Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nyamagana
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kwa kuokoa muda nianze tu kwa kutoa pole kwa Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza, Mkurugenzi pamoja na Madiwani, lakini kwa wananchi wa Kata ya Mandu kwa kuondokewa na Diwani wao mpendwa Mheshimiwa Wambura, naamini Mungu ataendelea kuwatunza vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nashukuru na mimi kwa kupata fursa ya kuchangia Wizara hii ya TAMISEMI. Pamoja na mambo mengi iliyonayo, lakini ningejielekeza kwenye mambo machache. La kwaza, namshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii ya TAMISEMI kwa namna ya kipekee ambavyo wamekuwa
wakijishughulisha katika kuhakikisha wanatatua changamoto tulizonazo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo moja kubwa ambalo naanza nalo ni juu ya usafi wa mazingira. Nami nimeshangaa kidogo, kwenye kitabu cha taarifa, Mheshimiwa Waziri kama usipojitengenezea mazingira ya sisi kukusemea na mwenyewe huwezi kujisemea, Serikali hii kwa mwaka huu wa fedha tulionao kwenye Majiji manne na Manispaa tatu, imetumia fedha nyingi sana katika kuhakikisha inaboresha taratibu za upatikanaji na uzoaji wa taka na kuboresha miji na majiji.
Mheshimiwa Spika, nimeangalia taarifa hii imezungumza mistari michache sana, inataja tu kununua vifaa. Vifaa vilivyoko Mwanza peke yake ni vya zaidi ya thamani ya shilingi bilioni nne. Kuna truck zaidi ya 12, kuna excavator, duzor, compactor na kadha wa kadha na sasa tunajenga dampo la kisasa kuhakikisha usafi wa Mji. Haya yote nilitegemea niyaone na haya yamefanyika Arusha, Tanga, Mbeya, Dodoma, Mtwara pamoja na Kigoma. Sasa usipojisifia wewe Mheshimiwa Waziri, sisi tutakusifia mpaka lini?
Mheshimiwa Spika, naomba nijielekeze kwenye suala la wafanyabiashara ambayo inaitwa sekta isiyo rasmi ya wafanyabiashara ndogo ndogo Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika, wafanyabiashara ndogo ndogo kwa sasa ingewezekana wakatambuliwa kama Sekta Rasmi, kwa
sababu wako zaidi ya 30,000 nchini kote. Mara kadhaa tumekuwa tunawachukulia kama watu ambao hatuoni umuhimu na thamani yao na ndiyo maana mara kadhaa wamekuwa wakifukuzwa na mgambo, wamekuwa wakipigwa mabomu, lakini mwisho wa siku wanaharibiwa
mali zao, kunyang’anywa na kuteketezwa. Siyo wao tu, hapa namwongelea Mmachinga wa kawaida, mama lishe, baba lishe na kadhaa wa kadhaa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa sote tunafahamu kwa sasa suala zima la Halmashauri zetu katika kukusanya kodi, limekwenda chini sana na mfano mzuri, ukichukua tu takwimu za Mkoa wa Mwanza na Halmashauri zake zote kwa ujumla, mwaka 2016/2017 tulitazamia kukusanya shilingi
bilioni 34, mpaka leo tunazungumza, taarifa inasema tumekusanya shilingi bilioni 16. Tunakusudia bajeti ya mwaka 2017/2018 tukusanye shilingi bilioni 35, ongezeko la milioni 600 peke yake.
Mheshimiwa Spika, nataka kusema nini? Machinga hawa wa leo ambao tunawaona sio watu muhimu kwenye shughuli zetu, tunaweza tukawafanya wakawa sehemu kubwa sana ya kipato kwenye Halmashauri ambazo Machinga hawa wamekaa mjini sana.
Mheshimiwa Spika, ukichukulia Mwanza peke yake, nimeangalia Dar es Salaam, Mbeya, Arusha na maeneo mengine ikiwemo na Dodoma. Kwa Mwanza peke yake, chukulia tunao Machinga 5,000. Machinga biashara yao inajulikana ni kwa siku, tu-assume Machinga mmoja kwa siku popote alipopanga alipie shilingi 1,000 peke yake ya kile kieneo kidogo ambacho amekitenga.
Mheshimiwa Spika, kwa Machinga 5,000 tutakusanya shilingi milioni tano, mara 26 kwa mwezi ukiondoa Jumapili, unatengeneza zaidi ya shilingi milioni 130; kwa mwaka mzima Halmashauri ya Jiji la Mwanza inaweza kuingiza zaidi ya shilingi 1,200,000,000. Fedha hizi hatutakaa tutegemee fedha za Serikali kuwasaidia wafanyabiashara ndogo ndogo, lakini kuwasaidia kuweka miundombinu ambayo kesho tutawapeleka wakakae katika miundombinu iliyo bora na sahihi (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini kupitia mfumo huu, tukikubali haya maeneo tuliyowapa sasa kwa muda wakakaa kwa miaka mitatu mpaka miaka mitano; tunaweza kutumia fedha zao wenyewe kujenga miundombinu rafiki na wao wakawa tayari kwenda kufanya biashara kwenye maeneo yale. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba hili linasambaa maeneo yote ya nchi ambayo mara nyingi ni maeneo ya Miji. Tunaweza kufanya hivi na tukawasaidia wafanyabiashara hawa. Kwanza watakuwa na uhakika na maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya kufanyia biashara. Wakiwa na uhakika, wamekuwa na uhakika na shughuli yao na kesho yao kwa sababu tunataka tuwasaidie.
Hili linajidhihirisha! Ukiangalia fedha za vijana na wanawake, kati ya shilingi 56,800,000,000; tumepeleka shilingi bilioni 27.5 peke yake, sawa na asilimia zisizozidi 27.
Mheshimiwa Spika, sasa kwa kufanya hivi pia tutakuwa tumemsaidia sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mavunde pale anayehangaika na kutatua kero za vijana kila siku. Kwa sababu siyo kweli kwamba ipo siku Halmashauri zitafikia asilimia mia kupeleka fedha za wanawake na vijana
kwa sababu mahitaji ni mengi kuliko kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimeongea sana hapa kwa sababu ni changamoto kubwa sana na sisi tunawaogopa kwa sababu hawa ndiyo watu ambao tunaamini wakitengenezwa vizuri, kwa haya tunayoyasema, Dar es Salaam kule Ilala peke yake, pale Kariakoo wanasema wana
Machinga zaidi ya 5,000. Ukiwafanyia utaratibu huu tunaouzungumza na wao watapata kipato, lakini na Manispaa nyingine pia pamoja na Majiji wanaweza kuwa na hatua kubwa sana ambayo itawapelekea kupiga hatua kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nigusie kidogo juu ya suala la ufya. Uboreshaji wa sekta ya afya, kwenye ripoti inaeleza wazi kwamba imejikita na inaelekeza katika kujenga vituo vya afya zaidi ya 244 lakini kujenga hospitali zetu za rufaa. Sasa ni lazima tukubali, tunapojenga Hospitali za Rufaa ni lazima pia tuwe tayari kuimarisha.
Mheshimiwa Spika, mwaka uliopita tulisema tutajenga zahanati na kituo cha afya kwenye kila Kata. Sasa mpaka leo tunatazamia kujenga Vituo vya Afya 244. Tunavijenga kwenye Kata zipi? Waziri atakapokuja tunaomba pia tujue ni Majiji gani na Halmashauri zipi, Kata zipi zitakazofaidika na hospitali hizi 244. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia Hospitali za Wilaya; tunazo Hospitali za Rufaa za Kanda na Mikoa. Leo kama hatuna Hospitali za Wilaya kwenye Wilaya zetu, ni vigumu sana kutoa huduma zilizo bora kule kwenye hospitali zetu za rufaa.
Mheshimiwa Spika, ukienda pale Wilaya ya Ilemela, ni Wilaya mpya, haina Hospitali ya Wilaya, wanategemea Hospitali ya Jeshi. Tunafahamu Jeshi namna na wao walivyo na shughuli zao nyingi, tuna wajibu wa kuhakikisha Wilaya ya Ilemela inapata Hospitali ya Wilaya ambayo kimsingi imeshaanza kujengwa kwenye eneo la Busweru. Siyo hivyo tu, wamejikakamua kwa namna wanavyoweza, wameanza na jengo la wagonjwa kutoka nje, lakini uwezo wa kukamilisha kwa gharama ya shilingi bilioni tatu haiwezekani.
Mheshimiwa Spika, tunaomba fedha hizi zinazokwenda kujenga Hospitali za Rufaa, tuelekeze pia kwenye Hospitali za Wilaya ili tupunguze mzigo hata kwenye hizi hospitali za rufaa tunazozijenga kuanzia huku wilayani.
Mheshimiwa Spika, kwa kufanya hivyo, leo kwenye Jimbo la Nyamagana kupitia Mfuko wa Jimbo na wadau mbalimbali tunayo maboma manne kwa ajili ya vituo vya afya; Kata ya Buhongwa, Kata ya Lwang’ima, Kata ya Kishiri na Kata ya Igoma, tunataka kukamilisha, tunayamaliza vipi?
Uwezo wa Halmashauri zetu kukusanya mapato kwa nguvu unaelekea kuwa siyo mzuri sana. Ni lazima tuhakikishe tunajikita kwenye kuboresha hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunazungumza sasa hivi, tunaelekea kwenye kukusanya kodi kwa wafanyabiashara ndogo ndogo waanze kulipa service levy, wenye leseni za kuanzia shilingi 40,000. Mfanyabiashara mwenye saluni yenye kiti kimoja au viti viwili anayelipa leseni ya shilingi
40,000; baada ya miezi mitatu anatakiwa alipe service levy.Ni wafanyabiashara wa namna gani tunaowakusudia?
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nashauri…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba niunge hoja mkono na ninashauri hayo yafanyiwe kazi. Ahsante.