Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nyamagana
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie walau maneno machache katika hii Wizara muhimu kabisa juu ya masuala mazima ya miundombinu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa maneno machache ya shukrani nikimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini pamoja na Waheshimiwa Mawaziri wa Wizara husika juu ya kazi njema na nzuri wanazoendelea kuzifanya katika kuhakikisha suala zima la miundombinu ya barabara, usafiri wa maji na nchi kavu unafanyiwa kazi na unakamilika kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na shukrani hizi nafahamu uko upanuzi wa uwanja wa ndege, tumeziona fedha pale Mwanza na niwapongeze sana kwa kutumia zaidi ya shilingi bilioni 18 kwa fedha za ndani na shilingi bilioni tano peke yake fedha za nje. Hii tafsiri yake ni kwamba zoezi hili linaweza kukamilika kwa wakati kama tulivyokusudia tofauti na tungetazamia sana kutumia fedha za nje. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili niwashukuru kwa upanuzi wa barabaraya kutoka Furahisha kwenda Kiwanja cha Ndege, kwa barabara nne. Ni kitendo kizuri ambacho kitaendelea kuujenga Mji wa Mwanza uendelee kubaki kuwa mji bora na mji wa pili kwa ukubwa Tanzania katika kuhakikisha shughuli zote za maendeleo na uzalishaji mali za kiuchumi zinazoifanya Mwanza kuwa mji wa pili katika kuchangia pato la taifa iendelee kuongeza zaidi ya pale ilipo leo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ili tuweze kufikia malengo haya tunayoyafikiria liko suala la barabara za kupunguza msongamano. Mara kadhaa nimekuwa nikisema, lakini nasikitika sana kwa sababu hata vikao vya RCC Mwanza mara kadhaa vimeshafanya mapendekezo zaidi ya vikao miaka mitatu mfululizo. Vinafikiri kupandisha barabara ya kutoka Buhongwa kupita Lwanima, Sawa, Kanindo kutokea Kishiri – Igoma na Fumagira kama itajengwa kwa kiwango cha lami, barabara yenye urefu wa zaidi ya kilometa 11.8 inaweza kusaidia sana Mji wa Mwanza kufunguka na tukaendelea zaidi kuwa kwenye hali nzuri ya kiusafiri. Lakini hii ni pamoja na barabara kutoka Mkuyuni kupita Igelegele - Tambukareli - Mahina na kwenda kutokea Buzuruga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiofichika kwamba mji wa Mwanza unakua, na kama mji wa Mwanza unakua na tunatambua ndiyo mji ambao uko kwenye kasi ya kuchangia pato la Taifa, sioni tunapata kigugumizi gani kuhakikisha kwamba barabara hizi zinafunguka kwa urahisi ili unapokuza uchumi wa Mwanza unaendelea kuchangia/ kuongeza pato la Taifa kutokea kwenye Mkoa huu ambao ni Mkoa wa pili kwenye kuchangia pato la Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimesema hapa ni ukweli usiofichika kwamba Mwanza ndiyo Mji pekee unaokua kwa kasi zaidi katika East Africa. Ukichukua Afrika ni mji wa tano katika Majiji kumi yanayokuwa kwa kasi. Leo hatuangalii kama kuna umuhimu wa kuendelea kuitengeneza Mwanza iendelee kuwa mji wa tofauti na mji ambao utakuwa unaendelea kutoa matunda bora zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unapoongelea kukua kwa mji unaongezea pia kuongezeka kwa watu. Sasa hivi tunazo barabara mbili peke yake, iko barabara ya Kenyatta na barabara ya Nyerere, hizi ndizo barabara peke yake unazoweza kujivunia leo Mwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee tu kusema, naamini Mheshimiwa Waziri analitambua hili na tusifikiri hata siku moja kwa fedha za Mfuko wa Barabara hizi zinazokuja kwenye Majimbo na Halmashauri zetu, shilingi bilioni mbili au tatu zinaweza zikasaidia kupunguza msongamano. Fedha hizi ni kidogo, kama zinaweza kufanikiwa sana zitatusaidia tu kutengeneza barabara za kilometa 0.5, 0.2 au 0.3 na kadhalika, hatutaweza kufikia malengo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo barabara ya kutoka Mwanza Mjini, naizungumzia barabara ya Kenyatta, kuja kutokea Usagara ambako unakwenda kupakana na Misungwi barabara hii ni finyu sana, lakini yako maeneo upanuzi wake unahitaji gharama kubwa sana. Kwa hiyo, kama hatuwezi kuitengeneza kwa maeneo kadhaa na yenyewe ikawa kwa njia nne hatutakuwa tumesaidia sana. Kwa hiyo, niendelee kumuomba Mheshimiwa Waziri, wakati wanakamilisha ujenzi wa njia nne kutoka Furahisha kwenda Airport tuifikirie kwa namna nyingine barabara ya Kenyatta, nazungumzia kutoka mjini kati kwenda Mkuyuni - Butimba, Nyegezi - Mkolani - Buhongwa na hatimaye kukutana na Misungwi ili tuweze kuwa kwenye mazingira ambayo yanafanana sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumze habari ya bandari. Imesemwa hapa, katika bandari hizi zinazojengwa, Bandari za Mwanza zimesahakuwa ni za kizamani sana. Lakini tukiboresha Bandari hizi za Mwanza, naongelea South Port na Mwanza Port, tutakuwa tumesaidia kwa kiasi kikubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, sote tunafahamu mizigo mingi inayotoka Kenya, Uganda wamekuwa wakitumia bandari hizi, lakini hata kukamilika kwa reli ya kutoka Dar es Salaam itakapokuwa imekamilika vizuri bandari hizi bado ni chanzo kikubwa sana. Juzi tumemsikia Mheshimiwa Rais wakati anazungumza na Rais wa Uganda, amezungumzia juu ya bandari ya nchi kavu iliyoko kwenye Kata ya Lwanima.
Mimi nioneshe masikitiko yangu makubwa sana kwa Mheshimiwa Waziri, bandari hii ambayo tayari miaka minne iliyopita toka mwaka 2012/2013 mpaka leo 2017 wananchi kutoka kwenye mitaa minne, nazungumzia wananchi wa Kata ya Lwanima kutoka kwenye mitaa ya Ihushi, Isebanda na Nyabahegi wameshafanyiwa uthamini miaka minne leo lakini bado hawajalipwa hata shilingi moja, Wameendelea kulalamika juu ya bandari ya nchi kavu na mbaya zaidi, hivi ninavyozungumza ziko taarifa kwamba ujenzi wa bandari hii unataka kuhamia Misungwi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Naomba nimpe taarifa kabisa hapa Mheshimiwa Waziri, wananchi wa Kata ya Lwanima mitaa ya Isebanda, nyabahushi hawatakubali kuona mradi huu unahama unakwenda kwenye kata na wilaya nyingine kwa sababu wamekuwa wavumilivu. Wamesubiri kwa muda wa miaka minne wakiwa na matumaini na Serikali yao kwamba watalipwa fidia na ukamilikaji wa bandari hii ya nchi kavu utaongeza ajira, shughuli za uzalishaji kwenye maeneo yao na tutapata fedha kwa ajili ya wananchi wetu, lakini tutakuwa tumeendelea kuchangia pato kwa Serikali yetu na kuhakikisha mazingira haya yanaboreka zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na hii lazima tukubali, ndiyo maana nasema mji wa Mwanza leo itakuwa ni ajabu sana, ukitaka kuangalia tuna kilometa ngapi za lami. Mji unaoitwa wa pili kwa ukubwa haufikishi kilometa 50 za barabara ya lami, hii ni aibu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia barabara za kupunguza msongamano zinarundikwa sehemu moja tu zaidi ya kilomita mia na kitu. Hivi leo mkitupa Mwanza hata kilometa 20 peke yake kupunguza misongamano sisi hatutafurahi? Wananchi hawataona thamani kubwa ambayo na wao wanashughulika katika kuhakikisha nchi yao inaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo haya mambo ni lazima tukubaliane; kasungura tunafahamu ni kadogo, tuko kwenye jitihada za kukusanya mapato lakini hao hao wanaochangia mapato lazima tuwape nafasi na wao wafaidi haka kasungura kadogo hata kwenye kukagawana ukucha, kapaja na kadha wa kadha ili waweze kufikia malengo ambayo wanayakusudia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la fidia naomba litazamwe kwa kipekee sana. Nimelisema kwa haraka kwasababu ya muda lakini haikubaliki wala haiwezi kueleweka miaka minne watu wamekaa wanasubiri fidia halafu wasifikie mwisho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la mwisho, mara kadhaa tunaamini vikao vya RCC ndiyo vikao vikubwa na vinapokuwa vinatoa mapendekezo ni lazima yafikiriwe. Haiwezekani miaka minne mnatoa mapendekezo mbali ya barabara za kupunguza msongamano, kutoka Kenyatta kuendelea kwenye maeneo niliyoyataja lakini tulishawahi kupendekeza na hii ni ahadi ya Mheshimiwa Rais, pale kwenye Jimbo la Ilemela kwa Mheshimiwa Angelina kiko kivuko kwenye Kisiwa cha Bezi ambako kuna wakazi zaidi ya 600 wamekuwa wanatumia mitumbwi ya kawaida. Hii peke yake inaonesha hali ya hewa wakati mwingine kwenye ziwa si rafiki, kuna kila sababu na kuna kila dalili kila wakati wananchi wanaendelea kupoteza maisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo baadaye walijadili kuhamisha kivuko kutoka Ukerewe ikaonekana haitakuwa sawa kwa sababu viko vingi na kadha wa kadha, lakini tumeahidiwa kupewa kivuko kipya. Nimuombe Mheshimiwa Waziri aangalie kwa kipekee hiki Kisiwa cha Bezi kiweze kupata kivuko kipya ambacho kitasaidia kuokoa maisha ya Watanzania zaidi ya 600 wanaoishi maeneo yale ili waweze na wao kuishi kama wananchi wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo nilisema nizungumze machache haya kwa sababu naamini sote tunafahamu Mji wa Mwanza ulivyo, na asilimia kubwa hapa kila mmoja anatamani kupita Mwanza. Ni mji mzuri, tukiutengeneza vizuri utakuwa umekaa kwenye mazingira mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mungu akubariki sana, nakushukuru na naunga mkono hoja asilimia mia moja. Ahsante sana.