Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi nzuri na hasa ya ziara zake mikoani na busara anazozitumia katika utatuzi wa changomoto mbalimbali. Pia niwapongeze Mawaziri Mheshimiwa Jenista Mhagama na Naibu Waziri wake Mheshimiwa Antony Mavunde na watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nianze mchango kwa mambo yafuatayo; ucheleweshaji wa pesa za maendeleo katika miradi ya maendeleo. Kutokana na pesa za miradi kucheleweshwa katika Halmashauri zetu kunasababisha miradi mingi kutokamilika kwa wakati na pia kuongezeka kwa gharama za miradi variation.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Manispaa yetu ya Iringa iliyopo katika Jimbo la Iringa Mjini kuna mradi wa machinjio ya Ngerewala. Mradi huu mzuri lakini umeanza toka mwaka 2007. Mradi huu ukikamilika ungeweza kutoa ajira kwa wananchi wa Iringa zaidi ya 200.
Mheshimwa Spika, nashauri ni vema Serikali ingetoa pesa katika mradi huu kiasi cha shilingi bilioni moja ili Halmashauri isiingie kwenye mkataba mbovu wa miaka 25. Pia atafutwe mtaalam mshauri ili asaidie mradi huu uendeshwe kwa faida kwa sababu hiki ni chanzo kizuri sana
cha mapato. Mfadhili akipata atapandisha bei ya uchinjaji na kusababisha wachinjaji kuchinjia mtaani na inaweza pia kusababisha bei ya nyama kupanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mifuko ya Jamii, nipongeze jitihada zinaofanywa na mifuko ya jamii ya NSSF, LAPF, PPF, GEPF, PSPF na NHIF kwa kukubali wito wa kuanza kujenga viwanda ikiwemo ufufuaji wa kinu cha kusaga mahindi. Lakini niiombe Serikali iweze kulipa madeni inayodaiwa na mifuko hiyo ili viwanda vijengwe ambavyo vitasaidia kukuza uchumi na kuongeza ajira nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu fao la kujitoa, pamoja na nia nzuri ya Serikali ya kujali wafanyakazi pale wanapostaafu au wanapoacha kazi, lakini sheria ya kuzuia wafanyakazi kujitoa kwenye mifuko pale ajira zao zinapokomaa hadi mfanyakazi atimize miaka 60 hili ni tatizo kubwa sana kwa sababu ajira za wafanyakazi zimetofautiana. Mfano sekta ya ujenzi, sekta ya kilimo na sekta ya kazi za majumbani si rahisi wafanyakazi wa sekta hizo kufikisha miaka 60 tunashauri sheria hiyo itofautishe sekta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la watu wenye ulemavu, niipongeze Serikali kwa kuwatambua watu wenye ulemavu nchini lakini bado wanachangamoto hasa katika suala la usafiri, bado vyombo vya usafiri sio rafiki, ni lini Serikali italiangalia hili? Pia ni kwa nini katika ile mikopo ya Halmashauri na wao wasitambulike kutengewa asilimia zao katika asilimia tano ya vijana na akina mama? Walemavu wengi ni wajasiriamali lakini hawakopeshwi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wengi wamezungumza kuhusu kumtua ndoo kichwani mwanamke. Katika Mkoa wetu wa Iringa limekuwa ni tatizo kubwa sana hasa katika maeneo ya vijijini. Kinachosikitisha Serikali imekuwa ikitumia pesa nyingi sana kwa miradi ya maji lakini maji hayatoki
kama miradi ya Ilindi, Ng’uruhe, Ihimbo, Iparamwa Ruaha Mbuyuni na Mkosi. Lakini mkoa wetu una Mto Ruaha, Lukosi na Mtitu na chanzo cha Mto Mgombezi. Ni kwa nini mito hii isitumike katika kusambaza maji kuliko hiyo miradi ya visima iliyotengwa. Je, Serikali inawachukulia hatua gani hawa? Mheshimiwa Mwenyekiti, Naunga mkono hoja.