Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalenga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Spika, nakushukru sana kwa kunipa nafasi. Awali ya yote, kwanza nipende kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri lakini vilevile niweze kumshukuru Mheshimiwa Jenista Mhagama na msaidizi wake Mheshimiwa Anthony Mavunde kwa kazi nzuri ambazo wameendelea kuzifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jioni ya leo napenda kuzungumza machache kuhusu hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Tunazungumza kuhusu masuala mazima ya kuhamia Dodoma. Suala la kuhamia Dodoma kama lilivyoelezwa kwenye hotuba ni suala jema na lazima tuipongeze Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi kwa maamuzi haya ambayo yamefikiwa. Ingawa Serikali zilizopita zilijitahidi kufanya hivi lazima tupongeze hatua zilizofikiwa na Serikali ya Awamu ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nigusie kidogo kuhusu suala la wanawake na vijana. Mheshimiwa Mavunde amejitahidi sana kufanya kazi na vijana. Katika utaratibu ambao ameuanzisha wa kuhakikisha kwamba vijana Tanzania nzima wanawezeshwa, napenda sana utaratibu huu Mheshimiwa
Mavunde uendelee nao na mimi kama kijana nakuunga mkono kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunazungumza uwezeshwaji wa vijana na akinamama lakini tunapofanya uwezeshaji huu tuhakikishe kwamba ajira inakwenda sambamba na uwezeshwaji wa mambo haya yaliyozungumzwa katika hotuba. Tunavyozungumza kuhusu uwiano wa ajira na namna ambavyo Wizara husika inafanya kazi kuinua uchumi wa akinamama na vijana tuangalie Kanda ya Afrika Mashariki namna gani ambavyo wenzetu wamefanikiwa au wameshindwa.
Mheshimiwa Spika, katika uwiano wa ajira Tanzania tuko kwenye asilimia 10.3 lakini vijana wako kwenye uwiano wa asilimia 13 tuko vizuri ukilinganisha na nchi ya Kenya ambao wao uwiano wa ajira kwa upande wa vijana ni mkubwa zaidi hata mara tatu ya Tanzania. Kwa sababu hiyo niipongeze sana Serikali na Mawaziri husika kwa kazi ambazo wanaendelea kuzifanya. Namwalika Mheshimiwa Mavunde kuja pale Kalenga kuwahakikishia vijana wenzangu kwamba nao wananufaika na utaratibu huu ulioanzisha.
Mheshimiwa Spika, naomba nijikite sasa kwenye suala maji. Maji ni tatizo kubwa sana katika nchi yetu ya Tanzania na hususan katika Jimbo langu la Kalenga. Nina miradi mbalimbali ambayo bado haijakamilika ambayo nimezungumza sasa zaidi ya miaka miwili na kwa sababu ipo
kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu lazima niizungumze.
Mheshimiwa Spika, Jimbo la Kalenga lina wananchi wengi ambao wanaiona miradi yao lakini haijakamilika. Nina mradi wa maji ambao unatoka Isupilo, Magunga na Itengulinyi ambapo jumla ya shilingi bilioni mbili ziliwekwa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba mradi huu wa maji unatekelezeka na wananchi katika vijiji hivi wananufaika. Leo ni miaka miwili mkandarasi aliyekuwa pale site ameondoka ingawa amelipwa zaidi ya shilingi bilioni 1.2, hakuna malipo yoyote yanayofanyika na hivyo basi kufanya wananchi waweze kuleta mkanganyiko na kutokuwa na
makubaliano kati ya Mbunge, wananchi, viongozi na Serikali.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, napenda sana kuona kwamba Serikali inakuja na mkakati maalum wa kuhakikisha kwamba mkandarasi huyu analipwa ili maji yaweze kutoka katika vijiji hivi vitatu. Tutakapofanikiwa kupata maji katika vijiji hivi vitatu nina uhakika tunaweza kusaidia vijiji vingine kwa sababu mtandao utakuwa umeshasogea katika vijiji vya jirani. Sasa kupoteza shilingi bilioni 1.2 na kumuacha mkandarasi aende ni hasara kwa Taifa.
Mheshimiwa Spika, mkandarasi huyu ameishtaki Halmashauri ya Wilaya yangu, anadai riba ya zaidi ya shilingi milioni 250 kwa sababu ya mradi ambao haujakamilika. Nashangaa wakati mwingine kwa nini Serikali inaweza ikaruhusu vitu vya namna hii kutokea katika Majimbo yetu
na mwisho wa siku fedha zinapotea, wananchi wanaendelea kulalamika maji na vilevile hata baada ya kuongea sana bado maji yanakuwa hayatoki. Huo ni mradi wa kwanza.
Mheshimiwa Spika, mradi wa pili ni wa maji wa Nyamulenge ambao nilizungumza hata katika bajeti iliyopita nikasema mradi huu unaweza ukahudumia zaidi ya vijiji 18 katika Jimbo la Kalenga na hata vijiji vingine katika upande wa pili wa Mheshimiwa Mwamoto katika Jimbo la Kilolo. Mradi huu unahitaji shilingi milioni 49 na nilipeleka dokezo kwa Mheshimiwa Naibu Waziri akanieleza kwamba tatizo hili tutalitatua. Leo hii bado hatujaweza kupata majibu, wananchi wanaendelea kupiga makelele na tuliwaahidi katika kampeni zetu tutawaletea maji lakini mpaka leo hii hakuna dalili za maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nisisitize zaidi na zaidi kwamba tunavyozungumzia maji tunazungumza uhai wa wananchi wetu waliotupa kura zetu. Tutakuja kudaiwa baadaye kipindi tutakapokuja kuomba kura. Ni kumbukumbu ambazo napenda kuzitoa kwa sababu tulipita tukiwaomba kura kwa vigezo hivi. Leo hii unazungumza na mkandarasi anakwambia sijalipwa, unazungumza na Mhandisi wa Halmashauri anasema nimepeleka certificate kwenye Wizara. Ukiongea na Wizara wanasema hapana hatujapokea certificate, sasa sijui nani tumtafute hapa?
Mheshimiwa Spika, ni jambo ambalo linasikitisha sana, lakini napenda kuona kwamba maeneo mbalimbali siyo Jimbo la Kalenga tu, Wabunge wengi wamepiga kelele kuhusu maji, uwekwe mkakati maalum ambapo tutaweza kuona kwamba maji yanawafikia wananchi wetu kwa ukaribu na katika namna ambayo ni ya kipekee. Tumefanikiwa katika umeme kwa nini tushindwe kwenye maji? Naomba hayo yaweze kuwekwa kwenye kumbukumbu.
Mheshimiwa Spika, lakini vilevile Jimbo la Kalenga lina Hospitali ya Ipamba nimeomba gari la wagonjwa sasa miaka miwili na nusu. Jimbo la Kalenga ambalo ndilo linabeba hospitali ile ambayo inahudumia Majimbo mawili ya Wilaya nzima leo hii hakuna gari la wagonjwa. Narudia
tena, Wilaya ya Iringa Vijijini ina Hospitali ya Ipamba ambayo haina gari la wagonjwa yaani nimeongea mpaka sasa naona kichwa kinaniuma.
Mheshimiwa Spika, naomba Serikali iweze kuiangalia hospitali hii inayohudumia zaidi ya wananchi ya 300,000 wa Jimbo la Isimani na Jimbo la Kalenga na hata Iringa Mjini kama Manispaa lakini bado tunaendela kuomba. Kuna mambo ambayo tunatakiwa tuyaangalie tu kwa haraka
haraka tukaona hawa ni wananchi wetu, hawa ni akinamama wanaokwenda kuhudumiwa katika huduma hizi ambazo ni za msingi. Kwa hiyo, napenda sana Serikali iweze kuliangalia suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine niipongeze sana Serikali na Wizara kwa ujumla kwa namna ambavyo wameweza kuliangalia suala la UKIMWI. Nimesoma katika kitabu nimeona kwamba kuna shilingi milioni 347 ambazo tumechangia kama harambee, niipongeze sana Serikali kwa hilo lakini vilevile kuna shilingi bilioni 5.6 ambazo zimetengwa. Tatizo hili ni kubwa, tunaomba zile fedha ziweze kutengwa kwa watu hawa ambao kwa namna moja au nyingine wamenyanyasika kwa muda mrefu. Mheshimiwa Spika, katika kitabu hiki jambo moja ambalo limenisikitisha kuna neno moja limetumiwa linaitwa WAVIU, WAVIU ni watu gani hawa? Watu wenye virusi vya UKIMWI ni watu gani? Watu hawa tukiwatafutia maneno ya stereotype tukasema kuna hawa wenye UKIMWI, hawa wenye hivi tutashindwa kufikia majibu yetu. Haya ni maneno ambayo tunayaweka wenyewe na tunakuja kufika wakati ambapo tunashindwa… (Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Godfrey.
MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na nakushukuru sana.