Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Korogwe Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
Naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri anayofanya, vilevile nisiache kumpongeza Waziri wa Wizara hii, Naibu Waziri na Katibu Mkuu na Mameneja wa Mikoa hasa Mkoa wangu wa Tanga kwa kazi nzuri wanazozifanya. Usiposhukuru kwa kidogo, hata kikubwa utakachopewa hutashukuru. (Makofi)
Vilevile Mheshimiwa Waziri wangu naomba nikwambie kitu kimoja ambacho kiko ndani ya msingi wangu mkubwa kwamba safari hii nitashika Mshahara wako, nasema haya kwa sababu zifuatazo.
Mheshimiwa Naibu Spika, toka mwaka 2010 Barabara ya kutoka Korogwe kwenda Bumbuli hadi Soni, iko ndani ta Ilani ya Uchaguzi, barabara hii ilitengewa kwamba itawekwa lami, lakini mpaka mwaka jana barabara hii haikutengewa pesa ya aina yoyote, mwaka huu imetengewa milioni 130 tu. Mheshimiwa Waziri hata bubu wakati mwingine ukimzidia anasema.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatupendi sana kuwa tunaongea sana humu ndani, kubishana na viongozi, lakini inapofika mahali tunaponyamaza sana tunaonekana watu wengine hatusemi. Sasa kwa mtazamo huu safari hii nataka niwaambie ukweli kwamba nitashika shilingi ya Waziri. Kwa sababu tumevumilia mno, mahali pengine kote kunatengenezwa barabara, lakini barabara yangu miaka saba. Na miaka saba hii sioni sababu yoyote ambayo inazuia, kila kitu kimefanyika! Niliona niliseme hilo mapema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara ya lami ambayo iliahidiwa na Serikali ya Awamu ya Nne, kilometa
1.1 katika Mji wa Mombo, lakini barabara hii mpaka leo wala sijui kwamba mawazo yao hasa ni nini. Mpaka leo hii haioneshi kwamba inaweza kujengwa kiwango cha lami na vilevile awamu zote mbili zimesema itajengwa kiwango cha lami. Naomba Waziri mhusika muiangalie, sisi hatupendi sana tuwe watu wa kubishana, sisi ndiyo wenye Serikali, tunataka tuisaidie Serikali, pale mahali ambapo tunaona inakwenda tofauti tuunge mkono ili mtusaidie. Sasa tukinyamaza na ninyi wenzetu mnatuona kwamba hatuongei haileti maana nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni bandari ya nchi kavu; katika awamu iliyopita tulikuwa tunasema kwamba katika Mkoa wa Tanga kutakuwepo na bandari ya nchi kavu pale Korogwe, hili mpaka leo imekuwa kama kizungumkuti, haioneshi dalili wala hakuna dalili yoyote, tunayoisikia hapa ni reli ya kati tu na bandari nyingine, Bandari ya Tanga na Mtwara tunaziona kama vile zinasahaulika. Mkifanya namna hii tunakuwa wanyonge kwa sababu ukitaka kuichukua Tanga lazima utaje Mkoa wa Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Mara, Mwanza pamoja na Manyara hii ukiijumlisha inatoa neno la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika reli, reli ambayo ni ya mwanzo kabisa, mojawapo ni reli ya Mkoa wa Tanga. Nashangaa inakuwa ni vitu tofauti, tunapigwa chenga tu, sijui kwa sababu hatuongei au kwa sababu tumenyamaza sana. Naomba Serikali ituangalie, unaposema kwamba mpango wa biashara, uchumi, uchumi hauletwi na Mikoa ya Kati peke yake ni Tanzania nzima lazima kuwe na uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kuhusu hizi barabara za mkoa. Barabara za Mkoa Mameneja wa Mikoa wanafanya kazi nzuri sana, lakini wakandarasi wanatuumiza.
Kuna sehemu inakuwa heavy grading ambayo ni lazima uchimbue barabara halafu ushindilie, lakini cha kushangaza kuna sehemu hawafanyi hizo kazi na hela wanapewa, halafu kibaya zaidi ni kwamba, hela ambazo zinatengwa na Serikali baadae unaambiwa zimechukuliwa tena kwenye Wizara zinapelekwa sehemu nyingine. Hivi maana yake mnaposema hela zinakwenda kwenye mikoa, halafu Wizara inakuja inazipunguza pesa zile na barabara zinakuwa zinaharibika, hivi mkifanya namna hii tutakuwa tunafika mbali? Naiomba Serikali kama tatizo hili lipo naomba litekelezwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kwenye barabara yangu ya kutoka Korogwe kwenda Maguzoni - Muheza imeondolewa hela. Barabara ya kutoka Korogwe kwenda Maramba – Daruni mpaka njia panda ya kwenda Mombasa, wameondoa fedha. Sasa hivi mvua imenyesha barabara ilijengwa vizuri, lakini imefumuka yote kwa sababu malengo ya kutengeneza barabara hayakufanyika. Naomba sana Serikali iangalie suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo linatusumbua sana ni mawasiliano. Katika Tanzania sehemu ambayo inatoa madini nyeti sana ni katika kata ya Kalalani katika kijiji cha Kigwasi lakini sehemu nyingine zote kuna mawasiliano, hapa pia ni Mbuga ya Mkomazi na hapa pia ndipo kunakotoka madini ya aina mbalimbali. Tumeongea, nimekuja nimeongea hapa Bungeni, yanaingia kwenye sikio hili yanatokea sikio hili. Sasa sipendi sana kubishana na Serikali kwa sababu kazi kubwa mmeshatufanyia, hizi ndogo ndogo ni kurekebishiana tu ili tuone kwamba namna gani mtatekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho wachangiaji wenzangu wameongea sana, lakini ukweli mnatuonea sana watu wa Tanga hasa Bandari ya Mwambani. Kila mwaka mnaongelea suala la bandari, mtu anatoka Tanzania anakwenda kutoa mizigo Mombasa anaacha kwenda Tanga kwenda kutoa mizigo wakati ni bandari nzuri. Mtu anaondoka anakwenda anaacha Bandari ya Mtwara yenye kina kirefu, mtu anakwenda Mombasa. Kwa nini jamani? Tuna makosa gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba mkigawa, hata kama kasungura kadogo kama alivyoongea Mbunge mwenzangu wa Mwanza lakini tugawane kidogo, mnapotugawia kidogo nasi tunakuwa na nguvu. Mkinyamaza sana mwisho wake tutakuwa tunasema kwamba hawa labda hatuna imani, lakini mimi nina imani sana na Serikali ya Awamu ya Tano kwa haya mnayofanya, kwa sababu leo pia Rais amenifurahisha sana baada ya kusema yeye hataki vyeti feki, anataka mtu elimu yake aiseme ile. Mimi elimu yangu ni ya darasa la saba na ninaomba muendelee kuichunguza hivyo hivyo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna minara pale kwangu kwa Mkole katika kata ya Chekelei, kijiji cha Bagai, mnara huo umefungwa toka mwezi wa kwanza mpaka leo hii haujafunguliwa sijui sababu ni nini? Kuna kata ya Kizara mmejenga mnara mzuri sana lakini mawasiliano yake yanakuwa ni hafifu.
Naomba Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wako, mmenisaidia sana katika mambo yangu ya kimsingi katika Jimbo langu hasa nilipokuwa naumwa. Mmefanya kazi kubwa sana ya kunipelekea fedha kwa kupitia Meneja wa TANROADS wa Mkoa wa Tanga na barabara zangu zinapitika vizuri, sitapenda kuwaangusha, lakini msituangushe mahali ambapo tunawaamini kwamba ni watendaji wazuri wa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya machache naunga mkono hoja, ujue usipokuja na majibu mazuri hiyo siku ya kuidhinisha ninatoa shilingi yangu mpaka uniambie barabara ya kutoka Korogwe - Kwashemshi - Dindila - Bumbuli - Soni, sasa ijengwe kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsanteni sana, naunga mkono hoja.