahishwa ila afuate utaratibu mambo mengine yaendelee. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi kwenye taarifa ya Kamati, niongelee kuhusu Ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali. Ndugu zangu Wabunge pale ndipo sheria zinachapwa, mtu yeyote ambaye unahusika na mambo haya ukienda kuona pale na ukaacha unafiki, ukatimiza wajibu wako kama Mbunge utaelewa hiki ninachokizungumzia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimwambia Mheshimiwa Jenista Mhagama kama kweli kuna utumbuaji kitu gani kinazuia kumtumbua yule mtu pale kwa sababu mambo yako wazi kabisa inakuwaje siri za Serikali zinakwenda kutolewa nje, kuna kitu gani kinaendelea? Tunaishauri Serikali ifanye utaratibu unaowezekana, kama mmefanya haraka kuhamia Dodoma mpaka kwenda kwenye Chuo cha UDOM, fanyeni haraka kutafuta utaratibu wa kudhibiti mazingira ya pale, kwa sababu tu moja, kwa maslahi ya nchi yetu ya Tanzania. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna suala la wanasheria wetu, yawezekana shida ni taaluma waliyo nayo au hakuna utaratibu wa kuwaangalia hawa wanasheria wa Halmashauri jinsi wanavyowajibika. Kuna watu wamehukumiwa kwa sheria hizi za Halmashauri ambazo ziko kinyume kabisa na sheria mama. Tunaishauri Serikali kuna kila sababu ya kufanya semina kwa hawa wanasheria wa Halmashauri kama kweli tuna nia njema. Kwa sababu yawezekana wanafanya kwa kutojua au kwa makusudi kwa sababu wanajua mmewatelekeza. Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana ukiangalia hata kesi nyingi za Halmashauri, nimewahi kukaa siku moja nikajiuliza kwa nini kesi nyingi za Halmashauri tukienda mahakamani tunashindwa? Kuna mambo mawili hapa, yawezekana wanasheria wenyewe wanapiga deal na hawa watu waliopeleka kesi mahakamani au Wakurugenzi wanapokuwa wanafanya shughuli zingine wanashindwa kuwashirikisha wanasheria. Haya mambo lazima tuyatazame kwa maslahi ya Taifa.