Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ziwani
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, sina ugomvi na Waziri lakini najua dhamira yake pia katika maslahi ya Taifa. Nataka niishauri Wizara pamoja na nchi kwa ujumla, nikumbushe kwamba mwaka 1997 Waziri Amani Karume wakati huo akiwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi pamoja na Waziri William Kusila kwa upande wa Tanzania Bara waliunda kamati ambayo ilikuwa ikiongozwa na Profesa Mahalu. Kamati ile pamoja na mambo mengine ilikuwa ikichunguza mambo ya Maritime Law. Kamati ile ilitoka na mapendekezo kwamba kuwe na chombo cha pamoja ambacho kitaweza kusimamia mambo ya marine kati ya Zanzibar na Tanzania Bara, kwa sababu kiujumla mambo ya marine siyo mambo ya Muungano.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lile lilidharauliwa na wala halikufanyiwa kazi, kwa hiyo, mwaka 2001 SUMATRA wakatunga Sheria ya SUMATRA na wenzao Zanzibar wakawa wamenyamaza kimya. Lakini mwaka 2003 wakatunga ile sheria ya The Merchant Shipping Act. Sheria ya SUMATRA ikatoa mamlaka kwa Mamlaka ya SUMATRA kuweza kusajili meli. Mwaka 2006 Zanzibar walivyoona kwamba aah, hawa
wenzetu tayari wameshatunga sheria na mambo yanaendelea na wao wakatunga Sheria ya Maritime Transport Act ambayo ilifuatiwa na sheria baadae mwaka 2009 ya Zanzibar Maritime Authority (ZMA).
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ushauri ule ulidharauliwa kilichotokea SUMATRA wakawa wanasaliji meli inapeperusha bendera ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Zanzibar wakawa wanasajili meli zinapeperusha bendera ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini katikati hapa hakuna chombo chochote ambacho kinawaongoza, kila mmoja anafanya vyake. Kama kuna chombo kilikuwa kinawaongoza nafikiri Mheshimiwa Waziri atuambie.
Mheshimiwa Naibu Spika, Zanzibar wakasajili meli za Iran ambazo ziliwekewa vikwazo na Umoja wa Mataifa, meli zile zikaleta mzozo mkubwa. Kwa hiyo, baada ya kusajiliwa kwa meli zile wakafanya ujanja ujanja wenyewe kwa wenyewe wakalimaliza lile suala.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama haitoshi, baadaye Zanzibar wakasajili tena meli ambazo zilikamatwa na cocaine katika Bahari ya maji ya Uingereza ikiwa na tani tatu za cocaine. Kile chombo hakipo, baada ya kudharau ule ushauri haikupita muda sana, ikakamatwa meli ya Gold Star kule Italy ikiwa na tani 30 za bangi. Kwa hiyo, kile kitendo cha kukataa ule ushauri kwa sababu hili jambo siyo la kimuungano ukitoka katika foreign affairs linaingia jambo la Muungano.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Tanzania imekuwa ikiendelea kupata aibu na wanaofanya hivyo mimi nawajua na wanafanya kwa lengo gani. Viongozi waandamizi wa Zanzibar wanashiriki kikamilifu katika kuhakikisha kwamba wanajipatia fedha kwa njia ambazo hata Taifa kuligharimu haina tatizo.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nilikuwa nazungumza na viongozi wa Zanzibar kuhusu hili jambo, wakaniambia kwamba baada ya matukio hayo kwanza wakaweka mfumo wa kielektroniki ambao sasa IMO wanakuwa wanaziona meli zikisajiliwa. Ule mfumo password waliyonayo SUMATRA, Zanzibar wakaitaka password SUMATRA hakuwapa. Nakubaliana nao wasiwape kabisa, kimsingi hapo sina tatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Zanzibar wanasema ukipitia sheria yao ile ya Maritime Transport Act, kifungu namba 8 wanadai kwamba 8(1) ukija (e) ukisoma huku kinasema kama ni Zanzibar wenye mamlaka ndiyo waliosajiliwa na International Maritime Organisation (IMO), SUMATRA wao hawajasajiliwa na IMO, kwa hiyo haki ya kupata password ni ya kwao.(Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshauri tu Mheshimiwa Waziri kwamba kwanza password wasipewe, pili; lazima tutengeneze chombo katikati hapa ambacho kitatusaidia kufanya mambo haya yasitokee tena. Kwa sababu kuna watu pale kazi yao wanatumia hii sehemu ya kusajilia meli kwa kujipatia kipato binafsi. (Makofi)
Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nikushauri kwamba ukae na timu yako mambo haya ni hatari kwa Taifa ili uweze kulitatua tatizo hili kiuangalifu kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni bandari kuhusu suala la flow meter. Tatizo la flow meter lilikuwa ni kubwa sana katika nchi hii, mafuta yakiibiwa kulikuwa kuna vituo vya mafuta havina idadi. Bandari sasa na watu wengine wameanza wanataka pale flow meter iliyopo pale Kigamboni iondolewe ipelekwe TIPER, maana yake mahali ambako palikuwa pakiibiwa mafuta ndipo sasa wanataka flow meter iondolewe wapate kuiba mafuta.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ujajiuliza flow meter hii tumeifunga kwa dola za kimarekani milioni 16 mwaka mmoja uliopita, bandari wamepeleka watu sita training, wawili kutoka TRA, wawili kutoka Vipimo na wawili kutoka Bandari, wamepelekwa training kwa ajili ya operation ya flow meter, lakini watu hao hawapo wamehamishwa kwenye flow meter.
Mheshimiwa Naibu Spika, flow meter ile wanashusha mafuta machafu, flow meter inapiga alarm wanakwenda kuzima alarm, wanashusha mafuta machafu. Hawana dhamira njema, ukiwauliza wanakwambia pale flow meter ilipo itaharibika mara moja kwa sababu mafuta yanakuwa hayajatulia machafu, nani kawambia walete mafuta machafu! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wanasema kwa sababu ya Kenya zile bomba ziko mbali na matenki yako mbali ndiyo flow meter ina uwezo wa kudumu siyo kweli. Kenya kwanza mabomba yote ni ya Serikali kutoka Mombasa mpaka Nairobi. Mabomba yanayopitisha mafuta ya Kenya tena yapo juu yanaonekana, ya Tanzania yako chini yamejificha yako chini kabisa, sasa watu wana uwezo mkubwa wa ku-bypass mafuta yale wakayachukua. Mheshimiwa Waziri hili usilikubali hawa wanataka kuiba mafuta kwa shinikizo la makampuni ya mafuta ili waweze kuiba mafuta. Kwa hiyo, suala hili Mheshimiwa Waziri lazima uwe mwangalifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, halafu kwa nini watu mmewasomesha, Uingereza, South Africa, mmewasomesha Marekani kuhusu flow meter halafu mnakwenda kuchukua watu wengine mbali mnakuja kuwaweka sasa ambao hawajaenda training mahali popote. Wamepelekwa training miezi mitatu, kwa hiyo, lengo hasa ni kuiba mafuta. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri hili ukilikubali basi utaingia kama yule Waziri mmoja aliyeandika kwa maandishi kwamba suala la flow meter zisimamishwe ili wapime kwa kijiti wapime kwa kijiti, wanapima kwa kijiti halafu nchi hii bwana! (Makofi)
Mheshimiwa Waziri, dhamira yako naijua vizuri sana.
Ahsante.