Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Julius Kalanga Laizer

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Monduli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa
Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nishukuru kwa kunipa nafasi hii. Pia nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametupa uhai na tumefika leo hapa kujadili masuala haya ya mustakabali wa nchi yetu katika Muungano na Mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ufunguzi wa neno langu kubwa ambalo napenda nilitumie ambao ni msemo wa wahenga unasema anayekufukuza akishaona hakupati basi nyuma huku hukurushia matusi. Kwa hiyo, namwomba Waziri wangu wa mambo ya Muungano, mambo ambayo yameandikwa yakawa presented hapa, haya mengine wewe yachukulie tu. Hawa wako mbali sana, kwa hiyo lazima watarusha maneno. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza utekelezaji wa mambo ya Muungano ambayo Mheshimiwa Waziri ameyataja kwenye kitabu chake kuanzia ukurasa wa 42 mpaka ukurasa wa 52 ambayo pamoja na mengine siyo ya kimuungano lakini ni ya ushirikiano ambayo ni sekta siyo za Muungano lakini tulishirikiana pamoja na Zanzibar. Kwa hili nakupa hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine kikubwa ambacho nakisema hapa labda pengine kwa watu wengine ambao wanasema kwamba labda Serikali hii haina kipaumbele au haijaweka mtazamo mkubwa katika kuangalia masuala ya Muungano ili waelewe, tunaelewa sisi kuna fedha za maji ambazo zimepita katika Jamhuri ya Muungano mkopo kutoka India, ni zaidi au karibu robo ya bajeti ya Zanzibar ambazo zimeenda kule, wasiojua walijue hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema hili kwa sababu wakati mwingine mtu ukiambiwa kipofu siyo lazima kwamba haoni, inawezekana mtu akapofua fikra. Kwa hiyo, humu kuna watu wamepofua fikra zao, zile fikra zao ndiyo vipofu hawawezi kuona, hata kama wana macho hawataweza kuona, hata kama wana masikio hawataweza kusikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la msingi labda nimnukuu Spika kwamba kumbe walemavu kweli wamo wengi humu, kwa sababu fikra pia nazo zinampeleka mtu kulemaa, akafikiria hata jambo la kuliona wazi asiweze kuliona. Kwa hiyo, hilo ni moja katika kuangalia mambo mazuri ambayo yamepangwa na yamefanyika katika Muungano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipengele ambacho Mheshimiwa amekizungumzia katika ukurasa wa 51, ushirikiano katika mambo ambayo siyo ya Muungano hasa katika masuala ya afya na nakwenda katika Bima ya Afya. Mfuko wa Bima ya Afya unafanya kazi Zanzibar, pia Mfuko huu wa Bima ya Afya unafanya kazi Tanzania Bara ambapo uko chini ya Wizara ya Afya. Jambo ninaloliomba hapa, muundo wa Halmashauri ambao uko huku ambao Wazee wanapata Bima ya Afya ni tofauti na muundo wa utawala kule Zanzibar ambapo mara nyingi Majimbo huwa yanajitegemea, tunajua Wazee kuna fedha zinatengwa kwa ajili ya kupatia Bima ya Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu au ushauri wangu, kwa nini tusiendeleze ushirikiano tukachukua katika ngazi ya Majimbo, likazungumzwa, likatazamwa kwamba linafanywaje ili tuweke huu ushirikiano katika kuwapatia wazee Bima ya Afya kama vile ambavyo wazee wanapata Bima ya Afya kupitia katika Halmashauri za Tanzania Bara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili binafsi katika Jimbo langu niliwahi kulitekeleza lakini zikatokea changamoto. Kwa hiyo kutokana na hizo changamoto zilizojitokeza, mwaka huu tumesimama. Kwa hiyo, naiomba Serikali yangu sikivu, hapa tuweze kuliratibu hili kama linaweza kufanyika hata katika ngazi ya Majimbo, kwa sababu katika Serikali ya Zanzibar hakuna utawala ambao uko maalum katika Halmashauri ambao unapelekewa fedha ili kuhudumia sekta za jamii. Majimbo yenyewe pengine kupitia Mbunge na Mwakilishi wanaweza wakafanya hili jambo, kwa hiyo tunaiomba Serikali ya Jamhuri ya Muungano iliangalie hili kupitia mzungumzo ya Wizara hii ya Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine alizungumza hapa Mheshimiwa Shamsi Vuai kwamba tuangalie jinsi gani uchumi mkubwa unaweza ukasaidia uchumi mdogo. Hapa moja kwa moja nije katika corporate tax. Tunajua kwamba pay as you earn inapatikana kama ilivyopangwa na makubaliano yalivyo. Nafikiri Mheshimiwa Waziri hili analifahamu. Pia custom duty na excise duty kwa Zanzibar wanakusanya wenyewe, lakini corporate tax inakusanywa kwa mujibu wa kampuni iliposajiliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa usajili mara nyingi, mtu atafanya usajili sehemu ambayo kuna urahisi wa kusajili na urahisi wa kusajili unakujaje, alipo regulator kwa mfano, benki nyingi sana haziwezi kuja ku-register Zanzibar, zita- register Tanzania Bara. Kwa hiyo, kwa kuwa zitakuja ku-register Tanzania Bara ina maana kwamba hata kodi yake itakuwa inalipwa Tanzania Bara. Kwa hiyo mapato haya yanayotokana na kodi ya kampuni tujaribu kuangalia kigezo kingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia kigezo kingine kwa sababu makampuni haya yanafanya kazi katika mazingira ya Zanzibar, wanawatumia wateja wale wa Zanzibar, wanafanya shughuli zao pale na mazingira ambayo yamewekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar lakini bado corporate tax zao wanalipa kwa Tanzania moja kwa moja. Tunaomba kungekuwepo kigezo cha operation au kama itakavyoonekana katika mazungumzo kwamba pia hizi corporation tax pia ziwe zinakusanywa Zanzibar kwa portion ya zile benki au taasisi za simu zinavyofanya kazi kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine katika hili, tumebadilisha Sheria kadhaa ambazo zinahusiana na mambo ya mapato ikiwemo ku-charge transactions whether za kwenye simu, miamala ya kifedha, lakini bado miamala ya kifedha kwa kuwa kwamba hivi vyombo vimesajiliwa Tanzania Bara haziwezi kwenda Zanzibar. Kwa hiyo, tutafute mazingira kwa sababu na Zanzibar wanatumia hizi benki, Zanzibar wanatumia hizi transaction, miamala hii waweze pia kuipitia na Zanzibar waweza pia kunufaika. Hili ni jambo ambalo nashukuru sana kama litafanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nianze na msemo mdogo unaosema kwamba muungwana ni yule ambaye akinena halafu anatekeleza. Mheshimiwa Naibu Waziri wa Muungano aliniahidi kwamba atakuja kunitembelea Jimboni na nashukuru akafanya uungwana ule akaja kunitembelea Jimboni, akaona mazingira niliyomuhadithia hapa, namshukuru sana. Namkumbusha tena Mheshimiwa Waziri aliwaahidi wananchi wangu baada ya kuja Jimboni kwamba atakuja kufanya jambo fulani la kimazingira ambayo aliyaona. Kwa hiyo namkumbushia na hili nalo pia aliangalie. Hili ni muhimu kama litafanyika kwa ajili ya kuboresha Muungano wetu na kufanya mambo ambayo yataweza kutusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni uvuvi wa bahari kuu. Katika uvuvi wa bahari kuu Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipanga kujenga bandari ambazo zitakuwepo Zanzibar pamoja na chombo cha kufanyia survey kwa uvuvi wa bahari kuu. Mpaka sasa hivi tunaona masuala haya yamekwama. Labda kupitia mazungumzo haya katika Wizara hii ya Muungano iweze kuangalia, kwa sababu Bandari ambazo ziko hata meli ziki-register kuja kuvua Zanzibar au kuja kuvua katika uvuvi wa bahari kuu, haziwezi tena kurudi kwa sababu mazingira ya bandari zetu kwa Tanzania Bara pamoja na Zanzibar siyo mazuri. Kwa hiyo, tufanye hayo mazingira yawe mazuri na tuweze kuendelea kunufaisha watu wetu katika uvuvi huu wa bahari kuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo, sina mengi ya kusema, naunga mkono hoja, Waziri wetu piga kazi.