Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Njalu Daudi Silanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Itilima

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu. Niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri wanayoifanya. Watanzania tunaamini na tunaotoka vijijini, Awamu ya Tano ni awamu ya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita katika sekta ya uwezeshaji, ukurasa wa 19. Niipongeze Ofisi ya Waziri Mkuu kwa jinsi walivyobainisha kuhakikisha viwanda vinafanikishwa katika nchi yetu hii. Kuna mashirika sita ambayo yameorodheshwa hapa na huu utakuwa muarobaini wenye kuleta ajira kwa vijana wetu nchini Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala zima la viwanda linahitaji malighafi. Nitaenda katika ukurasa wa 21, sekta ya kilimo. Sisi tunaotoka Simiyu na Mkoa wa Shinyanga na Kanda ya Ziwa kwa ujumla ni wakulima wa pamba, alizeti, mahindi na vitu vingine. Katika viwanda hivi ili viweze
kuendelea, naiomba Serikali iweze kutumia kila njia inayowezekana kuhakikisha pembejeo zinapatikana kwa wakati ili hivi viwanda viweze kufanya kazi vizuri kwa muda mrefu na vijana wetu waweze kupata ajira kwa muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na mwenzangu aliyemaliza kuzungumza kwamba Awamu ya Tano imefanya kazi kubwa sana. Ukienda kwenye Idara ya Maji, target ya mwaka 2015/2016 tulikuwa tumejiwekea malengo ya kukamilisha miradi 1,301 lakini hivi sasa tuna miradi 1,801 na bado miradi 509. Mungu atupe nini Chama cha Mapinduzi kwa mambo mazuri yanayofanyika haya? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao mradi wa kutoka Ziwa Viktoria ambao utahudumia vijiji takribani 253. Niiombe Serikali iendelee kuharakisha kwa maana ya Mji wa Gangabilili pamoja na Bariadi ambako unatoka Mheshimiwa Mtemi Chenge ili wananchi hao waweze kupata maji safi
na salama kwa sababu, mji wetu unakua kwa kasi na mahitaji ni makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yoyote utakayoyafanya mazuri lazima ukosolewe tu. Serikali ya Awamu ya Tano inafanya mambo makubwa sana, leo hapo Morogoro keshokutwa kuna reli inaenda kuzinduliwa ya kilometa 160 kwa saa moja. Ni maajabu ya nchi hii lakini bado watu tunalalamika. Mungu atupe nini ili tujue Serikali inapiga hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tujifunze Waheshimiwa Wabunge kuishauri Serikali kwa maana ya maendeleo na pale inapokosea tuiambie. Mimi ninakotoka Wilayani kwangu Itilima kuna bwawa lilikuwa limejengwa tangu mwaka 2002, hela zinakwenda na zinapotea. Leo hii Serikali ya Awamu ya Tano bwawa lile limejengwa kwa miezi minne, ni maajabu! Serikali ifanye nini na maji yanaendelea kupatikana katika maeneo haya! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nenda kwenye shule za sekondari na shule za msingi, ukifika maeneo ya kule utadhani umeingia Chuo Kikuu cha UDOM, wakati ni kijijini. Serikali ya Awamu ya Tano imeungwa mkono na Watanzania wote na tuendelee kutia moyo pale Mheshimiwa Rais anapotoa maelekezo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais anaungwa mkono na Watanzania. Kulikuwa na tatizo la madawati, amezungumza, wananchi wote wa Tanzania wameitikia na wametengeneza madawati ya kutosha na watoto wetu sasa migongo haiugui. Ni kwa sababu wanapata elimu iliyo safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la umeme. Sisi sote ni mashahidi tunakotoka umeme sasa hivi unamulika mpaka mafisi, hata uchawi utaanza kupungua. Ni kwa sababu ya maendeleo hayahaya katika maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana.