Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Ahmed Mabukhut Shabiby

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Gairo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa namshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake ambayo imegusa kila sekta na kila kona ya nchi yetu. Vile vile namshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na wasaidizi wake kwa kuwezesha vijana zaidi ya 1,000 kupata ajira katika Kiwanda cha Nguo cha Morogoro wakiwepo vijana wa Wilaya yangu. Nawashukuru kwa hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo nitaanza na pombe ya viroba. Najua wengi watashangaa, watasema huyu jamaa Muislam; na najua wale watu wanaopenda kuweka maneno kwenye midomo ya watu wengine, wataweka maneno mengi. Siyo kwamba naunga mkono watu wanywe viroba, napinga na viroba visiwepo kwa sababu vinaathiri hali za watu na hata sasa hivi watu wananenepa baada ya viroba kuacha kuwepo mitaani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nashauri kitu kimoja; kwa sababu katika bajeti ya mwaka 2016 wakati tunaweka kodi katika vinywaji na katika bajeti yetu na mapato yetu, hata viroba navyo tulivihesabu na vilikuwepo kihalali.
Mheshimiwa Spika, ni kweli pombe hii inadhuru watu, lakini naomba au nashauri kwa wakati mwingine utaratibu utakaotumika kuzuia vitu kama hivi, basi uchukuliwe kwa umakini sana. Waanze kuzuia kwenye production ili huku zinakouzwa, basi ziishe.
Mheshimiwa Spika, mimi ni mfanyabiashara sikuingia hapa kama nachunga ng’ombe wala kama mkulima au nani, nimeingia kama mfanyabiashara.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni lazima nizungumze habari ya biashara na kama sisi Wabunge wa vyama vyote hapa tusipozungumza wenyewe basi tujue biashara kwenye nchi hii itakufa. Kwa sababu mtu amenunua mali ya shilingi bilioni moja, shilingi milioni 300 halafu amenunua kisheria, ana risiti zote za TRA na amelipa kodi leo unakuja unamwambia kuanzia sasa hivi hii mali ni haramu. Tayari ameshaingia kwenye matatizo amekopa katika mabenki huko na biashara yake imeshafungwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba mnielewe vizuri, siungi mkono unywaji wa viroba lakini utaratibu uliotumika naomba usirudiwe tena. Kwa sababu leo anaweza akaja mtu hapa akasema tena kitu kingine kikaleta madhara. Kwa hiyo, tuangalie utaratibu mzuri wa kufanya mambo haya. Hilo la
kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la pili, wewe mwenyewe Spika ni shahidi kwa sababu kati ya watu wanaoathirika na jambo hili ni mimi na wewe. Wakulima wetu ambao wanalima katika upande wa Wilaya ya Kiteto wamekuwa wananyanyaswa kupita kiasi hasa na vyombo vya dola ambavyo viko pale wilayani na mkoani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika Mbuga ya Murtangos wanasema ile ni hifadhi. Hawawazuii watu kulima wakati wanakwenda kulima, wanangoja mahindi yameshafika labda mwezi mmoja, wanakuja ng’ombe wanachungia mule wakienda wale wakulima kushtaki na wao wanawekwa
ndani. Mpaka sasa hivi ninavyozungumza wapo watu wa Pandambili ambayo ni wilaya yako na wapo watu wa Gairo wapo ndani mpaka sasa hivi na wale Wamasai ambao wanachungia kwenye ile mbuga wapo nje, hao jamii ya kifugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama mnataka kuzuia, hatukatai kuzuia, kwa nini msizuie wakati wanalima mnakuja kuzuia wakati mahindi yameshakuwa makubwa? Kama hiyo ni hifadhi, hifadhi gani ambayo ng’ombe wanachungwa lakini wakulima hawaruhusiwi, hiyo ni hifadhi ya aina gani?
Naomba viongozi wetu na Mheshimiwa Waziri Mkuu wetu ambaye ni mtiifu na msikivu akienda pale asisikilize masuala ya wilayani wala mkoani, aangalie tu yeye mwenyewe atume watu wake wachunguze atapata jibu ambalo lipo sahihi. Akitaka na majina nitampa ya wakulima wetu ambapo zaidi ya heka 3,000 watu wamechungia na wako nje halafu tunasema zaidi ya asilimia 80 ya wananchi ni wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata hizi pesa, watu wanasema tu, pesa zimepotea, hamko kwenye mzunguko wa kibiashara, ukiujua vizuri mzunguko wa kibiashara pesa imepotea kwa sababu wakulima wa mwaka jana hawajapata mazao. Hawa wakulima wadogowadogo wangeweza kuvuna
mwaka jana kila mtu hapa angefanya biashara na mzunguko wa pesa ungekuwa mkubwa. Tunasema tu aah Magufuli kazuia pesa, Magufuli kafanya nini, Serikali imezuia pesa, wakulima hawakuvuna mwaka jana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi ni mfanyabiashara sasa hivi nina zaidi ya miaka 25, najua mwaka wowote mkulima mdogo anayelima heka mbili au tatu akipata mazao atakwenda kwa fundi cherehani atanunua sare, atakwenda kwa huyu atanunua maji, atakwenda kwa huyu atanunua
hiki, ndiyo mzunguko. Yule naye biashara yake ikitoka atapanda basi, ataenda Dar es Salaam, kwa hiyo kila mtu atafanya biashara. Wakulima hawa wasipopata pesa ina maana mzunguko haupo, kila kitu kitakuwa kibaya tu, tutalalamika tu. Hata ukiachiwa hizo pesa za benki, unasema
mkopo hakuna, hata ukiachiwa, security zenyewe unazo? Maana yake mabenki siyo rafiki wa mtu maskini, huo ndio ukweli.
Mheshimiwa Spika, kuna jambo lingine la matrekta. Tunashukuru matrekta 1,860 yale ya SUMA JKT yamekuja na waliwakopesha wananchi kwa kulipa asilimia 30. Hata kwangu Gairo pale nimepata matatizo makubwa sana maana niliambiwa Mbunge weka dhamana, nimeweka
dhamana nyingine badala ya kuandika jina la niliyemkopea limeandikwa jina Ahmed Shabiby ndiyo kakopa. Sawa watu wangu nawajua najua tu yatalipwa lakini wakati SUMA JKT anapewa auze matrekta hajui hata sheria za kuuza, kwanza na yeye mwenyewe akatafuta tena dalali mwingine ndio amuuzie. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, halafu baada ya hapo haya matrekta hata ukilipa hupewi kadi wala halina namba, kwa hiyo, linatembea tu kama mkokoteni wa ng’ombe. Tafuteni watu wote wenye matrekta haya, waliopewa kadi hawazidi 300. Mkulima akiomba kadi anaambiwa hebu soma engine number, wewe angalia namba yoyote bandika, sasa anabandika namba ipi, atakataje insurance? Kwa hiyo, matrekta yale hayana namba sasa sijui ni utaratibu gani. Halafu leo tena mnakwenda mnakamata, mnafanya kuangalia rangi, lile la bluu wanakimbiza wanakamata
yamejaa pale, hii ni dhuluma? Mkulima anataka umpe kadi yake akumalizie deni humpi, kwa sababu ameshaambiwa na wenzake waliomaliza madeni kwamba hatupati kadi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa matrekta yote ya Manyara, Tabora na Tanzania nzima kwa ujumla yamekamatwa halafu watu tunasifia tunasema hawa wameshindwa kulipa madeni, wameshindwa nini, jamani tusiwaangushe hawa wakulima wetu tuwaombee tena yaje matrekta mengine wakope, tuangalie kosa liko wapi. Naomba Waziri anayehusika aende akachunguze kama SUMA JKT wanazo registration cards za haya matrekta. Hakuna namba, hata insurance atakataje? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine ni maji. Leo maji nimeamua kuzungumzia chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Toka mwaka 2007, Gairo imepewa Sh.6,600,000,000, lakini kilichofanyika wamekwenda kuchimba visima vile vya maji tisa vinatoa maji lakini yale maji hata akinywa ndege anatapika. Haijawahi kutokea. Wamekwenda kupima kwa Mkemia hayafai. Nimewapa ushauri wa kila aina hawajafuata ule ushauri, sasa miaka 10 na mimi Mbunge nakwenda hiki kipindi cha tatu, kwa hiyo, hata wale wananchi wangu kwa sababu wengine hawana uelewa wanasema Mbunge amekula pesa alipewa yeye hela za mradi kafanyia biashara zake sasa maji hakuna. Nimewaambia basi huu
mradi kama mmefeli hizi pesa zilizobakia kuna chanzo cha maji kiko pale karibu tu, kilometa kama 25, nunueni basi mabomba tupate maji ya mserereko lakini imekuwa hadithi. Ukiongea hapa unajibiwa hiki lakini hakuna linalofanyika. Tunakwenda kwenye uchaguzi hiyo miaka ijayo, pesa zipo lakini hazitumiki, ndiyo maana leo nimeamua kumwachia Mheshimiwa Waziri Mkuu alifuatilie suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu niende naye Gairo, hapa na Gairo saa moja tu, aende akashuhudie matenki yamejengwa, mitandao ya matenki ipo lakini kuvuta tu maji kupeleka pale sasa hivi mwaka wa kumi hakuna kinachofanyika. Ndiyo na pesa ipo. Kila siku ukiwaambia kaleteni maji ya mserereko hakuna kinachofanyika. Wamekuja watu ambao wameletwa na Wizara ya Maji wamechora ramani wamefanya kila kitu lakini bado hatupati maji. Kila nikiongea na Mheshimiwa Waziri anasema subiri kidogo safari hii tayari wewe maji umepata, sasa maji nimepata yako wapi, haya maji nitasema mpaka lini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama unavyojua Jimbo la Gairo watu wanalima sana, wanapata sana mazao lakini tatizo maji yake chini ya ardhi yako mbali na hasa pale Gairo Mjini huwezi kupata maji matamu hata ufanye nini, utapata tu haya maji ya chumvi. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu safari hii angalau aje Gairo pale kwa sababu yeye kidogo wakimwona na akifahamu maendeleo ya pale ya miaka kumi na asilimia iliyofikiwa mpaka sasa hivi kwa kuona kwa macho itasaidia. Ndiyo maana leo hili suala la maji nimeona naweza nikakosa nafasi kwenye Wizara ya Maji nimuachie Waziri Mkuu ili siku nyingine mwakani kama hakuna maji mimi nitachangia tena Wizara hii hii nimuulize Waziri Mkuu imekuwa vipi. Mheshimiwa Spika, ahsante sana.