Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Mussa Bakari Mbarouk

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza mimi nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenijalia leo kuwa na afya njema na kuweza kuchangia Hotuba hii ya Wizara ya Ujenzi. Vilevile pia nawashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Tanga kwa kazi waliyonipa ya kuja kuwawakilisha katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano. Tatu naanza kwa kuunga mkono Hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, mimi sitapongeza sana, lakini niseme tu sisi watu wa Pwani tuna kawaida tunajua kwamba baba ndio mlezi wa familia na anapotimiza majukumu yake ametimiza majukumu hakuna haja ya kumsifu, ndiyo kazi yake hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naanza moja kwa moja kuchangia sekta ya barabara. Kwa muda mrefu tumetoa kilio watu wa Tanga kwa barabara ya Tanga – Pangani – Bagamoyo. Barabara hii ni ya kihistoria, barabara hii imepita katika majimbo matatu, kuanzia Tanga Mjini, Pangani hadi Bagamoyo na pia Muheza na ina Wabunge watatu au wanne, lakini kwa muda mrefu imekuwa haikufanyiwa matengenezo lakini safari hii tunaambiwa imetengewa shilingi bilioni nne ambayo ni sawasawa na asilimia 15 ya mradi mzima wa barabara.
Mimi kwanza niiombe Serikali ikamilishe asilimia 100 kabisa ili barabara ile iweze kutumika kwa wakati wote. Kwa sababu tukumbuke barabara ya Pangani imepita ahadi za Marais wanne waliopita, Rais Nyerere, Rais Mwinyi, Rais Mkapa na Rais Kikwete, wote waliahidi kujenga katika kiwango cha lami lakini ilishindikana. Tunaomba safari hii barabara ile ijengwe kwa kiwango cha lami na tusije tukaambiwa fedha bado hazijapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ninachoiombea barabara ya Pangani kujengwa, kuna Mbuga ya Saadani ambayo ni mbuga pekee duniani ukifika time za jioni kama hizi utakuta wanyama wote wamekusanyika beach kama vile binadamu. Kwa hiyo, hiyo nayo ni hali tunayoitaka barabara ya Pangani ijengwe itakuwa ni chanzo cha uchumi lakini pia itaboresha utalii wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala linguine ninalotaka kuzungumzia ni suala zima la reli. Kuhusu reli ya kiwango cha standard gauge niliwahi kusema mwaka jana kwenye bajeti kama hivi kwamba waswahili wanasema mwiba uingiapo ndipo utokeapo. Reli ya Tanzania au Tanganyika wakati huo ilianza kujengwa Tanga kuanzia mwaka 1905 ikaanzia Tanga ikaenda mpaka Moshi ikafika mpaka Arusha baadaye ikagawanywa ikapita Dar es Salaam ikaingia Morogoro hadi kufika Kanda ya Ziwa, lakini leo tunaona wenzetu katika standard gauge mnatutenga watu wa Tanga. Tunataka tuwaambie watu wa Kanda ya Ziwa sisi Tanga ndio walimu wenu, kwa hiyo, nataka reli ya standard gauge, Serikali pamoja na kwamba wanataka kuianzisha Dar es Salaam, lakini Tanga msije mkaisahau kwa sababu Moshi, Tanga yote hiyo ndiyo reli ya kwanza ilianza kujengwa.
Kwa hiyo, tunapenda keki hii ya Taifa igawanywe kwa usawa ambao hautaleta manung’uniko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu usafiri wa majini, nashukuru kwamba kampuni ya Bakhresa imetuletea meli kubwa inayofanya usafiri kati ya Pemba na Tanga na sasa ajali zitakuwa zimepungua. Kama mtakumbuka Januari, 09 ilitokea ajali kubwa kabisa ya boti ikaua zaidi ya watu 15.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfanyabiashara binafsi amejitolea kuleta meli, lakini bado kuna siku na siku; tunataka Serikali nayo ituwekee meli pale ili hata kama mfanyabiashara anaweza kuamua wakati wowote akiona hapati faida akaamua kuondoa meli yake, lakini ya Serikali itakuwa inahudumia wananchi wake. Kwa hiyo, mimi nakutaka Mheshimiwa Naibu Spika na Mheshimiwa Waziri mhakikishe Serikali nayo ilete meli katika bandari ya Tanga itakayotoka Tanga kwenda Pemba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na yote Tanga zimekuwa zikitokea ajali za mara kwa mara. Nimekusikia Mheshimiwa Mbarawa asubuhi ukisema kuna kikosi kazi cha uokoaji, lakini kikosi kazi kile hakina zana za kufanyia kazi, na hata pale wanapokuwa na zana za kufanyia kazi hawana mafuta. Iliwahi kutokea ajali moja, mimi na Mheshimiwa Khatib, wakati huo mimi ni Diwani, tukakubali kutoa hata mafuta ili wakaokolewe ndugu zetu ambao boti ilikuwa inawaka moto, lakini ikawa pia tunaambiwa mpaka Meneja wa Bandari atoe go ahead ndipo chombo kianze kutoka, kwa hiyo, hili ni tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka kikosi cha uokoaji kama kipo kweli Mheshimiwa Waziri akiimarishe kiwe na helikopta, kiwe na boti, kisisaidie tu kuokoa maisha ya watu wanaopata ajali baharini, lakini hata zinapotokea ajali za magari. Leo imetokea ajali Daraja la Wami au barabarani watu wengine wanapoteza maisha kwa sababu hakuna usafiri wa haraka unaoweza kuwafikisha katika hospitali zetu.
Kwa hiyo, nakuomba Mheshimiwa Waziri katika bajeti yako uongeze fungu ambalo litasaidia kupata hata helikopta za uokoaji zisaidie kuwahisha majeruhi katika hospitali zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusu usafiri wa anga. Usafiri wa anga Tanga imekuwa kuna kizungumkuti kidogo, uwanja ni uleule wa tangu mkoloni. Tunahitaji Tanga kutokana na uwekezaji mkubwa unaokuja tupate kiwanja cha ndege cha kimataifa (Tanga International Airport) kwa sababu pana uwekezaji wa bomba la mafuta, Tanga kuna utalii, vile vile Tanga pia kuna Tongoni Ruins, Amboni Caves na mambo mengine pamoja na Amani Research Institute, zote hizo zinatakiwa tuweke uwanja wa ndege wa kisasa ili tuweze kupata mafanikio ya uchumi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine katika hicho kikosi pia pawe na divers. Tumeona wakati wa ajali ya MV Bukoba watu walishindwa kuokolewa kwa sababu hatuna divers, tumeagiza divers kutoka Mombasa - Kenya, hii ukiangalia inatutia udhaifu kidogo nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Kuhsu suala la Daraja la Wami. Nimekuwa nikisema Daraja la Wami ni link yaani kiunganishi kati ya Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara na hata nje ya nchi kama Kenya kupitia Nairobi mpaka Ethiopia huko. Lakini daraja lile ni la tangu mkoloni, daraja lile lina single way hayawezi kupita magari mawili kwa wakati mmoja, hivi Serikali inashindwa kujenga Daraja jipya la Wami? Nimeona kwenye taarifa ya bajeti yako umetenga fedha, lakini nasema iwe ni kweli. Daraja la Wami limekuwa likipoteza maisha ya watu na mali zao. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, naomba Daraja la Wami lijengwe daraja kubwa na jipya la kisasa kama lilivyokuwa la Kigamboni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Bandari ya Tanga. Bandari ya Tanga imekuwa ikikimbiwa na wafanyabiashara kwa sababu kuna tofauti kubwa na usumbufu mwingi unaotokea katika Bandari ya Tanga na uliwahi kutoa taarifa kwamba Bandari ya Tanga imekuwa inafanya kazi kwa hasara, inafanya kazi kwa hasara kwa sababu wafanyabiashara wanaikimbia. Mfanyabiashara yuko radhi apitishe mzigo wake Bandari ya Mombasa, Kenya azunguke Holili, Kilimanjaro ndipo aje Tanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, kitabu cha kodi ni kimoja katika mipaka yetu yote ya Tanzania kwa nini watu wanaikimbia Bandari ya Tanga? Ni kwa sababu pana usumbufu na vilevile pana dosari za hapa na pale. Si hivyo tu hata border ya Horohoro kuna matatizo, wafanyabiashara pia wanakimbia na sasa hivi Serikali imeanzisha utaratibu kwamba kuna watumishi wa TRA ambao wapo Mombasa, Kenya wanafuatilia makontena huko huko, ukija Horohoro tena ushushe mzigo tena, ni usumbufu kwa wafanyabiashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi napenda nimshauri Mheshimiwa Waziri, aboreshe Bandari ya Tanga pasiwepo na usumbufu, mizigo itoke kwa muda mfupi ili wafanyabiashara waweze kuitumia vizuri Bandari ya Tanga, lakini pia tuongeze mapato ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala zima la ununuji wa ndege. Tunashukuru kuwa Bombardier zimepatikana, zifike Tanga, lakini ndege zile…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.