Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Maswa Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii kwa siku ya leo. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya bora kabisa. Awali ya yote kwanza kabisa Mheshimiwa Mwenyekiti naomba nitoe pongezi nyingi sana kwa wananchi wa Uyui kwa ushindi mkubwa walioupata. Kama tulivyosikia katika Uchaguzi Mdogo wa Vijiji CCM imepata viti 14 sawa na asilimia 93.3 hongera sana. Katika Vitongoji viti 58 CCM imechukua 51 sawa na asilimia 88 hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kutoa pongezi kubwa kwa Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kutoka katika Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kazi nzuri wanayofanya na kwa hotuba nzuri kabisa ambayo imejaa ukweli na uwazi. Katika Hotuba ya Mheshimiwa Waziri aliyozungumzia zaidi masuala ya mazingira ameeleza kwa uwazi kabisa kwamba hali ya mazingira nchini kwetu siyo nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mazingira ni suala mtambuka, tunatambua wazi kwamba nchi yetu sasa inakwenda kuwa ni nchi ya viwanda kwa hiyo tunapokuwa na mazingira ambayo siyo ya kuvutia inatupa hali ngumu sana kuona kama kweli nchi yetu inakwenda kwenye viwanda. Tunahitaji juhudi za ziada kuhakikisha kwamba tunatunza mazingira yetu ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukitizama juhudi za Serikali kwa namna moja au nyingine tumejitahidi, lakini tunahitaji juhudi zingine nyingi za ziada kuhakikisha kwamba mazingira yetu yanakuwa siyo tishio tena kwa viumbe wanaoishi juu ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa mabadiliko ya tabianchi yameleta mabadiliko makubwa sana, ukitizama hata kimo cha bahari kinaongezeka. Kimeongezeka kwa sentimeta 12, maana yake ni kwamba zile kingo ambazo ziko kwenye upande wa baharini na zenyewe ziko katika mazingira hatari ya kuweza kufunikwa na maji na baadhi ya maeneo mengine kuna visiwa vimeanza kufunikwa. Hii ni hali mbaya kwa sababu bila kuchukua tahadhari ya kutosha tutajikuta tuko katika mazingira magumu sana miaka ijayo. Kwa hiyo, ndugu zangu tunahitaji tuungane na mikakati ya Kimataifa pamoja na ile mikataba ambayo Tanzania imesaini ya Kimataifa kuhakikisha kwamba tunashiriki katika kudhibiti uharibifu wa mazingira unaotokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ningependa kuongelea suala la Mfuko wa Mazingira. Tunatoa pongezi kubwa sana kwenye Serikali ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Februari, 2017 umeanzishwa huu Mfuko wa Mazingira ambao Mheshimiwa Ndugu Ali Mufuruki amechaguliwa kuwa Mwenyekiti. Huu Mfuko wa Mazingira ni muhimu sana tuufanyie kazi. Mfuko huu wa Mazingira tuuwezeshe, tuhakikishe kwamba tunaupa nguvu ya kuweza kufanya kazi ya kutekeleza au kusimamia ile Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004. Tunaomba Serikali izingatie kuusaidia na kuhakikisha kwamba huu Mfuko unafanya kazi ipasavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitizama suala la mazingira kama tunavyosema ni suala mtambuka, lakini ukitizama Wizara hii haipewi fedha za kutosha, haipewi facilities za kutosha kuhakikisha inafanya kazi inavyostahili. Ukitazama katika tozo kuna tozo mbalimbali zinazohusiana na mazingira, ukiangalia tozo kwenye magari chakavu, ukiangalia tozo kwenye mkaa, ukiangalia tozo kwenye mafuta, tozo kwenye majengo, kwenye migodi, kuna magogo yanatozwa kodi ya mazingira, lakini Mfuko huu haupewi chochote maana yake nini?(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba hata katika Kamati ya Mazingira imeeleza angalau asilimia tano ya hizi tozo iende kwenye Mfuko wa Mazingira ili kusudi Mfuko huu uweze kupatiwa nguvu ya kuweza kufanya kazi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitazama hapa katika Mfuko huu wa Mazingira na juhudi kamili ambazo zinaendelea katika Wizara hii, utaona kuna mwingiliano wa hali ya juu katika Wizara zingine. Wizara ya Mazingira ina- insist watu waweze kutunza mazingira, waweze kupanda miti na kuacha ile misitu ya asili iendelee kukua, lakini kuna Wizara zingine kwa mfano, Wizara ya Maliasili kupanda miti siyo priority kwao, wao kuvuna miti ndiyo kipato kwao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, iangaliwe namna ya kuweza ku-harmonize hizi sheria ili kusudi hawa wote wawe na majukumu sawa ya kuweza kutunza mazingira. Ukitazama Wizara ya Maliasili wao misitu wanaitumia kwa ajili ya kutunzia wanyama lakini masuala ya kupanda na kuhakikisha kwamba misitu inalindwa hiyo inakuwa ni kazi ya Wizara ya Mazingira chini ya Mheshimiwa Makamu wa Rais. Sasa hapa hizi Wizara zote mbili au tatu zihakikishe kwamba wana- harmonize hizi sheria kuhakikisha kwamba Wizara ya Mazingira inakuwa na nguvu kuhakikisha kwamba inasimamia Sheria ya Mazingira na Sheria hizi zinahakikisha kwamba zinatunza mazingira kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ningependa kuongelea kuhusu bajeti ya mazingira, bajeti ya mazingira leo imeombwa hapa, lakini inasikitisha sana ukiangalia bajeti ya mwaka 2016/2017, walikuwa wametengewa shilingi billioni 20 lakini ile bajeti ceiling kwa mwaka huu imepungua. Tunaomba Serikali iangalie uwezekano wae kuitengea bajeti ya kutosha Wizara hii. Hii Wizara ni nyeti lakini inaonekana kama vile haipewi priority kama Wizara zingine, wanapewa pesa kidogo na kweli uharibifu wa mazingira ni mkubwa kiasi kwamba hapo baadae watashindwa kufanya kazi na mazingira yetu yatazidi kuwa mabovu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba kutoka billioni 20 ya mwaka 2016/2017, angalau wangerudia kupewa kiasi kile kile, sasa bajeti imepigwa panga imekatwa kutoka billioni 20 inakwenda kwenye billioni 15. Matokeo yake ni nini? Hawa wanafanya kazi kwa kutegemea Mfuko wa NEMC na NEMC ndiyo inayowalisha Wizara ya Mazingira na NEMC inalalamikiwa kwa kutoza watu tozo na penalty nyingi ambazo kwa kweli zinafanya watu wasijisikie vizuri na NEMC inavyofanya kazi. Kwa hiyo, naomba mambo haya yote yazingatiwe vya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Wizara yake kwa kutuwezesha Mkoa wa Simiyu kupata pesa za mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kiasi cha dola za Kimarekani millioni 100 sawa na billioni 230. Kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Simiyu, kwa niaba ya wana-Maswa na Wilaya zingine zote za Mkoa wa Simiyu, tuna uhakika sasa tutapata maji kutoka Ziwa Victoria na tutahakikisha kwamba tutapata maji ambayo yatatusaidia kutunza mazingira ya Mkoa wetu wa Simiyu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyotambua Mkoa wetu wa Simiyu ni Mkoa kati ya mikoa nane ambayo iko katika tishio ya kuwa jangwa hatuna vyanzo vya maji , hatuna vyanzo ambavyo ni vya uhakika kuweza kupata maji, kuweza kumwagilia na kufanya shughuli za kiuchumi kwa maana ya kilimo na shughuli zingine za kufuga na mambo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupata mradi huu tunashukuru sana kwamba sasa Mkoa wa Simiyu utaamka na utakuwa ni mkoa ambao utalima mazao mengi kwa kupitia mradi huu kwa maana ya kumwagilia, tutalima mpunga mwingi wa kutosha na tutatunza mazingira ya kutosha na mkoa wetu utakuwa ni green, tunasema ni mkoa ambao ni wa kijani. Tunawashukuru sana na tunaomba wana Simiyu wajiandae kwa miradi hii mikubwa inayokuja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni matumizi ya plastiki, tumeona jinsi juhudi za Serikali ilivyofanya tunawapongeza Serikali kwa kuweza ku-burn viroba, viroba ilikuwa ni moja ya vitu vinavyochafua mazingira. Ninachotaka kusema ni kwamba katika vile viroba vya pombe, uchafuzi wa mazingira wa viroba vya pombe ulikuwa ni kama niasilimia 0.001 something kule. Sasa kuna mifuko ya plastiki na yenyewe tulishatoa tamko katika Kamati yetu kwamba watengenezaji wa vifungashio vya plastiki watoke katika teknolojia ya sasa hivi ya mifuko ambayo haiozi waende kwenye teknolojia ambayo ni bio-degradable ambayo mifuko ukiisha i-produce baada ya miezi mitatu ukiitupa kwenye udongo mifuko ile inaoza. Tunaomba waende kwenye hiyo teknolojia, dunia yetu itakuwa salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, at the same time Serikali itoe elimu ya kutosha jinsi ya utupaji wa plastiki, watu wafahamu namna ya kutunza mazingira na mwisho Kamati iliishauri Serikali kwamba Serikali i-insist sasa kuwawezesha Wajasiliamali waweze kuanzisha viwanda vya bidhaa…...(Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.