Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Mchinga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa nakushukuru. Kwa kuwa muda wenyewe mdogo nianze na suala la uwanja wa ndege wa Lindi. Kwa masikitiko makubwa nimepitia kitabu cha maendeleo ukurasa wa 134 mpaka 136 ambapo vimeorodheshwa viwanja vya ndege ambavyo Serikali imevitengea fedha kwa ajili ya kuviendeleza. Kwa masikitiko makubwa uwanja wa ndege wa Lindi umeachwa. Sijui umeachwa kwa kuwa mmeusahau au hamuutaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwanja ule tangu Mheshimiwa Rais aliyetoka madarakani aondoke hatujaona tena ndege kwa sababu Mheshimiwa Salma hapa alikuwa anatua pale kama Mke wa Rais, tangu yeye ametoka madarakani uwanja wa ndege wa Lindi haujatumika tena na ni uwanja wa kihistoria, ni uwanja wa muda mrefu. Naishangaa Serikali kuna mradi mkubwa wa LNG ambao unataka kufanyika takribani kilomita moja tu kutoka uwanja wa ndege. Hao Wazungu wanaotaka kuja watakuja kwa magari? Ama watakuja kwa usafiri gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nataka atakapokuja kuhitimisha, siku moja hapa Mheshimiwa Naibu Waziri wakati anajibu maswali alieleza kwamba uwanja wa ndege wa Lindi utafanyiwa upembuzi yakinifu na pesa itatengwa, leo nimedhihirisha kwamba taarifa alizozitoa Mheshimiwa Naibu Waziri siyo za kweli, ni taarifa za uwongo, uwanja wa ndege wa Lindi mmeusahau, hamuutaki. Kwa nini hamtaki kutenga fedha kwa ajili ya uwanja wa ndege wa Lindi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la fedha za maendeleo ya barabara, nimemweleza Mheshimiwa Waziri, haiwezekani Mkoa mkubwa kama Mkoa wa Lindi mnautengea shilingi bilioni 800, kuna mikoa mingine midogo mnaitengea shilingi trilioni mbili tena ni mikoa ambayo tayari imeendelea. Leo Mkoa wa Lindi ambao miundombinu yake ya barabara bado ni mibovu, haijaendelea, mnautengea shilingi bilioni 800. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie mfano Mkoa wa Kilimanjaro, mmeutengea shilingi trilioni 2.2, Mkoa wa Lindi mnautengea shilingi bilioni 800 kwa sababu gani? Mheshimiwa Waziri tunaomba maelezo Mkoa wa Lindi ni mkubwa sana, mkoa ambao haujaendelea au kwa sababu ni Kusini? Au mnaona gere kwa sababu korosho inalipa sasa? Tunaomba sana Mheshimiwa Waziri kwa kuwa kuna korosho na inahitaji kusafirishwa, korosho hailimwi mjini Korosho inalimwa vijijini, lazima isafirishwe ipelekwe huko bandarini Mtwara ipelekwe Dar es Salaam, tunaomba miundombinu ya barabara ijengwe katika mkoa wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inasikitisha kwa sababu Majimbo nane, Majimbo yote saba hayajatengewa fedha, Jimbo moja tu la Mheshimiwa Waziri Mkuu ndiyo limepata fedha, hili jambo ni la hatari, Majimbo yetu wengine hayana fedha, yamekuwa hayana kitu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri aje atueleze kwa nini Mchinga haijatengewa fedha, kwa nini Liwale haijatengewa fedha, kwa nini Kilwa haina fedha, kwa nini Mtama haina fedha, kwa nini Nachingwea haina fedha, tunahitaji majibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la ubovu wa barabara ya kutoka Somanga kwenda Nangurukuru. Hii barabara imejengwa miaka michache iliyopita, leo hii ukipita katika eneo lile barabara ni mbovu, inathibitisha kwamba imejengwa chini ya kiwango. Eneo hili sasa hivi la Nangurukuru kumekuwa na uharamia, majambazi wanakaa, wanateka watu na sababu, kipande kile cha barabara ni kibovu. Kwa nini Serikali inatumia fedha nyingi lakini barabara zinadumu kwa muda mfupi? Kuna harufu ya nini? Kuna harufu ya ufisadi au kuna harufu gani? Kwa sababu haiwezekani barabara iliyojengwa miaka miwili au miaka mitatu iliyopita leo barabara mbovu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiwa unatembea kutoka Lindi ukifika kipande cha Nangurukuru unasahau kama upo kwenye lami, ni mashimo kwenda mbele. Tunaomba sana majibu ya kina juu ya barabara hususan kipande cha kutoka Nangurukuru kwenda Somanga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la kumalizia ni suala la alama za (X) ambazo mmeziweka kwenye nyumba zetu katika eneo hili la barabara. Tunataka majibu (X) zile za kijani mwisho wake lini? Kama mmeshindwa kulipa tuwaambie wananchi waziendeleze nyumba zao. Mnawawekea alama za (X) hawaendelezi nyumba. Leo ukiingia Jimboni kwangu kuanzia Mkwajuni, Kitomanga, Kilangala, Mchinga mpaka unafika Mto Mkavu kote kuna alama za (X) za kijani. Watu wale hawaendelezi nyumba zao mpaka leo kumekuwa hakuna maendeleo tunahitaji maelezo hizi (X) mwisho wake lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.