Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nishukuru kwa kupata nafasi hii. Mchango wangu unaanza na sifa. Kwa sisi tunaoabudu na tunaosali kwa Kikristo ukitaka kuomba lazima kwanza uanze na nyimbo za sifa ili Mungu au Bwana wetu Yesu Kristo afahamu kwa kweli unamsifu ili akupe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwanza naanza pia kwa kumpongeza Rais wetu kwa kazi anayoifanya katika Serikali hii ya Awamu ya Tano. Pia nawapongeza Mawaziri wote lakini kubwa nimpongeze Naibu Waziri wa TAMISEMI kwa sababu kwanza amefika kwenye Wilaya yangu na kutatua kero za wafanyakazi zilizoko ndani ya Halmashauri ya Mbulu Vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto ambazo zipo katika maeneo mengi hasa TAMISEMI ninao mchango mdogo ambao napenda kuuzungumzia leo. Serikali za Mitaa ilipaswa kukusanya mapato takribani shilingi milioni 332 lakini kwa bahati mbaya imekusanya shilingi milioni 232, ni sawa na asilimia 70. Ushauri wangu wa kweli katika kukusanya mapato ni vema sasa Wizara ikaelekeza msukumo
kwa Maafisa Maduuli ili kutumia mashine za EFD kukusanya mapato ambayo itasaidia Halmashauri zetu kuongeza mapato yanayoonekana kabisa. Kwa sababu research inaonyesha Halmashauri chache hazitumii mashine kukusanya mapato ya ndani. Kwa hiyo, niombe Wizara hii
iweze kupeleka moja kwa moja nguvu zake na kuwashauri Maafisa Maduuli kusaidia ukusanyaji wa mapato ili
Halmashauri zetu ziweze kujiendesha vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine tunazo ahadi ambazo zimewekwa katika maeneo yetu ya Miji Midogo. Kwa mfano Mbulu Vijijini tuna ahadi ya Mheshimiwa Rais na naamini sasa kutokana na Road Fund mnaweza kutusaidia ahadi ya kilometa tano ya lami iliyowekwa katika Mji Mdogo wa Hyadom. Nafikiri Mheshimiwa Jafo umefika na umepata maswali ya ndugu zetu wananchi wa pale ambao wametaka ile ahadi walau itekelezwe ili mji ule upate sifa hata ya kuwa na lami na kilometa mbili za Ndongobesh. Pia nafikiri umeonana na wananchi wa Dongobesh waliokulilia hasa ule mradi wa maji umaliziwe tu, imebaki hela kidogo shilingi milioni 600. Baada ya kushukuru kwa kutupa shilingi bilioni 1.8 malizieni basi ule mtaro ili maji yawezekwenda na wananchi wafaidike katika eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema nimesifu mapema ili ujue kwa kweli nahitaji kuomba. Kwa kweli maji ndiyo msingi hasa wa maendeleo ya wananchi wetu hasa kwenye kilimo. Katika haya basi mtusaidie kwa sababu Serikali imeshawekeza hela ya kutosha bado tu eneo dogo la kuweka mtaro wa maji kwenda kwa watumiaji ili kilimo kianze.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao viongozi wetu wengine wanaotusaidia kwenye kazi kwa mfano Wenyeviti wa Vitongoji, Wenyeviti wa Vijiji na Madiwani. Madiwani wako wenzangu wamezungumzia sana kwamba posho yao ni ndogo na wanasimamia miradi mikubwa ambapo kimsingi
wanafanya kazi nzuri sana. Niombe leo TAMISEMI waangalie namna nzuri ya kuwasaidia Madiwani hawa kwa kuwapandishia posho yao kidogo ili angalau wafanye kazi inayotakiwa kikamilifu kwa kusimamia Serikali za Mitaa hasa kwenye Halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia vijiji vyetu, Wenyeviti wa Vijiji wanafanya kazi nzuri sana lakini bahati mbaya sana hawana hata posho. Kama inashindikana kuwalipa kwa muda wote wapatieni basi bakshishi kwa muda fulani wafurahi na waone Serikali yao inawajali. Hata ndugu zetu Wenyeviti wa Mitaa na Vitongoji naomba muone namna ya kuwasaidia katika mapato yetu ya ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo tatizo hasa katika Wizara ya Utumishi. Namuomba sana dada yangu anisaidie hasa tatizo la upungufu wa watumishi. Halmashauri yangu inakabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi lakini pia tuna Wakuu wa Idara ambao wanakaimu kwa muda mrefu sana. Zaidi ya 80% ya Wakuu wa Idara wa Mbulu Vijijini kwenye Halmshauri yangu wanakaimu. Niombe basi wapandishwe washikilie hayo madaraka nao waone kwamba Serikali yao inawajali maana wamekaa kwa muda mrefu hawajui waende mbele au warudi nyuma. Mheshimiwa Waziri naamini wewe ni makini na unasikiliza haya, angalia Mbulu Vijijini kwa namna ya pekee sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara pia iangalie, tumeshafanya mabadiliko ya Sheria ya Manunuzi lakini kuna sintofahamu ya kutumia force account kwenye Halmashauri. Naomba basi Wizara isaidie na ije na kanuni ya kutumia ile force account ili watumishi waelewe namna ya
kuitumia na kupunguza gharama ya miradi katika maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nishukuru katika ajira mmetusaidia kwa kutupatia walimu wachache wa sayansi.
Sisi tuna upungufu mkubwa sana wa walimu katika maeneo yetu. Niombe basi wakati ujao ajira za walimu hasa wa sayansi ziongezeke, lakini pia tunaomba ajira ziongezeke kwa Watendaji wa Vijiji na Watendaji wa Kata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi umetoka maelekezo na waraka kuwaelekeza Wakurugenzi wawaondoe walimu katika kukaimu nafasi za kata na vijiji. Wananchi wetu sasa wameamua kuwaweka watu ambao wanawalipa wenyewe ili wasaidie kuzikaimu nafasi hizi za Watendaji wa Kata na Vijiji. Naomba Wizara iangalie namna gani ya kuajiri Watendaji hawa wa Kata na Vijiji. Wako watu wamemaliza shule na wana weledi wa kufanya kazi hizi hasa katika maendeleo ya jamii. Ni vigumu sasa kusaidia wananchi kwa sababu wale wanaoshika nafasi hizi hawana ule weledi wa kutoka. Kwa sababu Serikali za Vijiji ndiyo zinawalipa kwa hiyo wanaajiri mtu yeyote tu wanaoona anafaa na anakaa pale ofisi walau kufungua na kufunga kwa hiyo hawezi kuwasaidia wananchi katika kuibua miradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wako Maafisa Maendeleo ya Jamii wengi sana wamemaliza vyuo wako vijijini, Wizara iangalie tu namna ya kuwaajiri. Maana Serikali huku juu mnafanya kazi nzuri hapa katikati kwa Wakuu wa Mikoa vizuri, kwa Wakuu wa Wilaya vizuri, kwa Wakurugenzi vizuri, Wakuu wa Idara vizuri, kule vijijini wanakaimu watu wa kaiwada tu, tusaidieni basi tuleteeni wataalam ambao wataweza kufanya kaz kwa kuajiriwa na kuibua miradi, maana sasa hivi miradi inatoka juu inakuja chini. Kwa mimi niliyesoma Maendeleo ya Jamii wanasema top-down inatakiwa iwe bottom-up yaani miradi itoke chini kwa wananchi ili walau wao wenyewe waweze kujipangia miradi yao na waone miradi hii ni ya kwao na waiendeleze na wananchi wanaweza kufanya kazi hii kwa uhakika zaidi. Kwa hiyo, nilitaka niyaseme haya ili walau Serikali isaidie katika hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa naomba nizungumzie habari ya mikopo ya vijana na wanawake. Katika Halmashauri zetu zile asilimia tano, tano kufikia asilimia kumi ni vigumu kutekelezeka kwa sababu hii. Fedha zinazoenda kwenye Halmashauri kama OC haziendi kwa
wakati au haziendi kabisa. Kwa hiyo, Mkurugenzi anaona kuliko undeshaji wa Halmashauri ukwame anatumia zile fedha za mikopo ya vijana ambayo anatakiwa itoke kwa mujibu wa kanuni. Hawezi kutoa kwa sababu hana fedha za kutumia, kwa hiyo basi anakwenda kutumia zile fedha za mikopo ya vijana. Naomba Serikali ijitahidi kupeleka fedha walau fedha hizo ziweze kwenda...
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naunga mkono hoja.