Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ESTER M. MMASI: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru na mimi kunipa nafasi hii niweze kuchangia kwenye Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wajumbe walionitangulia utaona wengi wameonesha kusikitishwa ama kuwa na mkanganyiko fulani kwenye masuala haya ya D by D yaani ugatuzi wa madaraka. Leo hii Wizara ya Elimu tunaambiwa kwamba wao ni wabeba sera lakini utekelezaji wa azma hii ya kutoa elimu bora kwa Watanzania wameachiwa TAMISEMI.
Mheshimia Mwenyekiti, ifike mahali hebu tuone hili suala linahitaji umakini mkubwa sana kwa upande wa Serikali, kwa nini ninasema hivyo? Ukiangalia hapa michango yetu mingi kwenye elimu tunaongelea vyuo vikuu lakini tunapwaya sana au tunakuwa na machache sana ya kusema ama tunakuwa na insight finyu sana kwenye masuala mazima ya elimu kwa upande wa shule za misingi lakini hata sekondari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wenzangu watakubaliana na mimi, yako mambo mengi ambayo bado yanahitaji michango yetu, michango mikubwa ambayo tunaweza kusema na ifike mahali Serikali iweze kutuelewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala zima ya uendeshaji wa shule za msingi na sekondari zipo changamoto nyingi lakini solution zinazokuja hapa tunashangazwa kusikia kwamba Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa wanachukua madaraka kwa kuwafukuza walimu kuona kwamba walimu hawa ndiyo wanaosababisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najiuliza hivi viongozi hawa waliwahi kukaa chini na kufanya tathmini kujiuliza hata hii standard ambayo imekubalika kwenye mpango wa BEST taarifa ya mwaka 2012/2015 ile student ratio yaani mwalimu mmoja kwa wanafunzi 44 haya wanayasemea wapi?
Tunachosikia ni walimu kufukuzwa mashuleni hili hatutakubaliana nalo. Lakini wamejiuliza kuhusu miundombinu? Lakini wamesahau walimu wanadai satahiki zao miaka na miaka. Ifike mahali tuone kwamba tunahitaji kauli ya mwisho kabisa ya Serikali juu ya hatma ya walimu wetu, stahili za walimu, haki za walimu wetu zinalipika na tunahama kwenye hii ajenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe ni shahidi na mimi pia ni shahidi na Wabunge wenzangu ni mashahidi. Mwaka jana kwenye uwasilishaji wa bajeti ya Serikali nilipata taarifa kwa Dada yangu ninayempenda sana, Kiongozi wangu mahiri, Mheshimiwa Angellah Kairuki ambaye ni Mheshimiwa mwenye dhamana Ofisi ya Rais, Manejimenti ya Utumishi wa Umma akisema kwamba kuna Bodi ya Mishahara na wamejipanga comes this February kwamba madai ya walimu yatakuwa yamefika sehemu ambapo Serikali itakuwa na kauli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafikiri tutakapofika kwenye majumuisho tunahitaji kauli ya Serikali ni lini masuala haya yatakwisha? Tumechoka kuimba nyimbo hii miaka kenda mia, tumechoka, inasikitisha na inaumiza sana. Ukiangalia wengi hapa tumefika kwa sababu ya uwezo wa walimu wetu. Hatukufika hapa kwa sababu ya ngonjera, midomo mizuri ya kuimba ngonjera hizi, tulikaa darasani, tukaelimishwa, tukaelemika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa lililoelimika ni Taifa ambalo litafika kuthamini nguvu kazi ya Serikali na kufanya tafsiri yenye maana kwenye masuala mazima ya maendeleo. Kwa nini nasema hivi? Tumeongea masuala ya mikopo na Wabunge wengi wamechangia kwenye upande huu.
Mimi nimeenda pale chuo cha NIT majuzi hapa nikakuta pale kuna vijana wa mwaka wa pili na mwaka wa tatu, wananfunzi 38. Wanafunzi hawa hawajalipiwa ada ambao kwa ujumla wao wanafunzi hawa wanasoma programu ya uinjinia wa vyombo vya angani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana hawa wanaosoma Engineering Maintenance in Aircraft wamefika mahali wako stucked hawana pa kwenda. Mimi najiuliza kweli tunafika mahali tunashindwa kutafsiri hatua ya Serikali katika masuala mazima ya maendeleo? Leo tumeagiza ndege mbili, tuna mpango wa kuongeza ndege, lakini tumerudi nyuma kutafsiri rasilimali yetu ambayo itakwenda kuwezesha hatua hizi za Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli! Leo hatujajipanga pengine tunafikiria kwenye ku-poach lakini ni gharama sana. Sisi tunaweza kuajiri mtu wa Emirates? Hatuwezi. Tunapoanza hapa tumemchukua Mkurugenzi wa ATCL Senegal lakini pia Technical Manager wa ATCL tumemchukua Rwanda. Hawa watu tutashindwa kufika mahali kuona ufanisi wao kwa sababu tumefika mahali ambapo tunashindwa kutafsiri investment inayofanywa na Serikali kwenye masuala mazima ya maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ifike mahali tuone kwamba hawa vijana wetu wa NIT wanaosomea uinjinia na urubani pale wafike mahali Serikali iwalipie ada yao. Ada yao ni shilingi 10,500,000/=, shilingi 400,000,000 Serikali inapata ugumu gani kulipa hawa watoto wakasoma? Tutawaacha yatima mpaka lini? Lakini hatuoni unyeti, hatuoni nguvu ya Serikali tunayo invest pale na hata kuweza kuwakomboa vijana wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni gharama sana kumsomesha mwanafunzi ambaye anasoma course hii hapa NIT ukimpeleka Rwanda ni shilingi milioni 80, lakini kweli tunafika hapa kudharau na kuona kwamba comes rain, comes sun mambo yatakuwa sawa? Siyo sawa, ifike mahali tuone kwamba sisi kama Wabunge, sisi kama viongozi wenye dhamana tuna kila sababu ya kuisemea Serikali yetu na kuonesha njia pale inapobidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, masuala haya ya mikopo ni masuala ambayo inabidi kwa kweli tuweze pia kuoanisha. Leo wanamaliza wanafunzi 250,000 mathalani, lakini tunajiuliza baada ya hapa ni vipi? Tunasema hii fund iweze kuzunguka na kuweza kufikia watoto maskini zaidi na zaidi lakini mbona hakuna uwiano hapa? Wanaomaliza ajira zao ziko wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, last year hapa tumekaa, tumeongea masuala mengi, kutakuwa na Benki ya Wakulima, leo hii katika zile shilingi bilioni 55 nakumbuka, zimetoka only three percent tukasema kutakuwa na dirisha la vijana, mimi nikauliza hapa, dirisha la vijana likiwepo wanakopeshekaje hawa watu? Wakiwa na Hati za Kimila watakopesheka, God forgive! Mashamba haya nani kawapa watoto?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ifike mahali tupunguze ngonjera tuende kwenye vitendo. Tuna mengi ya kujibu tutakapokwenda kuomba kura majimboni. Ninarudia kusema kwamba Taifa lililoelimika ni Taifa ambalo litafika kukaa chini na kufanya tathmini ambayo inalenga maendeleo chanya katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni pesa nyingi sana zinapotea pale Bodi ya Mikopo. Mimi nimesikiliza, ninyi ni mashahidi, tulipitisha hapa sheria mbili juzi tu hapa, kulikuwa na ile Valuation and Valuer Registration Act ya mwaka 2016, lakini pia tulipitisha ile Procurement Act. Procurement Act ilikuwa inatambua asilimia 30 ya vijana waweze kutambulika Serikalini, waweze kufanyakazi na Serikali kwa maana kwamba kutoa service, kufanya consultancy na vitu kama hivyo. Uwezo mmewajengea wapi? Mikopo wakatoe wapi hawa vijana? Wavunje ofisi zetu? Tupunguze maneno tuende kwenye vitendo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani, tutakuwa hatutendei haki Taifa hili kama ujana wangu huu nakuja Bungeni kupaka lipstick na kupaka wanja na kurudi nyumbani, haiwezekan! Mimi sitakuwa tayari kupaka lipstick hapa ndani na wakati vijana hawana kazi, tutakuwa hatutendei haki Taifa hili. Sisi ni vijana akina Mheshimiwa Bulembo mnisikilize, tusimame hapa na tuisemee Serikali yetu kwa nia njema kabisa, lazima vijana watambuliwe, lazima vijana wapewe status yao katika hii nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mengi ya kusema nafikiri nikiendelea naweza nikatoa machozi, naomba niishie hapo.