Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye amenijalia kusimama katika Bunge hili Tukufu ili niweze kutoa mchango wangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaanza kuchangia ningependa nitoe shukrani zangu za dhati hasa kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali yake ya Awamu ya Tano kwa jitihada kubwa sana ambazo wamechukua hususan katika ujenzi wa flyover, ujenzi wa barabara na standard gauge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kabisa kwamba nchi hii sasa inakwenda kwenye maendeleo ambayo Watanzania wote tulikuwa tunayatarajia ndiyo maendeleo tunayoyataka. Nina imani kwamba siku atakapomaliza muda wake Watanzania watamkumbuka, kama siyo sisi watoto wetu basi watakuwa wanakumbuka historia ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno hayo ya utangulizi ningeomba sasa nianze kuzungumzia suala la barabara, barabara nitakayozungumzia ipo katika kitabu hiki cha hotuba yako Mheshimiwa Waziri, ukurasa 42 unazungumzia barabara hii ambayo inaanzia Handeni, inapita Kibirashi, Kijungu, inaenda Kondoa, Nchemba hadi Singida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii inaunganisha Mikoa Minne, inaunganisha Mkoa wa Tanga, Mkoa wa Manyara, Mkoa wa Dodoma na Mkoa wa Singida. Mwaka jana nimezungumzia sana barabara hii. Barabara hii ina urefu wa kilometa 460 na ipo katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Mheshimiwa Waziri, nimeshakuja ofisini kwako kuizungumzia barabara hii, nimeona mwaka huu katika kitabu chako katika hotuba hii umesema mnatafuta fedha, lakini katika kupitiapitia nikaona mmetenga shilingi milioni 500. Sasa sijajua shilingi milioni 500 ni kwa ajili ya kufanyia kitu gani. Ningependa wakati una-wind up niweze kupata maelezo ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kusema kwa nini tunahitaji barabara ya kiwango cha lami. Wilaya ya Kilindi ndiyo Wilaya peke yake ambayo haina barabara ya kiwango cha lami, lakini Wilaya ya Kilindi ina shughuli nyingi za kiuchumi, kuna ufugaji, kilimo, madini na barabara hii ni shortcut sana Mheshimiwa Waziri kwa mtu anayetokea Handeni akipita Kilindi anakuja kutokea Gairo hapa kwa Mheshimiwa Shabiby. Sijaelewa ni kwa nini mliamua kutengeneza barabara ya kupitia Turiani na kuiacha hii inayotokea hapa Gairo. Anyway siwezi kulaumu kwa sababu zote hizo ni barabara za Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachokiomba Mheshimiwa Waziri, tafadhali sana iangalieni barabara hii, wananchi wa Kilindi wanahitaji mawasiliano kwa sababu kujenga katika kiwango cha lami maana yake mtakuwa mmeinua maisha ya wananchi wa Kilindi, Mkoa wa Tanga na Tanzania kwa ujumla. Utaruhusu upitaji kwa rahisi kwa watu wanaotoka Manyara, kwa watu wanaotoka Tanga kufika Dodoma ambako ni makao makuu ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakuomba Mheshimiwa Waziri ufanye ziara uje uangalie ni nini kinachoendelea kule. Sasa hivi tuna kiwanda cha tiles kinachojengwa Mkuranga. Material yote yanatoka Wilaya ya Kilindi, yanapita magari mazito sana takribani tani 40 kwa siku zaidi ya malori 100. Barabara ile iko katika kiwango cha vumbi, barabara inaharibika na kipindi hiki ni kipindi cha mvua. Nikuombe Mheshimiwa Waziri najua wewe ni msikuvu, muadilifu, utaiona barabara hii, tutafutie wafadhili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hiyo naomba nizungumzie kilomita tano Makao Makuu ya Wilaya, narudia kusema tena, wananchi wa Kilindi wana kilio, mwaka jana nilikuomba tunaomba tujengewe kilometa tano ukatutengea hela ndogo sana shilingi milioni 150 ambazo hazitoshi hata kuwa na nusu kilometa, mwaka huu nimepitia kitabu hiki nimeona umetenga shilingi milioni 120. Ninakuomba Mheshimiwa Waziri, ukizungumza na wataalam wanasema kiasi hicho hakitoshi. Najua mahitaji ni mengi Watanzania wanataka barabara lakini nasi wananchi wa Kilindi tunahitaji, ungeanza hata kilometa mbili tu, kwa sababu inabadilisha hata sura ya mji. Ninaomba Mheshimiwa Waziri uje makao makuu ya Wilaya uangalie hali halisi au mtume Naibu Waziri baada ya bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ningependa kuzunzungumzia barabara ambayo inaanzia makao makuu ya Wilaya inapita Kikunde inaenda mpaka Gairo. Barabara hii Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne aliahidi kujenga katika kiwango cha lami, wakati huo Mheshimiwa Rais sasa hivi John Pombe Magufuli alikuwa ni Waziri wa Ujenzi aliahidi kujenga. Ninakuomba hebu iangalie katika taratibu zako baadaye ni namna gani mnaweza kujenga barabara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningependa kuzungumzia ni suala la minara ya simu. Leo asubuhi nilipata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, kuna matatizo ya mawasiliano Wilaya ya Kilindi, mawasiliano ni tatizo sana. Tunayo kata moja inayopakana na Simanjiro inaitwa kata ya Saunye kule kuna mbuga ya wanyama, kuna wafugaji wengi sana hawapati mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naamini Mheshimiwa Waziri mawasiliano ni biashara, hakuna sababu Wabunge tusimame hapa kulalamika. Ni juu ya makampuni kutafuta wateja ili waweze kupata mapato, mapato yasaidie Serikali. Nakuomba Mheshimiwa Waziri uchukue Kata zifuatazo kwa ajili ya kuweka minara ambazo ni kata ya Tunguli, Saunyi, Misufuni na Kilindi Asilia.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningependa Mheshimiwa Waziri kulichukua hapa ni suala la wakandarasi. Wizara inachelewa sana kuwalipa wakandarasi. Unapochelewa kumlipa mkandarasi maana yake una-entertain gharama kubwa zaidi kwa mfano mradi ulikuwa na shilingi bilioni kumi, ukichelewesha mradi ule kwa kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja maana yake unaruhusu gharama ya mradi iwe kubwa zaidi. Mimi naomba sasa muwe mnafanya tathmini ya muda, mnayo miradi mingi sana, lakini msianzishe miradi mingine mipya bila kuangalia ile ya zamani, nadhani hapo mtakuwa mmepunguza gharama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshuhudia sisi Kamati yetu tulienda katika barabara inayopita Turiani kupita kwa Mheshimiwa Murrad, mkandarasi pale muda umepita sana na gharama anazodai ni mara mbili ya gharama ya mradi ule. Kwa hiyo, nikashauri Mheshimiwa Waziri muwe mnafanya tathmini sana kuangalia gharama za hii miradi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni suala la reli ya Tanga. Waheshimiwa wengi wamezungumzia reli ya Tanga, wapo wazungumzaji waliosema kwamba ni ya muda mrefu sana na sisi watu wa Mkoa wa Tanga tunahitaji standard gauge. Reli ile inayotoka Tanga inaenda Moshi, inapita Kilimanjaro hadi kwenda Musoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wa Tanga tuna Kiwanda cha Saruji, saruji ile inayotoka Tanga ukiipeleka kwa njia ya standard gauge maana yake utaruhusu iuzwe kwa bei ya kiwango cha chini sana. Mimi nina uhakika kwamba mkishamaliza utaratibu wa kufika mpaka Mwanza na Kigoma basi mtarudi na Mkoa wa Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema maneno hayo machache naomba nikushukuru, naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.