Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuchangia Wizara hii ya Sheria na Katiba. Kabla ya kuanza kuchangia, naomba ku-declare interest kwamba mimi taaluma yangu ni ya ulinzi na usalama katika sekta binafsi lakini vilevile nina kampuni kubwa ya ulinzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipeleka kwa Katibu wa Bunge Muswada Binafsi kama ilivyo katika Kanuni yetu ya 81(1)(2) na (3), Toleo la 2016. Baada ya kupeleka Muswada wangu binafsi katika Ofisi ya Katibu wa Bunge alinijibu rasmi kwamba Muswada ule ulikuwa ni mzuri na Serikali iliuchukua Muswada huo kwa nia ya kuuleta tena Bungeni baada ya kutimiza kanuni za kuleta Muswada Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, makampuni binafsi ya ulinzi yalianza mawili tu mwaka 1980 lakini leo yapo makampuni karibu 850, yameajiri askari walinzi wengi zaidi ya mara tano au mara sita ya Jeshi la Polisi. Makampuni haya yanafanya kazi nzuri sana ya kulinda raia na mali zao lakini hayana miongozo, kanuni, sheria na wala hayana mamlaka binafsi ya kuongoza makampuni haya kama ilivyo kule nje yalikotokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilifungua milango ya sekta ya ulinzi binafsi hapa nchini na ikafungia nje sheria za kuyaongoza makampuni haya. Suala hili limekuwa ni tatizo kwani makampuni haya yana silaha, yanavaa sare kama za jeshi, yanacheza gwaride, yanafuata kanuni za kijeshi na yameajiri wataalam kutoka nje ya nchi wenye taaluma kubwa ya kijeshi. Hatuwezi kuyazuia tena makampuni haya hapa nchini yasifanye kazi kwa sababu kila kwenye uwekezaji mkubwa makampuni haya yapo na yanafanya kazi nzuri sana, tunachoweza kufanya ni kuyadhibiti makampuni haya binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, makampuni haya hayawezi kudhibitiwa bila sheria. Ni lazima Sheria inayoitwa Private Security Industry Act or Bill iletwe Bungeni ipitishwe. Huko yalikotokea makampuni haya kote, wenzetu Kenya, Uganda, Afrika Kusini, Uingereza, Marekani, Ulaya ziko sheria na mamlaka ya sekta ya ulinzi binafsi. Sheria ile niliyoleta mimi kama Muswada Binafsi ilizingatia kuanzishwa kwa mamlaka ya sekta binafsi ya ulinzi. Nia ile na sababu hiyo haijafutika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa, ajaribu kulieleza Bunge lako kama maslahi na madhumuni ya kuwepo sheria sasa yamefutika au mchakato wake umefikia wapi ili tujue tuweze kudhibiti makampuni haya ya ulinzi binafsi yaweze kulipa kodi na vilevile yanaajiri watu kinyume na kanuni. Kule kwenye Mahakama ya Kazi, robo tatu ya kesi zote ni za makampuni ya ulinzi, inakuwa kama ile Mahakama ya Kazi imeandaliwa kwa sababu ya makampuni ya ulinzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile makampuni haya yanatumia sheria ya kiraia, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004. Sheria hii ni ya kiraia na imepigwa marufuku majeshini kote. Hairuhusiwi kutumika Polisi, JWTZ, Magereza wala Immigration. Sheria hii kutumika katika sekta ya ulinzi binafsi inaenda kinyume na inashindwa kuyadhibiti makampuni hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii inaruhusu migomo. Hebu tufikirie ikatokea siku makampuni ya ulinzi yamegoma au wafanyakazi wa kampuni za ulinzi wamegoma, wakaacha malindo wazi na wana silaha mikononi, itakuwaje? Naomba Waziri atakapokuja hapa aeleze Bunge lako hili amefika wapi na Sheria hiyo niliyoipendekeza ya Sekta ya Ulinzi Binafsi yaani Private Security Industry Act or Bill pamoja na pendekezo la kuanzishwa Private Security Industry Authority.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo niende kwenye Idara ya Mahakama. Waziri wa Sheria hapa mwanzoni alisema kwamba wangependa kila Kata iwe na Mahakama. Kule kwetu Tabora Kaskazini (Uyui) kuna Mahakama ya Mwanzo ina kila kitu, Mahakama ipo, ina mabenchi, jengo zuri la Mahakama, nyumba nane za wafanyakazi wa Mahakama lakini imetelekezwa, huu ni mwaka wa 10 haifanyi kazi. Watu wameiba milango na madirisha yaliyojengwa kwa thamani kubwa na mpaka sasa sijui sababu ni nini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu nimekuwa Mbunge, wananchi wananiuliza imetokea nini Mahakama ikatelekezwa na kuna kesi nyingi. Juzi juzi kumetokea kesi ya mauaji kule Tabora, Uyui ndiyo inaongoza kwa kesi mbaya za mauaji, wizi na kadhalika lakini Mahakama ya Mwanzo imefungwa. Nimeona katika hotuba yake Mheshimiwa Waziri anaongelea kujenga Mahakama za Mwanzo katika maeneo mbalimbali, lakini Mahakama ya Mwanzo katika Kata ya Upuge, Wilaya ya Uyui, Mkoa wa Tabora imesimama na haifanyi kazi na majengo yanabomolewa tu wananchi wanachukua kama shamba la bibi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba atakapokuja Mheshimiwa Waziri kuhitimisha hoja yake ya bajeti, anieleze kimetokea nini mpaka Mahakama ya Mwanzo inayotakiwa sana kutelekezwa. Pia anieleze majengo yale yafanyweje sasa, maana watu wanaingia na kuiba milango kama haina mwenyewe. Mimi ningeshukuru Mahakama ile ingeanzishwa tena kwa sababu kesi za kutosha zipo, lakini kama kuna sababu iliyofanya Mahakama ile ifungwe naomba nielezwe ili nikawaambie wananchi wangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuniruhusu kwa heshima kubwa, nakushukuru sana na niwaachie wenzangu wachangie.