Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nsimbo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Kwanza nimshukuru Mungu kwa kuweza kutufikisha siku hii ya leo. Binafsi naomba nimpongeze Waziri Mkuu na timu yake na Mawaziri wote kwa jinsi ambavyo wameshirikiana naye katika kuandaa bajeti hii. Naomba nimpongeze Mheshimiwa Jenista Mhagama na Naibu Waziri, Mheshimiwa Mavunde kwa kushiriki vyema kwenye bajeti hii pamoja na uwashaji wa mwenge Kitaifa kwenye Mkoa wetu wa Katavi. Wametupa ushirikiano wa hali ya juu, tumekwenda nao na wamefanya kazi kubwa kwa kweli tunawapa pongezi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kidogo nigusie kwenye hotuba ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Mheshimiwa Mbowe. Kuna mahali alizungumzia kwamba bajeti ya Serikali ni ya kisiasa, kwamba ina vyanzo hewa vya mapato. Naomba alichukue hili, yeye
hotuba yake ndiyo ya kisiasa kwa sababu kwenye hotuba yake ile amesema kwamba Serikali kwenye bajeti ya mwaka 2016/2017 iliweka chanzo cha kodi kwenye kiinua mgongo cha Wabunge wakati kodi hiyo itakwenda kutozwa mwaka 2020. Naomba nimwambie kwamba yeye ndiyo amefanya kisiasa, sio sahihi. Nakumbuka mwaka jana nilileta schedule of amendment kwenye eneo hili na Kanuni ilifuatwa, kulikuwa hakuna financial implication kwenye masuala ya kodi kwenye kiinua mgongo cha Wabunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, kwenye bajeti hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu ameweza kuzungumzia kwa kina kuhusu uwezeshaji wa wananchi kiuchumi. Naunga mkono, wameweza kutoa shilingi bilioni 1.5 kwa vijana kutoka kwenye ofisi yake na takribani shilingi bilioni 4.6 kwa upande wa mapato ya ndani kwenye Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tatizo ninaloliona ni Halmashauri nyingi kutotimiza ile kanuni inayoelekeza kutoa asilimia tano kwa vijana na asilimia tano kwa akina mama. Kwa hiyo, niombe sasa ili tuweze kufikia kuwawezesha wananchi wetu kufanya shughuli za kiuchumi, Serikali iweke msisitizo kwenye kuhimiza Wakurugenzi na kuwasimamia ili waweze kuhakikisha kwamba fedha hizi zinakwenda, maana Halmashauri nyingi maombi yapo lakini watu hawajapewa hizo fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia yale mafunzo ambayo yaliweza kutolewa chini ya Ofisi hii ya Waziri Mkuu kupitia VETA, Don Bosco, tunaomba yawe endelevu na hapa ndipo itakapokwenda kutusaidia katika kujenga ajira maana kuna watu wameweza kupata mafunzo haya na cheti. Naomba Serikali, Halmashauri zetu tuna mwongozo tunapeleka magari yetu kwa mfano TEMESA, lakini utaangalia gharama ile ambayo Halmashauri zinalipa kule TEMESA kwa baadhi ya huduma ni ghali sana. Kwa hiyo, tuombe sasa Serikali kwa mafunzo haya ambayo yanaendeshwa kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu tuweke ajira za mikataba kwa watu ambao wamepata mafunzo ya ufundi ili tuwe na mafundi wetu katika Halmashauri tupunguze gharama ambazo zinakuwa hazina tija kwa upande wetu, tukiwezesha vijana tayari tumejenga suala la ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni migogoro. Ofisi ya Waziri Mkuu hili liko chini yenu kuna CMA na Mabaraza ya Wafanyakazi lakini kuna matatizo ya watumishi wanakuwa wanahamishwa bila tija tu kwa malalamiko ya baadhi ya viongozi. Utakuta kiongozi eneo moja tu
analalamika kwa makosa ambayo mtu anaweza akasahihishwa basi anahamishwa, kwa hiyo, tunaongeza gharama kwa Halmashauri na ndiyo tunazidi kuweka madeni upande wetu wa Serikali kwa uhamisho ambao hauna tija. Tunakumbuka wakati Mheshimiwa Rais alivyoapishwa
alisema kwamba hatamhamisha mtu, mtu atakuwa anachukuliwa hatua za kinidhamu kwenye eneo ambalo yuko. Sasa tunaomba Ofisi ya Waziri Mkuu itoe mwongozo kwa Wakurugenzi wasifanye uhamisho ambao hauna maslahi ya kihalmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni la Bunge letu hili. Wabunge wamechangia, tumeona kwamba kuna ongezeko la bajeti karibu shilingi bilioni 21. Napenda kujua, kwa mwelekeo mpaka mwisho kuna upungufu wa shilingi bilioni 21 na gharama nyingine za msingi ambazo Serikali
iliweza kuziomba na kuziahirisha, je, hii bajeti ya sasa hivi ya shilingi bilioni 121 kweli inakidhi? Kwa hiyo, tuangalie zile gharama nyingine, kwa mfano, ile wiki ya kwanza kutokana na Kanuni tarehe 11 Machi hatukuweza kufika, je, ile gharama imekuwa-incorporated kwenye hiyo shilingi bilioni 21? Kwa hiyo, tunaomba kwa misingi ya Katiba kama Bunge tunaofanya hiyo kazi bajeti hii iweze kuangaliwa kwa undani zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuongelea kuhusu walemavu. Ofisi ya Waziri Mkuu ina wajibu huo na sheria ipo ya mwaka 2010, Sheria Na. 9 na kuna Mabaraza ya Walemavu katika ngazi ya Kitaifa, Mkoa mpaka kwenye Kata. Je, nani mwenye wajibu wa kuhakikisha kwamba Mabaraza ya Walemavu kwenye Kata na Wilaya yanafanya kazi na kanuni zake zipo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama inavyofanya kazi TASAF basi na walemavu wawe na mfuko wao tuweze kuwawezesha iwe ni sehemu ya ruzuku na isiwe mkopo ambao una riba na wapewe mafunzo kulingana na ulemavu mtu alionao ili aweze kufanya kazi yoyote ile. Siku moja redioni nilisikia mtu mwenye ulemavu wa macho anampima mtu na anashona nguo. Kwa hiyo, tunahitaji sana tuwaendeleze ili waweze kuondoka kutoka kwenye utegemezi. Kwa hiyo, tuombe sasa Ofisi ya Waziri Mkuu huu mfuko kama haupo basi muuanzishe na angalau hata kabla Bunge hili halijamalizika tuweze kuupata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la Mifuko ya Jamii. Mwaka 2012 tuliweka sheria ya kuzuia lile fao la kujitoa lakini sina uhakika, ila ni kwamba NSSF japokuwa hii sheria ilikuwa inazuia waliweza kuendelea kutoa fao la kujitoa. Nchi yetu tunahitaji hii mifuko ya hifadhi ya jamii iweze kusaidia katika kuleta viwanda na tumeona maelekezo kwenye randama humu kuna karibu mikoa 14 ambayo mifuko ya jamii inaelekezwa kwenye kuwekeza. Maoni yangu kwa sababu kuna mwingine anakuwa ameachishwa kazi na hana uhakika wa kupata kazi basi Serikali iangalie angalau katika lile fao la kujitoa ama akate asilimia 25 ya akiba mtu aliyonayo au theluthi moja yule mtu aweze kupewa ili katika kipindi cha mpito wakati anatafuta kazi ziweze kumsaidia katika kuendeleza maisha aliyonayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye upande wa kisekta tunajua tuna Wizara zinahusika na haya mambo ya kisekta, upande wa viwanda, lakini nizungumzie kuhusu barabara ambayo kwenye bajeti hii ipo, ya Mpanda - Tabora kwa kiwango cha lami. Tender zilitangazwa lakini mpaka sasa hatujafahamu ni watu gani wamekwishapewa hizo tender kutokana na marekebisho ya mkandarasi mshauri. Kwa hiyo, tuombe watu wa TANROADS watuharakishie. Sisi tukifanya ziara kule wananchi wanatuuliza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami Mpanda mpaka Tabora lini unaanza? Sasa kama fedha ipo tulishapata toka ADB kwa nini watendaji wetu wa TANROADS Makao Makuu wanachelewesha kurekebisha hiyo BOQ ili kazi ziweze kuwa awarded? Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye upande wa kilimo tumeona taarifa kwenye mpango, kilimo kimekuwa kimekua kwa asilimia 2.9 tofauti na malengo ya asilimia sita. Sasa tatizo ni nini na hapa ndiyo ajira kubwa ya wananchi wetu ilipo. Kwa mfano, Jimbo langu la Nsimbo asilimia 90 ya wananchi wangu ni wakulima wanalenga zaidi kwenye shughuli hii ya upande wa kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, upande wa maliasili, tuna Mbuga yetu ya Katavi, tunahitaji miundombinu iboreshwe na huduma ya Bombardier ya ATCL ianze ili watalii waje. Tuna viboko, Ziwa la Katavi, twiga mweupe ambaye atakuwa ndiyo kivutio zaidi kwa watalii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono bajeti hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Ahsante.