Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
HE. LATHIFAH H. CHANDE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote napenda kwanza kuanza kwa kuchangia sekta ya ujenzi hususan barabara. Katika Mkoa wetu wa Lindi tunashukuru barabara imejengwa ambayo tunaunganishwa kutoka Mkoa wa Lindi hadi Mkoa wa Mtwara na kuelekea Ruvuma. Sasa utata unakuwepo katika barabara za kuelekea kwenye Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni suala la kusikitisha sana kwa sababu inafika wakati unaenda kwenye Wilaya ya Liwale na Nachingwea lakini inakuwa kama ile ni barabara ya kuelekea kijijini. Naiomba Serikali iangalie katika kujenga barabara zinazoelekea katika hizo Wilaya ili nazo ziweze kuwa katika kiwango cha lami kuliko kila siku kuendelea kuiboresha katika kiwango cha vumbi. (Makofi)
Mhshimiwa Naibu Spika, hii pia inaleta adha kubwa kwa watumiaji wa hizi barabara hususan Wana-Lindi pale wanapohitaji kutoka Wilaya moja kwenda Wilaya nyingine. Imepelekea hadi akina mama wanapoteza maisha yao pale ambapo wanahitaji kuhamishwa kutoka Hospitali ya Wilaya na kupelekwa kwenye Hospitali Mkoa ya Lindi, kutokana adha hii ya barabara kuwa mbovu.
Mheshimiwa Naibu Spika, upembuzi yakinifu umefanyika kutoka barabara ya Nanganga kuelekea Ruangwa. Sasa sijui ni kwa kuwa kuna Waziri Mkuu ambaye ana interest pale, kwa sababu inawezekanaje kuwe na mpango wa kujenga barabara ya kutoka Nanganga kwenda Ruangwa na iachwe hii inayoelekea Nachingwea na Liwale?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Serikali iweze kuliangalia hilo ili kuwatoa wananchi wa eneo hilo kwenye adha ya tatizo la usafiri, especially kipindi hiki cha masikika, usafiri inakuwa ni shida. Kwa gari dogo unatumia siku mbili kutoka Nangurukuru hadi kufika Liwale kwa kupitia barabara ya Njinjo ambayo ina urefu wa kilometa 230. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile hata wafanyabiashara wanaishia kuharibikiwa na magari njiani na kutoweza kuendelea kutokana na ubovu huu wa barabara na kupelekea hadi kufika siku saba, ambayo ni wiki nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuishauri Serikali iweze kuangalia hili na pia ikiwezekana Waziri husika aweze kutupa jibu; lini atahakikisha kwamba barabara hizi za kutoka Nanganga - Nachingwea hadi Liwale na kutoka Nangurukuru hadi kufika Liwale zitajengwa katika kiwango cha lami? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuchangia katika sekta ya uchukuzi juu ya matumizi ya bandari yetu katika kukuza mapato ya Taifa letu. Hadi sasa hivi shehena zinazopita katika bandari zetu zinaendelea kushuka na zimeshuka kutoka asilimia 5.2 mwaka 2014/2015 hadi kufika asilimia 0.1. Hii ni ishara mbaya sana kwa mapato ya nchi yetu. Maana yake ni kwamba mapato ya bandari yanaendelea kushuka.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia Machi, 2017 takwimu za TRA zinaonyesha kwamba mapato yaliyotokana na forodha, ikiwemo bandari ni shilingi trilioni 4.3. Sasa kama kusingekuwa na upungufu wa shehena katika Bandari, maana yake haya mapato yangeongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ukiangalia bajeti nzima ya mwaka 2016/2017 ni shilingi trilioni 29.54, lakini tumeendelea kushuhudia mapato ya bandari yanavyozidi kushuka kwa kasi. Sasa je, tutaweza vipi kuboresha vyanzo vyetu vya mapato kwa usimamizi mbovu kama huu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania tumebarikiwa kijiografia kuwepo katika Ukanda wa Maziwa Makuu, lakini hii lawama Serikali haiwezi kuikwepa kutokana na kuwa na sera mbovu juu ya uratibu wa shughuli za bandari. Hili ni janga kwa Taifa letu.
Napenda kuishauri Serikali iweze kuboresha sera zake juu ya uratibu wa bandari ili tuweze kutumia vizuri baraka hizi tulizopewa na Mwenyezi Mungu ya kuwa strategically positioned na hatimaye kuweza kuongeza mapato yatokanayo na bandari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuchangia juu ya hii sekta ya uchukuzi kuhusiana na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL). Naungana mkono na juhudi zilizotumika katika kufufua Shirika hili la Ndege la ATCL, lakini siungi mkono njia zinazotumiwa na Serikali katika kusimamia Shirika hili la Ndege. Kwa nini nasema hivyo? Nasema hivyo kwa sababu kitendo cha Serikali kununua ndege kwa gharama ya shilingi bilioni 500 na kuzikodisha hizi ndege kwa Shirika la ATCL naona ni kitu ambacho ni kibaya kwetu sisi kama Taifa ambalo kwa sasa hivi uchumi wetu upo dhaifu na bajeti ikiwa ime-under perform. Kwa nini tumeshindwa kuendelea na mfumo wa Public Private Partnership (PPP) ambapo wenzetu wa Kenya tukiangalia Kenya Airways asilimia 29.7 shares zinamilikiwa na Serikali ya Kenya huku asilimia 26.8 zinamilikiwa na Shirika la Ndege la KLM.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile wamejiingiza katika soko mitaji, soko la hisa Dar es Salaam, Uganda na Nairobi ambapo umma nao umeweza kumiliki hizo shares nyingine zilizobaki. Kwa nini ishindikane kwetu sisi? Tuna mambo mengi ambayo tunahitaji ku-prioritize na siyo kununua ndege. Kwa sababu tungeweza kuendelea huu mfumo wa PPP, japo tulifanya vibaya, hii siyo kwamba tuachane kabisa na huu mfumo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili suala la Serikali kununua ndege kwa gharama hizo za shilingi bilioni 500 kwangu mimi naona siyo sahihi kwa sababu tuna mambo mengi. Vijijini maji hamna, dawa hamna katika sekta ya afya, elimu pia haijaboreshwa kwa kiwango kile inavyotakiwa, lakini tunahangaika kununua hizi ndege. Napenda kupata majibu juu ya kwa nini Serikali imeshindwa kuendelea na huu mfumo wa PPP? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile napenda kuishauri Serikali iweze kusisitiza ATCL iweze kukabidhi mahesabu yake kwa sababu hadi Februari Waziri Mkuu aliagiza CAG iweze kupatiwa mahesabu ya madeni na mali juu ya management nzima ya ATCL tangu waweze kupatiwa hizi ndege mwaka 2016. Nashauri kwamba wakabidhi mahesabu haya ya tangu 2009 ambayo tangu mwaka 2009 walishindwa kuyakabidhi kwa CAG. Kwa sababu kuna poor management ya ATCL inayopelekea kuongezeka kwa madeni na kutokuweza kujua exactly mali zetu za ATCL ziko kiasi gani mpaka dakika hii. Kwa hiyo, kikubwa napenda pia kushauri Serikali iweze kufanya hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, yangu ni hayo. Ahsante, nashukuru.