Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Khadija Hassan Aboud

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kwa dhati kabisa kuwapongeza Viongozi wetu Wakuu wa nchi, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Viongozi wote wa Serikali pamoja na Wizara hii ambayo leo tunajadili bajeti yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mazingira ni suala pana na linahitaji mbio za haraka ili kunusuru nchi yetu. Kama lilivyoelezwa na Wizara yenyewe na hatua mbalimbali ambazo wanachukua napongeza kwa jitihada hizo ziendelee na wazo la kuongeza fedha katika bajeti ya Wizara hii ni muhimu kwa sababu ndiyo urithi wa nchi yetu na vizazi vijavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, historia ya Muungano ni pana, hivi sasa vizazi vingi tuliopo tumezaliwa baada ya Muungano. Kwa mantiki hiyo, vijana sisi ambao wengi wetu ni raia wa Tanzania tunaoishi sasa tunaupenda na tuko tayari kuupigania kwa nguvu zote Muungano wetu huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie changamoto za Muungano. Nashauri changamoto za Muungano pale zinapotatuliwa zitangazwe bayana kila mwananchi azielewe, kwa sababu ni changamoto nyingi zimefanyiwa marekebisho na zimeshafanyika kazi lakini bado wananchi hawaelewi. Nasisitiza pia ushirikiano wa sekta ambazo siyo za Muungano, kwa sababu raia wa nchi mbili hizi au wa Jamhuri ya Muungano wanatumia fursa mbalimbali kwa nchi zote mbili Zanzibar na Jamhuri ya Muungano kama hospitali, elimu na mengineyo, pamoja na utamaduni na mila zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa jina la sasa Tanzania una umri wa miaka 53, ni chombo muhimu sana kwa maisha na maendeleo ya Watanzania na hasa Wazanzibari wapenda amani, utulivu na maendeleo. Yeyote anayebeza au kudharau Muungano huu na kuwa hautakii mema tunamjua ni mmoja katika maadui wa nchi yetu. Dunia, Afrika na majirani zetu wanafahamu kwamba Tanzania ni nchi ya amani na hususan ikiwemo Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Muungano huu na Mapinduzi ya Zanzibar, majaribio mengi ya vitimbakwiri yalifanyika kutaka kudhoofisha au kuondosha kabisa, lakini kwa uimara wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Muungano wa Tanzania majaribio hayo yameshindwa. Moja kati ya jaribio hilo ambalo limeshindwa lilisababisha kifo cha muasisi wa Mapinduzi na Muungano Mheshimiwa Abeid Amani Karume, lakini kwa uimara wa Serikali zetu majaribio hayo yameshindwa na yataendelea kushindwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie miradi ambayo inatokana na fedha na mambo yanayohusu Muungano. Naomba nichukue nafasi hii kwa kifupi sana kwa wale wasiofahamu umuhimu na maendeleo ya Muungano. Kwanza ni ulinzi na usalama, hilo sina shaka nalo ni faida moja ya Muungano, nikigusia kwenye elimu kuna miradi mikubwa ya uanzishwaji wa shule za sekondari 19 pamoja na ujenzi wa Chuo cha Benjamin Mkapa kule Pemba, hizo ni faida za Muungano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukarabati wa shule sita za sekondari zikiwemo shule tatu zilizomo katika Jimbo la Mheshimiwa Ally Saleh shule ambazo ni Forodhani, Hamamni na Tumekuja, zimo ndani ya Jimbo moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Mifuko hii ya Muungano tumepata mafunzo ya Walimu ambapo jumla ya Dola za Kimarekani milioni 42 zilitumika kwa mkopo wa Benki ya Dunia zilizokopwa na SMT. Pia kuna dola milioni 10 kwa ujenzi wa school mpya sita Unguja na nne Pemba. Hayo ni matunda na mafanikio ya Muungano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hayo tu, kuna miundombinu ya barabara ikiwemo Mkapa road Mkoa wa Mjini Magharibi, kuna barabara Pemba zilizojengwa kwa Mfuko huu wa Muungano.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi juzi tu tarehe 4 Julai, Mkopo wa India wa USD 92.1 milioni kwa ajili ya mradi mkubwa wa maji Mkoa wa Mjini Magharibi. Pia kuna uimarishaji wa miundombinu ya maji mijini na vijijini kwa mkopo wa ADB wa dola milioni 21. Pia tumesikia leo miradi ya mazingira kupitia TASAF na mifuko mingineyo kuhifadhi mikoko, ujenzi wa kuta, kuzuia bahari, bahari inakula visiwa vyetu lakini Mifuko ya Muungano inakwenda kusaidia kulinda bahari isile visiwa vyetu kule Zanzibar. Pia kuna miradi mikubwa ya mikopo ya SMT ndiyo inayodhamini Zanzibar pale ambapo itashindwa SMT inalipa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tulivyoona Mifuko ya TASAF imesaidia wajasiriamali wetu wadogowadogo, pia imesaidia masoko, ujenzi wa vituo vya afya na zahanati, imesaidia kaya maskini, yote hayo ni matunda na faida za Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijamaliza naomba niunge mkono hoja kwa asilimia mia moja. Muungano wetu imara tutaulinda, tutaudumisha, kwa maslahi wa wananchi wote wa Tanzania, vizazi vya sasa na vizazi vijavyo. Dunia inaona, Afrika inaona na sisi tuko imara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha ahsante sana na naunga mkono hoja.