Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Halima James Mdee

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, na mimi mchango wangu utaongezea yale ambayo yamezungumzwa kuhusiana na dawa za kulevya; na nitarejea ukurasa wa saba na wa nane wa taarifa ya Kamati, naomba kunukuu inahusiana na mwenendo wa bajeti ya Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya, ukurasa wa saba unasema; “Hata hivyo katika kipindi cha mwaka 2015/2016, 2016/2017 bajeti za Tume zilishuka hadi kufikia sifuri kwa miradi ya maendeleo kwa mwaka 2016/2017 kutokana na ukomo wa fedha za wafadhili na kubadilika kwa vipaumbele vya Bajeti ya Serikali.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati hotuba ya Kamati inasema haya leo Mheshimiwa Rais wakati anamuapisha Mkuu wa Majeshi amesema kinaga ubaga kwamba anaunga mkono vita ambayo kwa mtazamo wake yeye imeanzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na kwamba hakuna atakayepona na kwamba wote wawekwe ndani na haangalii umaarufu. Ifike kipindi hii nchi yetu tuache kuiendesha kwa sanaa. Ninarudia, ifike kipindi hii nchi yetu tuache kuiendesha kwa sanaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya mwaka 2016/2017 ambayo Rais Magufuli anayetoa tamko la kumuunga mkono Makonda ndiyo alikuwa ameshakuwa Rais; bajeti ya maendeleo ni sifuri, na bajeti ya maendeleo ndio tunatarajia ikafanye hizi shughuli; leo anasimama Ikulu anadai eti anaunga mkono hii vita. Isipofika kipindi kama nchi tukaamua kutembelea ama kusimamia maneno tunayoyasema ama kutembelea kauli zetu haya majanga hayawezi kuisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, President Nickson mwaka 1971 wakati anaanzisha vita dhidi ya madawa ya kulevya Marekani mpaka sasa Taifa la Marekani limetumia si pungufu ya dola trilioni moja na bado wanapambana. Kwa mwaka mmoja Taifa la Marekani linatumia sio pungufu ya dola bilioni moja angalia GDP yetu halafu linganisha na dola bilioni 51; lakini vita bado ni kubwa. Leo bajeti sifuri halafu anasimama mkuu wa nchi anasema eti vita ipiganwe; tutapigana kwa viboko? Tutapiganaje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo ifike kipindi tuache kutafuta headlines na tuache kucheza na vichwa vya Watanzania kwa kutengeneza headlines kwa sababu hii vita si ya jana, si ya leo na wala si ya juzi na wala si ya mtu mmoja.
Kwa hiyo, lazima tuwe na political will na dhamira ya kisiasa haipimwi zaidi ya kwenye maandiko, huna pesa huwezi kufanya kitu, tuache usanii, tuache sanaa na tulisaidie hili Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninyi hatuwaji wauza unga sisi? Hatuwajui wanaoagiza unga sisi? Si ndio wanaotuchangia kwenye kampeni sisi? Hatuwajui? Si ndio tunakula nao sisi? Si ndio tunalala nao sisi? (Makofi)
Leo tunaenda tunakamata vitoto vya watu eti vinatumia unga; Rais anasema kamateni hao watumiaji watatusaidia kutuambia wanaouza, mzee kama hawajakwambia ukweli inawezekana kampeni zako ulichangiwa na hawa watu, hii vita ni kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, inawezekana Rais amezungukwa na watu ambao anadhani anawaamini, mimi naamini hili Baraza lina watu makini, lakini naamini kuna watu anaowasikiliza zaidi na wengine anawapuuza. Tuanze kupima na kuangalia Rais anazungukwa na watu gani. Kwa hiyo, kama leo kwa sababu kuna mtu amesema hapa inawezekana Rais ametuma tu, labda Makonda ndiyo msemaji wake siku hizi anaambiwa tangulia halafu mimi nafuata, kwa sababu haiwezekani ikawa ni coincidence. Yaani anatokea anasema kitu halafu Mzee anafuata! Hii vita if we are serious, waliokuwepo kwenye Bunge lililopita, mnakumbuka Mheshimiwa Lukuvi alipokuwa Waziri anayeshughulika na masuala ya Bunge, alituingiza kule akatuonesha sinema, anasema watu wanawajua, iko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kikwete alisema anawajua na sisi tunaamini Rais akiondoka Ikulu mafaili yanabaki Ikulu, kwa hiyo, tusikimbie vivuli vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais John Pombe Magufuli na wasaidizi wake mnanisikia, list ya waagizaji siyo watumiaji, waagizaji, wafanyabiashara wa dawa za kulevya wanaotuma watu huko nje unayo Ikulu, tunaomba fanyia kazi list iliyokuwa Ikulu, tusicheze na akili za Watanzania kwa kutafuta headlines.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila siku tunakwepa masuala ya msingi, wanaona uchumi unadorora wanamwambia mzee toka na hiki ili tu-divert minds za Watanzania, wanaona kuna njaa wanasema toka na hiki tu-divert akili za Watanzania, msitupotezee muda. Mmepewa hii nchi kwa dhamana, more than 50 years now, jana wametimiza 40 years kama chama, watu wazima yaani 40 years maana yake mtu mzima, shababi. Tu-behave kama watu wazima, tulisaidie hili Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba, niambiwe kabisa na Waziri wa Afya, kwa hizi mbwembwe mnazoanza hizi, hii kutoka zero itakuja ngapi ili tuweze basi kuanza kupambana na hili tatizo. Akina Amina Chifupa walizungumza sana humu wakaja akina Mheshimiwa Ester Bulaya na hoja zao binafsi wakaungwa mkono na Waziri Mheshimiwa Jenista, tukatunga sheria, sheria ukiisoma ni kali kwelikweli, na ile sheria ukiisoma between the lines inalenga wale mashababi, ambao inawezekana wengine, ndiyo maana yule dogo alikuwa yuko Marekani siku 20, hakuna anayejua nani kamfadhili Marekani siku 20, hana ubavu wa kuishi Marekani siku 20. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana hawa wauza unga ndiyo wanampeleka huko, anakuja anamkamata Wema, Wema kweli! Alizunguka na ninyi kwenye kampeni mlikuwa hamjui, alikuwa na Makamu wa Rais miezi mitatu, sijui Mama na Mtoto, mkapata kura za ma-teenagers kwa kumpitia huyo dogo. Kwa hiyo, siku zote yuko na Makamu wa Rais kumbe ananusa kitu Makamu wa Rais hajui, acheni usanii. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetumia muda wangu mwingi kulizungumzia suala hili, nirudie tumuogope Mungu, tuache usanii. Tunadhamira ya kuwasaidia watoto wetu hawa, tuwasaidie watoto kwa kuwapa tiba tukamate majambazi na majangili wanaoharibu Taifa letu, tumechoka maneno, tunataka vitendo sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la HIV…….
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Mdee.