Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

Hon. Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

MHE. OMAR M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote kabla sijaanza kuchangia juu ya Mpango huu wa Serikali, napenda kwanza nikushukuru wewe na niwashukuru Wanakilindi walionipa fursa hii ya kuweza kuwa Mbunge wao wa Jimbo la Kilindi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimepitia Mpango huu, una mambo mengi mazuri, nami naamini kabisa nia ya Serikali hii ni kuleta maendeleo ya dhati kwa wananchi wa nchi hii ya Tanzania. Mpango huu umeangalia mambo muhimu sana ambayo kwa muda mrefu yalikuwa hayaendi sawasawa, sasa basi ni mambo gani ambayo nayadhamiria kwa leo kuyazungumzia? Nitaanza moja kwa moja kwenye Sekta ya Mawasiliano tunapozungumzia barabara.
Mheshimiwa Spika, suala la miundombinu ni suala muhimu sana, nikiamini kwamba miundombinu ikiwa ni mizuri, basi maendeleo ya maeneo mbalimbali na ya nchi kwa ujumla yataweza kufanikiwa. Katika eneo la barabara, naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuliwekea uzito unaostahili kwa sababu maeneo mengi yalikuwa hayapitiki hususan barabara katika kiwango cha lami. Hili limeweza kufanikiwa, nami naomba niipongeze Serikali katika suala hili.
Mheshimiwa Spika, katika eneo langu ambalo nimetoka katika Jimbo la Kilindi, kuna mpango wa kuijenga barabara ile kwa kiwango cha lami ambapo barabara ile itaanzia Handeni kwenda Kibirashi hadi Kiteto kupitia Namrijo Juu pamoja na Jimbo la Mkoa wa Singida.
Mheshimiwa Spika, nataka nilizungumzie suala hili kwa sababu kama nilivyozungumza awali kwamba mawasiliano ni kitu muhimu sana, katika eneo langu ninalotoka kuna mazao yanalimwa hususan mahindi na utakuta hata nchi jirani mazao mengi yanakuja kuchukuliwa Jimbo la Kilindi, lakini kwa sababu miundombinu siyo mizuri, unakuta mazao mengi yanaishia kuozea katika mashamba.
Mheshimiwa Spika, namshauri kaka yangu, Mheshimiwa Profesa Mbarawa pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri waliangalie hili, japokuwa najua kwa mwaka huu wa fedha unaoanza Julai hautakuwepo Mpango huu, lakini barabara hii ipewe kipaumbele cha hali ya juu kwa sababu italeta maendeleo ya dhati kwa wananchi wa Kilindi na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, sehemu nyingine ambayo ningependa kuchangia ni Sekta ya Madini. Nimeona imezungumziwa hapa; na tunapozungumzia madini, tunazungumzia Sekta ya Nishati. Ni kweli kwamba umeme ndiyo kila kitu na Mheshimiwa Waziri hususan Waziri wa Nishati na Madini, ameweza kuweka mipango mizuri sana juu ya nishati, lakini nishati hii haijafika maeneo mengi hususan katika vijiji.
Mheshimiwa Spika, nitolee mfano tu katika Jimbo langu la Kilindi. Tunavyo vijiji kama 102, lakini vijiji vichache sana ambavyo vimenufaika na huduma hii ya umeme kwa maana ya REA, ushauri wangu ni kwamba, yale maeneo ambayo kwa asilimia kubwa wameshapata huduma hii, basi waangalie maeneo mengine ambayo hayajanufaika na huduma hii, kwa sababu wananchi hususan wa vijijini wanahitaji umeme kwa ajili ya maendeleo, wanahitaji umeme kwa ajili ya shughuli mbalimbali. Ni imani yangu kwamba Serikali italiangalia hili kwa umuhimu wa juu sana.
Mheshimiwa Spika, lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni suala la maji. Maji imekuwa ni kilio, kila Mbunge anayesimama hapa anazungumzia suala la maji. Labda tu nizungumzie kwa eneo ninalotoka mimi. Ni kwamba eneo lile lina maji mengi sana lakini hatuna visima na miundombinu kwa kweli ni ya muda mrefu kiasi kwamba maji imekuwa ni tatizo kubwa sana.
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwa Mheshimiwa Waziri wa Maji ni kwamba, maji yanapotea sana. Kuna Mpango kule wa bwawa katika Kata ya Kibirashi; utaratibu ule wa kuhifadhi maji kwa njia ya mabwawa ni utaratibu mzuri sana. Badala ya kuchimba visima tuwe na njia ya kuweza kuhifadhi maji kwa njia ya mabwawa. Nadhani utaratibu huu ni mzuri sana. Ni utaratibu ambao unaweza ukaisaidia Serikali kupunguza kero ya maji kwa muda mrefu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, utakuta sasa hivi mvua zinanyesha kule lakini maji mengi yanapotea kwa sababu hatuna utaratibu mzuri wa kuhifadhi maji. Nadhani muda umefika sasa, tuone namna ya kuwashirikisha wananchi pamoja na Serikali juu ya kuweka visima au kuweka mabwawa ambayo yanaweza kuhifadhi maji kwa muda mrefu. Kwa sababu ukiangalia katika eneo langu, siyo rahisi kusema labda maji yatoke Ruvu yafike Kilindi; lakini njia mbadala ambayo inaweza kusaidia kutatua tatizo hili la maji ni kuhakikisha kwamba tunakuwa na mabwawa.
Mheshimiwa Spika, naishukuru Serikali yangu kwamba imeweza kuliona hili, tuna bwawa la mfano kabisa ambalo halijakamilika, liko Kata ya Kibirashi. Bwawa hili litawanufaisha wafugaji pamoja na wakulima, naishukuru sana Serikali yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo ningependa kugusia ni suala la viwanda. Nimeona Serikali yetu ina mpango mzuri sana wa viwanda hususan kufufua viwanda vya zamani pamoja na viwanda vipya. Naomba niipongeze Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi katika hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa kinachonishangaza hapa, ukiangalia upande wa Tanga ambapo tulikuwa na viwanda vingi sana; tulikuwa na viwanda vya matunda, lakini viwanda vile vimekufa. Nashauri kwamba muda umefika wa kuvifufua viwanda vile pamoja na kuanzisha viwanda vingine.
Mheshimiwa Spika, eneo ninalotoka kuna wafugaji wengi sana, lakini nikiangalia Mpango huu, sioni namna ambavyo wananchi hususan wafugaji wa Wilaya ya Kilindi wanaweza kunufaika na Mpango huu wa viwanda vidogo vidogo. Sasa najiuliza, mifugo hii ambayo Wanakilindi wanayo, watanufaika na nini katika hili? Namshauri kaka yangu Mheshimiwa Waziri wa Viwanda pale aangalie namna ambavyo tunaweza na sisi wananchi wa Kilindi tukaweza kupata kiwanda kidogo cha kuweza hata kutumia maziwa haya mengi ya mifugo ya Wilaya ya Kilindi ili wananchi waweze kunufaika na fursa hii ambayo wanapata wananchi wa sehemu nyingine.
Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo ningependa kuchangia ni suala la utalii kwa ujumla. Ni kwamba eneo la utalii ni eneo muhimu sana ambalo naamini Serikali yetu lazima itie msisitizo wa hali ya juu sana. Wengi wamezungumza hapa kwamba watalii wanafika Kenya, halafu wana-cross wanakuja Tanzania. Hili limeelezwa kwamba mpango mzuri wa Serikali ni kununua ndege kusaidia kufanya watalii waweze kufika nchini kwetu kwa urahisi zaidi.
Mheshimiwa Spika, napongeza mpango huu, ni mzuri na wale ambao wana-discourage suala hili, naona hawako pamoja na sisi. Naomba Serikali yangu iendelee mbele na utaratibu huu. Pia kuna maeneo ambayo Mheshimiwa Waziri wa Utalii naona hawajafika maeneo mengi, labda nitoe mfano mmoja, katika eneo ninalotoka, kuna Mbuga ya Wanyama ya Saunyi. Mbuga ya Saunyi ina wanyama wa aina mbalimbali, lakini nina wasiwasi kama Serikali inajua kama kule kuna mbuga za wanyama.
Mheshimiwa Spika, fursa ile inawezekana hata wanyama ambao wanachukuliwa kwenda nje ya nchi, wanachukuliwa kutoka kule kwa sababu sijawahi kusikia hata siku moja watu wanaizungumzia Mbuga ya Saunyi.
Mheshimiwa Spika, nashauri kwamba ili tuweze kuimarisha utalii, ni kwamba Serikali iwe na utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba kila fursa ya utalii iliyopo, inatumika vizuri. Haya ni mambo ya msingi ambayo wenzetu wa nchi jirani wameweza kuzitumia na kwa hakika uchumi wao umeweza kwenda juu sana kwa kutumia utalii vizuri. Nina imani kwamba tunavyo vivutio vingi sana lakini Serikali haijatumia vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia napenda kuchukua fursa hii kuzungumzia changamoto ambazo tunazipata katika madini. Ni kwamba nchi yetu ina madini mengi sana, maeneo mengi yana madini na Wilaya ninayotoka mimi, Jimbo langu la Kilindi lina maeneo mengi sana yenye madini, lakini wachimbaji wadogo hawajaweza kunufaika na Mpango huu. Hawajanufaika pengine kwa sababu ya sheria zilizopo.
Mheshimiwa Spika, nitoe mfano mmoja tu kwamba hawa wachimbaji wadogo wadogo ndiyo watu wa kwanza ambao huwa wanagundua wapi pana madini. Mchimbaji huyu mdogo akishapatiwa license, inapokuwa muda wake umepita, hapewi fursa mchimbaji huyu kwa sababu hana uwezo. Unakuta license hizi wanaopewa watu wengine wenye uwezo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo hili limeleta malalamiko makubwa sana na namwomba kaka yangu Waziri wa Nishati na Madini aliangalie tena na atakapoleta Muswada wake hapa tuangalie upya sheria hizi zinazohusu wachimbaji wadogo wadogo kwa sababu naamini Serikali ina nia nzuri ya kuwawezesha wananchi wadogo ili waweze kusimama vizuri kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, haya mambo ni ya msingi sana kwa sababu sisi kama Wawakilishi wao tunapata malalamiko mengi sana hususan katika maeneo ambayo yana wachimbaji wadogo wadogo. Ni imani yangu kwamba itakapofika muda wa kuchangia Bajeti ya Nishati na Madini, hili tutalichangia kwa nafasi nzuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine ni elimu. Elimu ni kila kitu. Elimu imezungumzwa hapa na nashukuru kwamba Serikali imeliangalia kwa kulipa kipaumbele. Kama alivyozungumza Mheshimiwa mwingine aliyepita hapa, amezungumzia juu ya kuvipa kipaumbele hivi Vyuo vya VETA. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Vyuo vya VETA vimeweza kuinufaisha nchi hii kwa muda mrefu sana hususan wanafunzi ambao hawajapata fursa kwenda Sekondari. Nashauri kila Wilaya, kila Mkoa, ikiwezekana tuwe na VETA ili iweze kuwasaidia vijana wetu, kwa sababu tumezungumzia kwamba tunataka tuwe na viwanda. Viwanda hivi watendaji au wafanyakazi hawatakuwa ni ma-graduate peke yake, ni lazima tutahitaji kada za katikati ambazo zitazalishwa kutokana na VETA.
Mheshimiwa Spika, katika Jimbo langu nilikuwa nafuatilia kabla sijawa Mbunge, ni kwamba kulikuwa na ahadi ya kujenga Chuo cha VETA katika Jimbo la Kilindi Kata ya Kibirashi. Bahati mbaya ahadi hiyo imekuwa ni hewa, lakini naamini kabisa Serikali yangu ni sikivu, watanisikiliza na wataweza kutimiza wajibu wao katika hili, kwa sababu wananchi wanahitaji VETA kwas ababu watoto wengi hawapati fursa ya kupata mafunzo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimezungumzia hili kwa uchungu mkubwa sana kwa sababu maeneo tunayotoka sisi, wananchi vipato vyao ni vya chini sana na sio wote ambao wana uwezo wa kupeleka watoto wao sekondari. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, labda nikwambie tu, Wilaya yangu ya Kilindi kwa mwaka huu imekuwa ni Wilaya inayoongoza kimkoa katika matokeo ya Kidato cha Nne mwaka 2015. Naomba kwa niaba ya Halmashauri ya Kilindi, nimshukuru pia Waziri wa Elimu kwamba amefanya jitihada kubwa sana kuhakikisha kwamba pamoja na changamoto nyingi tulizonazo tumeweza kusonga mbele.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.