Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

Hon. Lucia Ursula Michael Mlowe

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru sana kwa kunipa nafasi kuweza kuchangia Mpango huu wa Miaka Mitano.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nitoe masikitiko yangu, kwa sababu nimeupitia huu Mpango lakini wanawake tumesahaulika katika Mpango huu. Wanawake ndiyo jicho la Taifa, ndiyo wachapakazi, lakini sijaona msisitizo au kipaumbele kwa wanawake.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na wanawake wajasiliamali, niki-refer Mkoa wangu wa Njombe, akina mama wajasiriamali wanahangaika sana, wanajitahidi kufanya biashara zao, wanajitahidi kuanzisha shughuli ndogo ndogo kwenye familia zao, lakini hawapati support au mwongozo ambao unaweza kuwasaidia wakasimama. Maana mwanamke akiwezeshwa na akijengewa msingi anaweza kulibadilisha Taifa, hivyo ninaomba kwenye Mpango huu akinamama vilevile waingizwe kwenye kipaumbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni juu ya miundombinu. Wabunge wengi wamechangia juu ya tatizo la miundombinu, niki-refer Mkoa wangu wa Njombe, sasa hivi mvua zinavyoendelea kunyesha, barabara zinazounganisha Mkoa na Wilaya ya Njombe hazipitiki, na huo umekuwa wimbo wa Taifa, kila kipindi zinapoandaliwa Bajeti naona watu wa Njombe wanasahaulika, na hapa kwenye Mpango sijaona Mkoa wangu wa Njombe kama angalau umefikiriwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la elimu bure. Elimu bure ni sera ambayo imewafurahisha watu wengi sana hasa wazazi. Lakini kuna changamoto kubwa sana kwenye hiyo sera ya elimu bure, sijaona hapa mkakati wa maandalizi ya walimu ambao watasaidia hasa kwa watoto wadogo, kwa sababu kutokana na hii elimu bure, mwaka huu watoto wengi sana wameandikishwa. Lakini maandalizi ya Walimu hakuna, vyumba vya madarasa hakuna.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilifikiri hili lingefanyika baada ya kufanya utafiti, lakini hakuna utafiti uliofanyika, matokeo yake sasa hatutakuwa na msingi kwa hao watoto wadogo, watakwenda huko mashuleni watakaa chini, watacheza cheza watarudi nyumbani, mwisho wa siku watoto hakuna watakacho kipata, na hatimaye tunaharibu msingi wa watoto kutoka kule chini, kwa sababu kule chini ndiko kwenye msingi wa elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata tunapoongelea elimu ya juu lazima tuwe na msingi kule chini, kwa hivyo ninaomba mkakati uoneshwe hapa kwenye Mpango wa Miaka Mitano, kwa sababu ni miaka mitano, sasa miaka mitano maana yake hakuna kitakachofanyika kama hakijaoneshwa hapa, tunaomba Waziri wa Fedha ahakikishe anaingiza Mpango huu au mkakati huu, kwa ajili ya maandalizi ya walimu kwa ajili ya watoto wadogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kuhusu ada elekezi. Shule za private ndiyo zinazotupatia heshima katika nchi yetu, kwa sababu wanatafuta mbinu mbalimbali za kuhakikisha watoto wanafanya vizuri. Wanatumia mbinu mbalimbali kwa gharama kubwa, kutafuta walimu huku na huko hata kutoka nje, kuhakikisha wanaleta elimu kwa watoto wetu inayofaa na ndiyo maana shule za private ndizo zinazoongoza. Sasa tunapowaletea maelekezo juu ya ada kwamba watoe kulingana na maelekezo yetu tunawakosea haki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la afya ni tatizo kubwa kwa sababu miundombinu ya hospitali ni mibaya sana. Niki-refer Mkoani kwangu Njombe, mwezi wa pili Naibu Waziri wa Afya alitembelea Hospitali ya Kibena na akatoa maelekezo kwamba wahakikishe wanabadilisha au wanaleta mabadiliko na kurekebisha baada ya siku 90 wawe wamefanya kazi hiyo. Lakini ukienda sasa hivi pale Kibena ni majanga, hakuna hata paracetamol, hakuna x-ray, hakuna hata vipimo vile vingine kwa ajili ya maabara reagents hakuna, na miezi mitatu nafikiri tayari huu ni mwezi wa tatu sasa. Kwa hiyo niombe suala hili la afya liangaliwe kwa namna ya pekee, kwenye Mpango huu wa miaka mitano.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kilimo, Serikali imekuja na sera ya viwanda, lakini huwezi ukawa na viwanda kama hujaandaa mazao. Wakulima wetu wamekuwa wakipuuzwa sana. Niki-refer Mkoa wangu wa Njombe, mwaka huu wameunguliwa viazi vyao, sikuona jitihada iliyochukuliwa kuwasaidia wakulima hawa na ni kilio kikubwa sana kwa Mkoa wetu wa Njombe, sikuona Serikali inachukua jitihada ya pekee kuwasaidia wale wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakulima hawa wamekata tamaa, ningeomba tafadhali watu wa Njombe wafikiriwe, hasa wale wakulima wadogo wadogo, zaidi akina mama ndiyo hasa ambao wanateseka na kilimo, lakini mwaka huu wamepoteza pesa zao, na hawana tena mtaji wa kununua viazi kwa ajili ya mwakani. Niombe suala hili lichukuliwe kama inavyochukuliwa dharura sehemu nyingine au kwenye matukio mengine, mara nyingi yanapotokea mafuriko au nyumba zinaezuliwa, kuna pesa au kuna msaada wa dharula ambao huwa unatolewa kwa watu hawa, niombe hata Njombe wakulima wapate msaada kama huo kwa sababu hiyo kwao imekuwa janga.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mazingira hasa kwa Mkoa wangu wa Njombe kwa kweli yanatisha, hasa kwa upande wa takataka au karatasi plastic. Sijaona mkakati ambao unaonesha kwamba suala hili litaweza kushughulikiwa kwenye Mpango huu, imedokezwa kidogo sana, lakini mimi niombe suala hili liingizwe tena litiliwe mkazo, kwa sababu kweli takataka au makaratasi ya plastic pamoja na chupa za plastic ni majanga. Kila kona unakuta kuna chupa za plastic, siyo makaratasi tu lakini hata chupa za plastic za soda na juice zimetupwa kila kona. Hivyo ningeomba huku kwenye Mpango basi ioneshwe kwamba Serikali itachukua hatua gani kuweza kukomesha suala hili la plastic.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo tuna tatizo kubwa la utoaji taka, kwenye mashimo ya takataka. Nili-fight na Mkoa wangu wa Njombe, takataka zinajaa, zinafurika, ukiuliza Mkurugenzi anasema gari ni moja kwa hivi inashindikana kutoa takataka hizi, hivyo basi ningeomba suala la mazingira litiliwe mkazo. Vilevile juu ya utunzaji wa vyanzo vya maji, naomba vilevile lisisitizwe kwenye Mpango huu, kwa sababu ndio madhara hayo tunayoyaona sasa ambayo yanatuathiri, mabadiliko ya hali ya hewa, ni kutokana na mazingira yasiyo rafiki kwa binadamu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ushuru, wajasiriamali wengi wanakata tamaa kwa sababu ya ushuru na kodi mbalimbali au tozo mbalimbali, kwa mfano, wajasiriamali wa Njombe, hasa pale Njombe Mjini, kwa kweli wanatia huruma. Mtu ana nyanya anatembeza kwenye sinia ameweka kantini yake ndogo hapo, lakini anatozwa hela nyingi sana, naomba hili liangaliwe kwa hawa wajasiriamali wadogo, wasaidiwe na hii ningeomba ioneshwe kwenye Mpango, ni namna gani hawa wajasiriamali watasaidiwa.