Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Konde
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia leo kuwepo hapa katika hali ya uzima. Pili, nakushukuru wewe binafsi kwa kunipa nafasi hii kuweza kuchangia hotuba hii muhimu iliyopo mbele yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kuchangia naomba kwa heshima kubwa tu nimwombe Mheshimiwa Waziri Mkuu na nimwombe Mufti Bulembo kidogo ampe nafasi Mheshimiwa Waziri Mkuu ili atusikilize. Naomba tu Mufti Bulembo, tafadhali!
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nachukua nafasi hii kwa dhati ya nafsi yangu kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kumteua Profesa Kabudi kuwa Waziri wa Sheria na Katiba. Hii inatoka ndani ya moyo wangu. Sambamba na hilo, nampongeza kwa kumwondoa Mheshimiwa Mwakyembe katika nafasi hiyo na kumpeleka katika Wizara ile ya kucheza; atacheza, sasa tunamwona anapiga makofi uwanja wa Taifa. Huu ni ujumbe tosha kwamba akufukuzaye hakwambii toka, waona nyendoze zimebadilika; waweza ukae, huwezi ondoka. (Kicheko/ Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuipongeza sana Kamati ya Katiba na Sheria. Naipongeza kwa dhati sana kwa kuacha mapenzi ya vyama na kueleza lile lililo sahihi na la ukweli kwa mustakabali wa nchi yetu. Nawapongeza kwa dhati kwa kuona umuhimu wa kumwambia na kumweleza Msajili wa Vyama vya Siasa kama yeye wajibu wake ni kuvisajili na kuvilea vyama vya siasa na siyo kuvifarakanisha vyama vya siasa. Atekeleze wajibu wake na siyo kufanya mambo kwa mapenzi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba sana utusikilize. Mheshimiwa vyama hivi, mpaka chama kinaposimama kuna mambo mengi kinayopitia. Siyo jambo rahisi; vimeundwa vyama zaidi ya 20 ndani ya nchi hii, lakini hadi leo vyama vilivyosimama ni vyama visivyozidi vinne. Leo kwa sababu tu ya ulevi wa madaraka wa mtu mmoja, anatumia nafasi yake kufanya hujuma za waziwazi kwa ajili ya kukiteketeza Chama cha Wananchi - CUF, hilo jambo siyo sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunasikitika sana kwamba amani ya nchi yetu ni miongoni mwa sekta muhimu ambayo vyama vya siasa wanabidi kuvisimamia inavyopasa. Leo hii tunaona yanayofanyika, tunaona jitihada zinazofanywa hata kumbeba yule kibaraka anayetumiwa na wanaomjua; baada ya kufanikiwa kuingia Buguruni, leo wanaandaa njama za kuvamia katika Makao Makuu ya Chama Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, haya yanafanywa chini ya usimamizi wa watu wanaojulikana na kuna Waziri mmoja wa Zanzibar anaitwa Hamad Rashid ndiye plan master wa kuandaa mambo haya kwa kushirikiana na Makamu wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ally Iddi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunasema wazi haya ili dunia ijue na Watanzania waelewe. Haya yanayotokea kwetu siyo ya bure, ni mambo yamefanywa. Haiwezekani mtu anaacha chama mwenyewe zaidi ya mwaka mmoja anaenda kukaa huko, anarudi anajishauri. Hata kama ni mke, unakuta ameshaolewa na watoto ameshazaa na mume mwingine. Haiwezekani! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, haya yanayofanyika kwetu, leo hii nitashangaa nisikie Sofia Simba leo karudi kajitangaza tayari ni Mwenyekiti tena UWT. Hamtakubali! Kwa hiyo, kuchochea hayo katika vyama vyetu vya upinzani ni jambo la athari mbaya, jambo ambalo halitaipeleka Tanzania
katika neema ambayo tunatarajia kuipata kwa Mwenyezi Mungu.
Mheshimiwa Naibu Spika, neema ya Mwenyezi Mungu inakuja kwenye masikilizano. Msituchochee ndani ya Vyama vya Upinzani ili mkidhi haja zenu. Haiwezekani! Mlipoomba kura kwa Watanzania, mlisema Watanzania mtawaletea maendeleo, mtaleta elimu, maji; hamkusema kama
mtafitinisha vyama vya siasa ili mambo hayo muweze kuyapata. Haiwezekani! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukae tufikirie, tunapoandaa uwanja; tunapopanda nyasi tucheze vizuri, msitupandie michongoma ili tuumie miguu yetu. Haiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani ujumbe huo umeupokea, naomba tufanye kila linalowezekana lililo ndani ya uwezo wenu, Serikali isaidie kutatua migogoro hii na isiwe wao ndio sababu ya kuimarisha migogoro hii. Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, hivi karibuni katika vyombo mbalimbali vya habari ilitangazwa kwamba Watanzania tuko nafasi ya 153 kwa kukosa furaha duniani. Kwa kweli hili jambo lilinisikitisha, lakini halikunipa homa sana, lakini sasa baada ya kukosa furaha, inakuja Tanzania tunajengewa hofu ya lazima. Hili la furaha tungeliacha mbali,
lakini hofu ambayo Tanzania tunajengewa sasa ndiyo jambo ambalo linanitisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, matokeo haya yanayotokea ndani ya nchi sasa hivi katika tawala zote zilizopita hatukuzoea kuyaona. Wamepita Marais kadhaa na Mawaziri Wakuu kadhaa, hatukuona matukio yanayotokea ndani ya Tanzania yetu ya leo. Leo hivyo vikosi vinavyokwenda
vinachukua watu na kuwapeleka ambako hakujulikani na bado sisi Watanzania, sisi Wawakilishi wa wananchi wa Tanzania tuliomo humu, kama hatukusemea hili na Serikali ikawajibika katika hili, itakuwa hatutendi haki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kundi la swala, anaweza akanyakuliwa mmoja, wawili na swala wakaendelea na safari, lakini siyo kundi la binadamu, kundi la Watanzania. Iwezekane yafanyike hayo na bado sisi tuendelee kufanya mambo mengine; hili jambo ni la hatari. Leo Mheshimiwa Bashe amesema, kama kuna orodha ya Wabunge kumi ambao wako listed haijulikani ni nini kitakachowapata wakati wowote. Mimi nimeingiwa na homa, sijui kama na mimi nimo! Eeh, Mungu wangu, tulinde waja wako na hizi hujuma ambazo hatujui nani anayeziandaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kitu cha hatari! Mheshimiwa Bashe anasema amepata taarifa kutoka kwa baadhi ya Mawaziri wa Serikali; hili siyo jambo dogo. Nadhani leo sisi Wabunge tusingekuwa na lingine la kujadili zaidi ya kufikiria hili. Kama kuna list ya Waheshimiwa Wabunge, hao raia wadogo wao wakoje?
Mheshimiwa Waziri Mkuu, tunajadili bajeti ya maendeleo, maendeleo yapi yatakayopatikana wakati tayari tumejengewa hofu ya namna hiyo? Maendeleo yanaletwa pale watu wanapokuwa na amani, wanapojadili mambo kwa uwazi, wanaposema kwa uwazi; na mambo yale wakakaa wakapata muda wa kuyafikiri. Leo ikiwa Wabunge kumi hatujui, Mheshimiwa Selasini sijui yuko, sijui nani yupo, tunakaa sasa kila mmoja ana maswali ndani ya moyo; haijulikani ni nani yumo kwenye hiyo list, hebu Serikali tutoleeni hofu juu ya haya mambo. Tutoleeni hofu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo Wafanyabiashara hawana furaha, Wamachinga hawana furaha, Wanasiasa hawana furaha, bodaboda hawana furaha; sasa jamani ikiwa kila mtu hana furaha na kila mtu anaiishi kwa hofu, ni Tanzania ipi tunaipeleka na ni wapi tunaipeleka? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo anayeapa nambari moja Tanzania ni Mheshimiwa Rais, anaapishwa mbele ya Watanzania wote wanaona. Leo Mheshimiwa Rais baada ya kula kiapo kulinda na kuitetea Katiba, ni wa mwanzo anayetangaza vyama vya siasa ni marufuku kufanya mikutano ya kisiasa katika nchi hii. Hebu niambieni, ni nini kinachofanyika? Vyama vya siasa mnavipa ruzuku; sasa mnavipa ruzuku waende wakale na wake zao? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mnawapa ruzuku wajitangaze watoe elimu ya siasa, elimu ya uraia, wajipanue wapate wanachama ili siasa za ushindani zitendeke ndani ya nchi. Leo mnawaambia tunawapa ruzuku, lakini ni marufuku kufanya mikutano ya vyama vya siasa. Maana yake
nini? Sasa wataenda kuvizuia vyama vya siasa kupewa ruzuku, mnamchukua kibaraka Lipumba, mnamchotea mahela ya Serikali, anaenda kutumia anavyotaka yeye. Hiyo siyo sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana, haya mambo anayefikiria kwamba kufa kwa CUF ndiyo neema yenu Zanzibar, anajidanganya. Ziko roho zilizotangulia kwa ajili ya CUF na ziko tayari roho nyingine kuzifuata kama mtafikiria kukifuta Chama cha Wananchi – CUF. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsanteni sana.