Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Dr. Mary Machuche Mwanjelwa

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mbeya Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

HE. DKT. MARY M. MWANJELWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia. Awali ya yote ninamshukuru sana Jehova kwa kunifanya hivi nilivyo. Mimi nitachangia katika maeneo mawili tu kwa leo, katika eneo la uchukuzi pamoja na ujenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa sijamtendea haki Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano, jemedari wetu na mtumishi wa Mungu huyu Dkt. John Pombe Magufuli kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya Tanzania tumeweza kuwa na flyovers Dar es Salaam na tutakuwa nayo, lakini pia Serikali imeweza kujenga standard gauge kwa upande wa reli ya kati. Ninaamini sasa na reli yetu ya TAZARA itaangaliwa upya ili iweze kuboreshwa zaidi kutokana na umuhimu wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Ndege la Taifa (ATCL). Sasa hivi tumeweza kuwa na national carrier yetu, ni jambo jema na shirika hili limefufuliwa. Napenda kutia mkazo kwa Waheshimiwa Wabunge ambao wamesema kabisa kwamba mashirika haya ambayo yako chini ya Wizara hii, yaweze kupewa full autonomy ili yajiendeshe kibiashara, kwa maana ya kwamba yasiingiliwe ili marketing teams zao ziwe na ubunifu zaidi. Kana kwamba hiyo haitoshi wajaribu kuangalia ni jinsi gani wanaweza wakawa wabunifu kimkakati zaidi kujaribu kwenda katika nchi ambazo zitakuwa zinatuletea mapato mengi zaidi kwa kuongoza utalii wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niende kwetu sasa kule katika uwanja wa kimataifa wa Songwe pale Mbeya. Katika ukurasa wa 169 tumeona Serikali imetenga milioni 1,530 kumalizia jengo na mambo mengine, lakini mimi nilikuwa ninaomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa ku-wind up atueleze suala zima la taa za uwanja huo wa ndege wa Songwe kutokana na umuhimu wake. Kuna ndege mara kwa mara zimeshindwa kutua, wewe mwenyewe ni shahidi kutokana na kwamba uwanja huo hauna taa. Kwa hiyo, nilikuwa naomba pesa ya dharura iweze kutolewa ili uwanja wa ndege wa Songwe tuweze kupata taa wakati wowote wananchi waweze kufurahia huduma hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kuzungumzia naamini wote watasema na Mheshimiwa Waziri anaelewa pale kwamba siwezi kukaa chini bila kuzungumzia barabara ya by-pass, barabara ya mchepuko kutoka Uyole hadi uwanja wa ndege wa kimataifa wa Songwe, na jambo la kusikitisha sijaona hata kwenye kitaba cha taarifa ya Mheshimiwa Waziri hapa, sijaona commitment ya Serikali. Hili jambo ni kizungumkuti, nimekuwa nikilipigia kelele mpaka Waziri aliyepita wa Ujenzi ambaye ni Rais wetu mpendwa sasa hivi, hili jambo analijua na alishatuahidi. Vilevile kana kwamba haitoshi mpaka kwenye vikao vyetu vya Road Board vya Mkoa tulishakubaliana kwa pamoja, tatizo ni nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Mheshimiwa Waziri atueleze hapa wana Mbeya tusikie, kwa sababu foleni msongamano kutokea Uyole mpaka Mafiati pale barabara haipitiki kabisa, dakika 10 inachukuwa saa tatu. Mimi bila kusita Mheshimiwa Waziri kaka yangu ninaekupenda na kukuheshimu sana nitashika shilingi mpaka kieleweke, maana hili jambo sasa hatuelewi sisi Wana-Mbeya.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini barabara hii ya mchepuko madhara yake ni mengi, inaleta ajali, inaharibu barabara. Vilevile itakapokuwa ina mchepuko sisi wana Mbeya kwetu ni faida kwa sababu tunaweza tukawa pia tuna bandari kavu. Ninayoyazungumzia ni haya malori
makubwa katika hii barabara ya mchepuko, sijazungumzia magari madogo; kwa hiyo Mheshimiwa Waziri anaelewa na alishakuja Mbeya na tumezungumza sana hili jambo lifike muafaka na lifike mwisho, maana mambo haya ya upembuzi yakinifu hata Mheshimiwa Rais hataki kuyasikia, tunataka utekelezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kabla sijakaa ni barabara ile ya Isyonje – Mbeya Vijijini hadi Makete kupitia Kitulo, hii barabara inaunganisha mikoa miwili. Kwa hiyo, nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri atueleze, kwa sababu kule kuna Hospitali ya Mission ya Ikonda ambayo inasaidia wananchi wengi sana, actually wananchi wote wa Mikoa ya Nyanda za juu Kusini.
Kwa hiyo, nilikuwa ninaomba barabara ya kuunganisha mkoa wa Mbeya na mkoa wa Njombe kwa maana ya kwamba Makete kupitia Kitulo kwa ajili ya wananchi wetu hawa wanokweda kwa wingi kuhudumiwa pale Ikonda basi Mheshimiwa Waziri atuletee majibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache ninaomba kuunga mkono hoja bajeti hii, ahsante sana.