Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Anatropia Lwehikila Theonest

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nitaanza kwa kum-quote mwanasayansi mmoja anaitwa Albert Einstein aliwahi kusema; “Dunia ni mahali hatari pa kuishi siyo kwa sababu ya watu ambao ni wabaya, bali ni kwa sababu ya watu ambao hawafanyi lolote dhidi ya uovu.” Nitarudia, dunia ni mahali hatari pa kuishi siyo kwa
sababu ya watu waovu bali kwa sababu ya watu wema ambao hawawezi kukemea uovu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa nini nasema haya? Tangu asubuhi leo tunaongelea kupotea kwa mwananchi wa Tanzania anayeitwa Ben Saanane. Wanahesabika ni watu wangapi wanasema Ben Saanane kapotea na wanaoonekana kuongelea kupotea Ben Saanane wamekaa upande fulani, lakini Ben Saanane ni mwananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ana haki ya kuishi na ambaye kwa kupitia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaipa Serikali mamlaka ya kulinda uhai na usalama wa raia wake kwa mujibu wa Katiba hii. Tunapoongea kila siku hapa hatupewi jibu kutoka kwenye vyombo husika na kwa Waziri husika, huko ni kuonesha tunashindwa kutimiza wajibu wetu na ndiyo tunarudi kwenye kauli kwamba watu wema tunavyozidi kunyamaza kimya tunafanya dunia iwe siyo mahali salama pa kuishi, hilo ni jambo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitarudi kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nirudi kwenye majukumu yetu kama Wabunge hasa tukiwa kwenye Bunge la Bajeti hasa tukiwa na wajibu mkubwa wa kuisimamia Serikali. Siku za hivi karibuni nimeona mara nyingi mtu ukiongea
unaambiwa umemwongelea Rais badilisha hotuba au umemtaja Rais, nataka kujua ni lini Bunge kama Bunge inaruhusiwa kuisema au kuisimamia Serikali?
Mheshimiwa Naibu Spika, nitasoma kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Toleo la mwaka 1977 ibara ya 4(2) inaipa mamlaka Bunge na inasema; “...na vyombo vyenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma vitakuwa ni
Bunge na Baraza la Wawakilishi.”
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Bunge tunapewa mamlaka ya kuisimamia Serikali, kusimamia utendaji wa kazi zake za umma na tunafanya hivyo kwa niaba ya wananchi ambao ni umma. Tunapokuwa tunakuja hapa tunasema Serikali haijafanya moja, mbili, Rais katoa tamko moja, mbili na tunaambiwa tufute nini wajibu wetu kama Wabunge?
Mheshimiwa Naibu Spika, naenda mbali zaidi kifungu cha 63(2) nitasoma kinasema; “...kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Katiba hii.”
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge humu ndani kila mtu aliapa kuilinda Katiba hii, tunapofika hapa tunaambiwa tusiseme, tusiielekeze Serikali, tusiikosoe Serikali tuliapa nini hapa kama siyo unafiki? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Katiba hiyo hiyo tuliyoapa kuilinda na kuitekeleza inakuja Ibara ya 100 kama Bunge inaongelea Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge Ibara ya 100(1) na (2) “Kutakuwa na uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu katika Bunge…” Pia kifungu cha 46A kinaongelea ni namna gani Bunge kama muhimili linavyoweza kumshtaki na kumwajibisha Rais. Kama tunakuja hapa Bungeni tunaambiwa usimseme mtukufu ukimsema umevunja Katiba ni lini kama Bunge likiamua sijasema lifanye hivyo, lini kama Bunge likiona inafaa linaweza kumjadili na hata kumwondoa Rais madarakani kama tunaogopa hata kusema utendaji wa Rais. (Makofi)
Waheshimiwa Wabunge wenzangu tusikwepe madaraka yetu, hii nchi imeridhia utawala bora, kuna checks and balances. Kama Bunge tunawajibu wa ku-oversee Serikali inafanya nini, kama Bunge tunapaswa kuiambia Serikali ulivyofanya hivi ni sahihi au siyo sahihi. Iweje kila siku mnasema msitamke hilo neno huyo ni mtukufu, huyu ni nani, naona sasa tunavuka mipaka. Tunaendelea kupunguza uhuru wetu bila kujua kwamba kuendelea kujinyima uhuru hatuwatendei haki watu tunaowawakilisha. Tunasahau tunavyoendelea kujinyima uhuru tunashindwa kuhoji mambo kadha wa kadha ambayo yanatuhusu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu bajeti. Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye ni kiongozi na msimamizi wa Serikali Bungeni, tunaongelea Serikali unayoisimamia kwa mwaka unaoisha wa fedha 2016/2017 Serikali yako tukufu ikiwa imepanga bajeti ya shilingi trilioni 11 imeweza tu kukusanya trilioni tatu sawa na asilimia 26 kama mapato ya ndani, ikaweza kupata shilingi bilioni 871 ambazo ni fedha za wahisani. Kwa hiyo, jumla ya bajeti kwa fedha tuliyonayo ya
maendeleo tunaona tuna shilingi bilioni 33 ambayo ni asilimia 33 ya bajeti nzima mnayoileta tuiongelee.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini ninayasema haya? nasema haya kwa sababu ukisoma kwenye takwimu unaambiwa uchumi unapaa, uchumi haupai tu, uchumi ni matokeo ya fedha zilizopekewa kwenye Halmashauri. Uchumi kukua mabadiliko ya maisha ya watu ni matokeo ya fedha tulizoweza kukusanya, takwimu za TRA zinasema kwamba uchumi umeendelea kupaa na wamekusanya fedha nyingi. Wanaonesha mpaka Machi, 2017 wameweza kukusanya
shilingi trilioni 1.34; ukilinganisha na mwezi wa Machi 2016 ambako walikusanya shilingi trilioni 1.31 ikiwa ni ongezeko la asilimia 2.23. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani kwa mwaka huu tumekuwa na turn over ndogo ya fedha za maendeleo kuliko wakati mwingine wowote. Nataka nijue kama uchumi unakua kwa TRA mbona fedha ya maendeleo haiendi? Mimi ni mtu wa Dar es Salaama kwa takwimu za mwezi Oktoba 2016, kulikuwa na biashara 1,741 ambazo zimefungwa katika Jiji la Dar es Salaam ambayo inaonesha ni sawa na biashara 580 sawa na biashara 19 kwa siku zinafungwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hapo naona contradiction TRA mapato yanapanda na biashara
zinashuka, lakini bajeti ya maendeleo inazidi kushuka kabisa, hapo kuna kitu hakipo straight Waziri Mkuu, msimamizi wa kazi za Serikali Bungeni tunaomba utuambie mbona contradiction? Mapato yamepanda, biashara zinafungwa na fedha ya maendeleo haiongezeki ni lazima tuangalie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana nimewasomea Waheshimiwa Wabunge kwamba abunge tuna jukumu la kuisimamia Serikali, Serikali ituambie kama uchumi unakua mbona hatuoni fedha za maendeleo kwenye maeneo yetu? Mmechukua hata hela yetu ambayo ni kodi
ya majengo, mmeiongeza kwenye hiyo fedha ya maendeleo, kule kwetu kumedorora kule. Mimi nadhani ni heri zile fedha za kodi ya majengo tuziache kwenye Halmashauri ili kwenu yakibuma walau kwenye Halmashauri zetu mambo yanaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais aliwaomba wananchi kwamba wampe muda kitambo ana hakiki watumishi hewa, aliomba miezi miwili leo tunaingia mwaka wa pili, watu wamemaliza elimu zao, watu wamepata mikopo wamesoma huu ni mwaka wa pili hawajui wataajiriwa lini, tunataka kujua hawa watu wataajiriwa lini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho kabisa ambalo lipo kwenye Ofisi ya Spika ni kwamba tuliambiwa fedha zilibaki kwenye Mfuko wa Bunge takribani shilingi bilioni sita zikarudishwa Ikulu lakini hapa Wabunge wanalia wanasema hawana Ofisi, Ofisi hazina furniture, tumekuwa tunajibana lakini kumbe watu wanapeleka fedha Ikulu. Tuangalie kipi kipaumbele tunaweza kufanya kama taasisi ya Bunge ni kuwapendezesha waliopo Ikulu au ni kufanya kazi kama muhimili na kujenga ofisi kwenye maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaweza kuamua tunataka kufanya nini, tunataka kufanya kama Wabunge au tunataka kufanya kama vivuli vya Serikali Dodoma? Tuamue tunaweza kufanya vipaumbele tukaamua kwamba tunataka tuisimamie Serikali, tunataka kuishauri Serikali na tunataka kuihoji Serikali ni kwa nini fedha za maendeleo hazijaja, kwa nini fedha za wahisani haziletwi? Ni kwa sababu tumeamua sisi kama Wabunge na pengine Wabunge waliokuwa wengi wameamua kunyamaza kimya. Pengine Wabunge walio wengi wanaoamua kusema wanaonekana wanasema sana na hawapaswi kusema, tuangalie tunawatendea haki Watanzania au hatuwatendei haki? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaitendea haki mioyo yetu na ninarudi kwenye kauli ya Albert Einstein anasema; “Dunia ni mahali hatari pa kuishi si kwa sababu ya watu ambao ni wabaya, bali ni kwa sababu ya watu ambao hawafanyi lolote dhidi ya uovu.” Ujiulize upo kwenye upande upi wa shilingi, umeamua kunyamaza na kuacha mabaya yatamalaki au umeamua kukemea uovu ili mambo mema yatamalaki. Tukifuata kauli ya maneno hayo tutaweza kuwa Wawakilishi na Wabunge wema wenye kuisimamia Serikali na Serikali haiwezi kuleta tena asilimia 35 ya bajeti, itahakikisha itamiza hata asilimia 70 kwa sababu inajua wakija Bungeni bajeti haitapita, wakija Bungeni wataulizwa maswali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunachokiona hapa hata ikija asilimia tatu wanaoafiki tusemeje wanakuwa wengi inapita, lakini maendeleo hayaendi, Tanzania ya viwanda tunaweza kuisubiri na tukakesha inaweza isionekane kesho wala keshokutwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru.