Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

Hon. Salma Mohamed Mwassa

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

MHE. SALMA M. MWASSA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii nami nichangie Mpango wa Pili wa Maendeleo.
SPIKA: Jitahidi sauti kidogo, weka vizuri hiyo microphone.
MHE. SALMA M. MWASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Naomba nami nichangie Mpango wa Maendeleo. Kwanza kabisa naomba nichangie kuhusu masuala ya maji. Mpango umejikita zaidi kusema kwamba utajenga miundombinu mipya kuhusu masuala ya maji, lakini haukueleza kipaumbele katika mikoa mingi ya Tanzania.
Kwa mfano, katika Jiji la Dar es Salaam, ni kweli Serikali imejitahidi kuanzisha mradi mkubwa wa maji kutoka Ruvu Chini Bagamoyo kwenda Dar es Salaam na kutoka Mtambo wa Ruvu Juu kuja maeneo ya Kibamba, Mbezi na mpaka katikati ya Jiji, lakini haikuangalia upungufu uliopo.
Mheshimiwa Spika, upungufu uliopo kwa Jiji la Dar es Salaam, tunahitaji lita milioni 450, lakini kwa sasa wakazi hao wa Jiji la Dar es Salaam wanapata lita milioni 180 na kama maji haya ya Ruvu Chini yatafunguliwa kwa mkakati wa huu Mpango mpya, wanatarajia kupata lita 270. Sasa najiuliza, Mpango unasema kwamba watahakikisha kabisa kwamba matatizo ya maji hayatakuwepo tena hasa katika Jiji la Dar es Salaam: Je, hizi lita milioni 130 hata kama huo mradi mpya utatekelezwa, zitakuwa covered wapi? (Makofi)
Vile vile, nije katika masuala ya miundombinu. Miundombinu ya maji katika Jiji la Dar es Salaam ni michakavu sana, lakini ukiangalia mradi ule mkubwa haukuangalia kwenye kusambaza miundombinu mipya, unasema tu kukarabati ile ya zamani. Ukiangalia, maji yanapotea kwa wingi mno kutokana na miundombinu chakavu.
Mheshimiwa Spika, mara nyingi unakuta barabara nyingi hizo ambazo Mheshimiwa pale alisema kwamba zimejengwa kwenye Jiji la Dar es Salaam, lakini unazikuta mara kwa mara zipo kwenye madimbwi ya maji, mafuriko. Siyo tu kwa sababu ya mvua, bali ni haya mabomba ya DAWASCO ambayo mara nyingi huwa yanapasuka. Kwa hiyo, miundombinu ile ni chakavu, ni mibovu! Hivyo, hata kama yale maji yatafunguliwa, hizi lita milioni 270 hazitaweza kufika kule kutokana na miundombinu ile chakavu mno. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niishauri Serikali kwamba, kabla ya kuyasukuma yale maji kwenye ule mradi mpya, ianze kwanza kutengeneza mikakati ya miundombinu mipya, iondoe kabisa ile miundombinu ambayo ni chakavu na siyo kukarabati, iondoe kabisa. Kule ambapo ni maeneo ya pembezoni kama Bunju, Mabwepande iendeleze kusambaza ile miundombinu ya maji mipya ili wananchi wote wa Jiji la Dar es Salaam wapate maji kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hivi kweli tunaongelea miaka 54 ya Uhuru, Jiji kama la Dar es Salaam, ndiyo Tanzania, lakini watu bado ni shida kabisa, yaani wakisikia maji yanatoka, wanalala kwenye mabomba. Sasa je, mtu kama wa Katavi huko sijui wapi, itakuwaje? Yaani bado sijaelewa kabisa! Maana yake ukiongelea Tanzania, ndiyo unaongelea Dar es Salaam; sasa kama Dar es Salaam hakuna maji ya kutosha, mpaka sasa hivi bado watu ni shida, wanaishi kwa kuchimba visima, wanaishi kwa kuhangaika huku na kule, sasa maeneo kama hayo ya pembezoni yatakuwaje? (Makofi)
Kwa hiyo nashauri, Serikali ije na mpango mkakati mpya wa kuangalia je, maji yatapatikana vipi? Vilevile isitegemee tu Ruvu, kuna mito mingi inayozunguka Jiji la Dar es Salaam. Kuna Wami! Kwa nini tutegemee tu chanzo kimoja tu cha Mto Ruvu? Kuna mto Rufiji ambao unaweza ukaleta maji mengi zaidi kuliko sasa.
Mheshimiwa Spika, vilevile nijikite pia kwenye elimu. Serikali katika Mpango imeongea zaidi kuhusu kuongeza vijana wetu kwa ajili ya viwanda na Elimu ya Juu, lakini utaongeleaje Elimu ya Juu bila kuongelea Elimu ya Awali, Elimu ya Msingi na Elimu ya Sekondari? Huko juu atafikaje? Ukiangalia miundombinu ni mibovu kabisa!
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, Mpango haujasema kabisa kuhusu Shule za Awali. Shule za Awali tunaona tu ni hizi tu za binafsi ndiyo zinazofanya vizuri, lakini hakuna mikakati ya kusema kwamba Shule za Awali itakuwaje, hakuna mikakati ya kusema kwamba miundombinu kama ya madarasa, vyoo kwenye shule zetu za msingi itakuwaje, hakuna mikakati ya kusema kwamba Sekondari itakuwa vipi? Kwa mfano, Sekondari za Kata, ukiangalia ndiyo zinazozalisha mabinti ambao wanapata mimba, kwa sababu hazina mabweni, hazina nini. Sasa unasema tu elimu itaboreshwa, lakini sioni miundombinu yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukiangalia katika Jiji la Dar es Salaam lina upungufu mkubwa, kwa mfano, sasa hivi kutokana na elimu bure, darasa moja watu wameandikishwa labda wanafunzi 1,000. Sasa kama hakuna mkakati wowote, hii ni mwaka huu tu; wanafunzi I,000, wengine 900; kuna shule moja huko Mbagala unakuta wameandikisha karibu 2,000. Sasa unajiuliza, je, mwakani itakuwaje? Nikiangalia huu Mpango hakuna kabisa mikakati ya kuongeza miundombinu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vile vile nisemee kuhusu gender kwenye hii hii elimu. Huko nyuma shule nyingi zilikuwa ni Kilakala, Msalato kwa ajili ya wasichana tu. Naomba tu tuangalie jinsia ya kike kwenye mambo ya elimu. Zijengwe tena zile kwenye mikakati tena, ziongezwe kama hiyo Msalato, Kilakala ziwepo na nyingine na nyingi ambazo ni za kikanda zinazohudumia wasichana tu. Siyo wanafunzi wa kike kuwapeleka kwenye Shule za Kata.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, mtu anafaulu, wazazi wanakaa labda let‟s say Magomeni, mtu anasoma sijui Kimara huko Bonyokwa, kwa mfano katika Jiji la Dar es Salaam, sasa huyo mwanafunzi sijui apande pikipiki amalize, apande gari, mtoto wa kike itakuwaje?
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Serikali ijikite tena kuangalia miundombinu hasa kwa mtoto wa kike kwamba tuwe na zile Special School kwa ajili ya wasichana tu kama ilivyokuwa awali hizo Shule za Special School unakuta ziko nyingi.
Mheshimiwa Spika, vile vile nijikite kwenye viwanda. Serikali inasema kwamba inaongeza uchumi wa viwanda, ndiyo kipaumbele cha Mpango, lakini bado napata tabu. Hapa inaongelea viwanda vikubwa zaidi, lakini kuna vile viwanda vya mikono (handcraft), haijaongelea kabisa kwamba itavifanyaje na ndivyo vinavyoajiri watu. Hivi ukiongelea viwanda vikubwa (modern technology) lakini hujaongelea viwanda kama SIDO, hivi vya mikono, unarukiaje kwenye vikubwa?
Mheshimiwa Spika, tukiangalia huko nyuma, viwanda hivyo vilikuwepo vingi, ni nini kimeua? Yaani utaendaje kusema kwamba viwanda vitakuwa vikubwa! Nakumbuka miaka ya nyuma SIDO ilikuwa ndiyo solution ya hawa vijana wetu kupata ajira na akina mama. Kwa hiyo, nilitegemea kwamba Serikali ingekuja na mpango kwanza wa vile viwanda vidogo vidogo kama SIDO viwekwe kila Mkoa kama ilivyokuwa huko nyuma, yaani wanawake walikuwa wanajifunza angalau kutengeneza batiki, wataweka vile vifungashio na kadhalika.
Mheshimiwa Spika, Mpango ungeangalia viwanda kama hivyo vidogo vidogo kwanza kabla ya kwenda kwenye Viwanda vikubwa. Unapoongelea viwanda vya nguo, mbona hujamwangalia mama anayetengeneza batiki utafanyaje? Kwa nini uiangalie Sunguratex, sijui Mwatex lakini hujamwangalia mama kama huyu anayetengeneza batiki? Kuna nguo za pamba za kienyeji, zipo tu. Katika viwanda vile, yaani wale watu wangepewa kipaumbele kwanza. Kabla ya kwenda katika hivyo viwanda vikubwa, tuangalie kwanza hivi vidogo.
Mheshimiwa Spika, vile vile niangalie tena kwenye mambo ya afya. Nashukuru kwamba Mpango umejikita zaidi kwenye hospitali kubwa, imeliona hilo, kwamba hospitali kubwa ndiyo zina mlundikano wa wagonjwa sana. Imeongelea Taasisi ya Mifupa (MOI), imeongelea Muhimbili, ikaongelea hospitali za Kanda, lakini haikuongelea kabisa Hospitali hizi za Kata na Wilaya.
Sasa kwa mfano, unaiimarisha Muhimbili, lakini umeacha Hospitali hizi za Kata kwa mfano, labda Kata ya Mbezi, Mbagala na nyingine za pembezoni. Halmashauri zimejitahidi, zimejenga vizuri, labda kila Kata ina Hospitali yake lakini zile Hospitali hazina vifaa, kama ni labour unakuta ni chumba kitupu peke yake. Hivi mtu atajifunguaje kwenye chumba hamna kitanda, hamna nini? Kile kitanda unakinunua kwa Hospitali ya Muhimbili tu, lakini huangalii kabisa Hospitali kama hizo za Kata ambazo zingepunguza msongamano wa wagonjwa.
Kwa hiyo, naomba Serikali kwa kushirikiana na Halmashauri ijenge hospitali kila Kata. Labda kwenye mambo kama haya ya vifaa tiba, vile vile isijaze tu Muhimbili au MOI, tusiziangalie hizi kubwa, kwa sababu ndiyo tunaleta mlundikano wa wagonjwa. Unakuta kila mtu hawezi kwenda kujifungulia hospitali labda ya Manzese, sijui hospitali ya wapi huko yaani ile ya Kata, haiwezekani, kwa sababu kwanza haina wataalam, haina hivyo vifaa tiba, majengo yenyewe hovyo hovyo tu. Kwa hiyo, mtu anaona kabisa kwas ababu Muhimbili ndiyo kwenye vitanda vizuri, ndiyo kila kitu, kuliko nikalale hizi hospitali za kawaida, bora niende kwenye hizo hospitali kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda pia Serikali ingejikita kwenye hospitali hizi kwa ajili ya kuangalia mambo ya wanawake na watoto. Kwa mfano, nikiangalia Mpango ule uliopita, ulifeli kabisa ku-control vifo vya akinamama. Vifo vya akinamama na watoto vilikuwa vinaendelea kuongezeka.
Kwa hiyo, napendekeza kwamba Serikali ingejenga hospitali za Kanda special kwa ajili ya mama tu na mtoto na kuongeza Madaktari Bingwa kwa ajili ya mama na mtoto peke yao. Yaani hizo ziwe special! Ziwe kwenye kila kanda ambazo zitatibia watoto na akinamama na kuweka Madaktari bingwa, kuliko kwenda kuwachanganya akinamama kama labda kwenye hizo hospitali kubwa. Yaani haieleweki, huku kuna wagonjwa hawa; huku kuna wagonjwa hawa! Kwa kweli mama na mtoto anahitaji special care ili tuweze kupata Taifa endelevu na ili kupata Taifa endelevu na sahihi, ni lazima hizo hospitali za rufaa za akinamama na watoto ziwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa nijikite kuangalia kilimo. Mpango huu umeeleza kwamba kilimo ndiyo uti wa mgongo na ndiyo kipaumbele. Toka Uhuru nasikia hivyo hivyo, toka nikiwa nasoma; uti wa mgongo wa Taifa ni kilimo, lakini cha kushangaza sasa kilimo hicho hakiwekewi mikakati. Hakuna wataalam, hakuna pembejeo! Kwa mfano, leo ukiangalia mtu ni mkulima kila siku ni kulalamika tu, hivi Vyama vya Ushirika ndiyo vilivyokuwa vinatetea haki za hawa wakulima; Vyama vyenyewe havieleweki lakini mpango haujaja kutueleza kwamba hivi Vyama vitakuwa vipi? Hawa wakulima wapate hizi mbegu wapi? Hawakuongea! Bado Serikali haijaona kuwa hili ni tatizo.
Mheshimiwa Spika, kuna research mbalimbali zilikuwa zinafanyika, kwa mfano, research kwa ajili ya kahawa, chai, lakini zote hizo sasa hivi hazieleweki kama zinaendaje. Haziko! Mkulima huyu anasaidiwa vipi? Yaani ukiangalia kwa mfano, pembejeo, ziko juu mno! Wataalam wa Kilimo, vitu kama mashamba darasa yangekuwepo kila Kata. Kwa hiyo, naishauri Serikali kwamba…
SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Salma.
MHE. SALMA M. MWASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.