Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwasababu ni dakika tano nitachangia haraka haraka na nitaanza kwa kuchangia mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira yetu yameharibika, na sana sana yameharibika kwasababu ya mkaa pamoja na ukataji wa kuni. Watu wote mnajua kuwa Mkoa wetu wa Morogoro, Mkoa wa Pwani na nchi nzima ya tanzania kwa wastani, mara unapopita utakuta mkaa na utakuta kuni. Kwa hiyo, naomba mikakati iwekwe pamoja na Ofisi ya Makamu wa Rais kuona kuwa itafanyaje ili kuweza kutafuta nishati mbadala badala ya kutumia kuni au kutumia mkaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni karibu asilimia 90 ya Watanzania wanatumia mkaa na Dar es Salaam tu wanatumia mkaa magunia 200,000 mpaka 300,000. Kwa hiyo, naomba sana hii iweze kupewa kipaumbele kwa kuwa inaleta jangwa, joto, mvua hatupati na tabia nchi inabadilika. Kwa hiyo, naomba itiliwe mkazo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu viwanda. Nashukuru Mheshimiwa Waziri kwa kuwa tutakuwa na kiwanda cha sukari Mkulazi lakini ijulikane kuwa viwanda vingi vya Mkoa wa Morogoro havifanyi kazi. Nilikuwa nakuomba tuone jinsi ya kufufua hivi viwanda viweze kufanya kazi, Mkoa wa Morogoro ulikuwa ni mkoa wa viwanda lakini sasa hivi havifanyi kazi. Ni vizuri tuna Kiwanda cha Maji Udzungwa kinafanya kazi, Kiwanda cha Tumbaku kinafanya kazi lakini viwanda vikifanya kazi tutaweza kupata ajira kwa wakina mama pamoja na vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili viwanda viweze kufanya kazi ni lazima uwepo umeme wa uhakika, lazima yawepo maji ya uhakika na ni lazima kuwepo na malighafi na hizi malighafi lazima zitokane na kilimo. Kwa hiyo, inabidi tuangalie hayo mambo na tuangalie mikakati ya kuwa na umeme wa uhakika, maji ya uhakika pamoja na kilimo cha uhakika kinachozalisha malighafi ambazo zitaweza kuendeleza viwanda vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa sababu umenipatia nafasi hii na ahsante sana.