Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kinondoni
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MAULID S. ABDALLAH MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumshukuru Allah (S.W.) kwa kuniwezesha kuchangia hoja hii muhimu kwa mustakabali wa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira ya nchi yetu ni kitu muhimu sana na yasipolindwa bila shaka madhara yake yanaweza kutuathiri sote kama Taifa bila ya kubagua nani amesababisha au nani hakusababisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu kubwa ya uharibifu wa mazingira ni sisi wenyewe tunaoishi na kuyatumia mazingira haya mfano, kilimo kisichozingatia uharibifu wa mazingira; kama vile kulima kwenye misitu yetu ya hifadhi, kilimo kwenye vyanzo vya maji, kulima kwenye maporomoko bila ya kufuata kanuni ya kilimo hasa kwenye maeneo ya maporomoko. Aidha, mifugo isiyozingati mbinu za kisasa, mfano, kufuga na kulisha kwenye hifadhi za misitu na mbuga za wanyama, kufuga wanyama wengi kuliko uwezo wa ardhi iliyopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Bahari, Mito, Maziwa na Mabwawa kutumia uvuvi haramu wa mabomu au nyavu ndogo maarufu kama jalife. Katika yote haya tusisahau ukataji wa mkaa na kuni kama nishati hasa kwa ajili ya Majiji ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya na Tanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha hayo, bado tuna tatizo kubwa la uharibifu wa mazingira katika majiji na njia kuu kwa uzalishaji wa taka ngumu na majitaka kutoka majumbani na viwandani. Aidha, vifungashio vya bidhaa za viwandani na vibebeo mfano, mifuko ya plastiki, maboksi na plastiki ngumu na sehemu kubwa yanayochafua na kuharibu mazingira yetu. Mfumo mbovu wa utiririshaji wa maji taka kutoka viwandani na majumbani kwenda maeneo maalum kwa ajili ya kuhifadhi, kuyatupa au kuchakata ili uweze kutumika tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni au ushauri;
(i) Mifugo yetu iwe kwa kiwango kisichoharibu mazingira hivyo basi, wafugaji wetu waelimishwe ufugaji wa kisasa wenye tija yaani mifugo kidogo tija kubwa.
(ii) Wafugaji wasihamehame kiasi ambacho wanaweza kuharibu mazingira kwa sehemu kubwa badala ya eneo dogo kama hawatahama. Pia wafundishwe kupanda nyasi kwa ajili ya malisho ya wanyama wao.
(iii) Wavuvi wadogowadogo na wale wanaotumia zana haramu, wafundishwe uvuvi bora na Serikali iwapatie vifaa vya kisasa vya kuvulia samaki ili waweze kupata mavuno mengi ya samaki jambo ambalo ndicho kivutio kikubwa cha kutumia uvuvi haramu.
(iv) Wakata mkaa; katika hili Serikali naishauri yafuatayo:-
• Mosi, Serikali iwafundishe wakulima njia mbadala ya kujipatia kipato kinyume na kuuza mkaa. Wanakijiji wengi hawana njia mbadala ya kupata fedha zaidi ya mkaa.
• Pili, kusambaza gesi majumbani katika Majiji ya Dar es Salaam na mengine. Aidha, tuna kila sababu ya kupunguza bei ya umeme ili watu wapike kwa jiko la umeme.
(v) Serikali iwe na takwimu zote za wazalishaji taka wa viwanda au majumbani na kila mtu achangie gharama za usafi na utunzaji wa mazingira kulingana na kiwango chake cha uchafuzi wa mazingira.
(vi) Serikali iwe mfano bora wa kutunza mazingira na kusimamia mazingira kwa kutumia vyombo vyake mfano mzuri, utunzaji wa mikoko Jangwani na daraja la Salenda. Serikali isiache mikoko na uoto wa asili ukifa maeneo ambayo Serikali au Ofisi ya Makamu wa Rais ni karibu yake.
(vii) Serikali isiweke ubaguzi wa utekelezaji wa Sheria. Mfano, Sheria ya mita sitini ya Mito. Kwangu Dar es Salaam Ofisi ya DART Jangwani na Jengo la MOI Muhimbili ni majengo yaliyo karibu na mito ndani ya mita sitini, lakini hayaguswi badala yake Serikali imeenda kubomoa nyumba za wananchi ambao Sheria imewakuta, jambo hili si utaratibu wa Serikali.
(viii) Serikali ishirikiane na Manispaa za Mijini zenye kuzalisha taka nyingi ili ziweze kujenga mitambo ya kuchakata taka na kuwa mbolea na manispaa zitalipa kidogo kidogo kwa Serikali; jambo hili lina faida ya mazingira, ajira, mbolea na kadhalika.
(ix) Sheria itungwe ya kudhibiti uzalishaji wa plastiki ngumu na laini ili kupunguza au kuondoa taka ambazo si rahisi kuzidhibiti.
(x) Wakulima wetu waelimishwe kilimo bora cha kisasa chenye tija. Bila shaka wananchi wakielimishwa vizuri hawana haja kwenda kwenye vyanzo vya maji, maeneo ya hifadhi na maeneo ya maporomoko.
(xi) Kuanzisha operation ya kupanda miti mingi kuliko kasi ya wakata miti na wavuna misitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Ahsante.