Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkuranga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naanza kwa msemo wa Waswahili tunaosema kwamba “Haja ya mja hunena muungwana ni vitendo.” Namshukuru sana na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya na kila mmoja anaona kabisa. Tuseme ukweli kwamba ni lazima tukubaliane kwamba hatuwezi kufanikiwa bila ya kufunga mkanda na ku-sacrifice kwa ajili ya kizazi cha leo na cha kesho. Wazungu wanasema no pain no gain. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa, tulikuwa tukitukanwa hapa, nchi kubwa ya Tanzania tunashindwa na nchi ndogo ndogo. Leo tumenunua ndege sita na mwakani tunanunua ya saba, wapo watu wanakuja na maneno sijui terrible teen, sijui kitu gani. Hayo ni matango pori na mimi namshauri sana Mheshimiwa Waziri akiinuka hapa aseme maneno ya kitaalam awaambie Watanzania na Waheshimiwa Wabunge wasiwe na wasiwasi, hatuna wasiwasi na Mheshimiwa Waziri Profesa aende akanunue ndege eti zenye wasiwasi. Nina hakika kabisa kwamba akiinuka Mheshimiwa Waziri hapa atatuwekea na kutufungia mjadala huu ili tuweze kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kulisema hilo, naomba pia niishukuru sana Serikali yangu, kwa sababu nimekuwa nikiinuka mara nyingi sana kuzungumzia barabara ya kutoka Mkuranga Mjini kwenda Kisiju - Pwani na sasa kazi imeanza. Nimeona katika hotuba ya Rais ya kwamba upo uwezekano mkubwa mwaka huu tukapata pesa za kutengeneza kilomita mbili za lami, hii ndiyo Serikali ya Awamu ya Tano ya Hapa Kazi Tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwa kuwa barabara hii imekuwa ikitengewa pesa nyingi kila mwaka kwa ajili ya maintenance, tunanunua kokoto zinazotoka Jaribu Mpakani takribani kilomita 65 kufika Mkuranga. Tafadhali sana Mheshimiwa Waziri atazame jambo la namna hii. Waone kabisa kwamba huu mpango waliouanzisha wa lami ya kidogo kidogo waufanye kila mwaka badala ya kuingiza hela nyingi katika maintenance ambayo baada ya muda mfupi inaharibika tena. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unaiona Mkuranga ya viwanda na Mheshimiwa Rais amekuja Mkuranga mara mbili, mwezi huu wa Tano au wa Sita atakuja mara ya Tatu kuja kufungua kile Kiwanda cha Tiles. Mvua hizi za masika zimetaka kukifanya kiwanda kile kisipate malighafi, kwa nini? Kwa sababu barabara ya Kimanzichana mpaka Mkamba, Mkamba - Mkuwili kuungana na wenzetu wa Kisarawe imekufa kwa sababu ya mvua. Naomba sasa tuliangalie jambo hili kwa umakini sana, kwa sababu kiwanda kile kinakwenda kulisha tiles za nchi nzima, hatutakuwa na sababu ya kununua tiles kutoka nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri iangalie hii ni barabara ya uchumi, watu walikuwa wakisema humu kwamba malighafi za kiwanda hicho zinatoka nje ya nchi. Nataka nikuhakikishie malighafi yote inatoka Kisarawe, Kilindi
- Tanga, Mkuranga, Kisegese, Vianzi na Mkamba. Hivyo, naomba barabara hii ifanyiwe kazi maridadi kabisa ili tuweze kuinua uchumi wa watu wetu na watu wetu waweze kuona kwamba utengamano wa viwanda na uchumi wao unakwenda sambamba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia kwa ufupi sana nizungumzie suala la kupandishwa hadhi za barabara. Ninazo barabara mbili ningependa zipandishwe hadhi. Barabara ya Kiguza – Hoyoyo, Hoyoyo mpaka kwenda kutokea Kitonga - Mvuti. Barabara hii upande mmoja ni trunk road ya Natioal Road - Kilwa Road na upande mwingine ni barabara ya Mkoa wa Dar es Salaam. Pande zote hizi mbili zinabeba mizigo mizito tena zina lami, lakini sisi barabara yetu ya Kiguza – Hoyoyo kupita pale Hoyoyo kwa Mama Salma pale ni barabara ya vumbi na barabara imechoka. Sasa tunabebeshaje mizigo mikubwa barabara hii na Halmashauri hazina uwezo. Naomba sana Mheshimiwa Waziri akiona barua ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Kamanda Injinia Evarist Ndikilo aipitishe haraka barabara hii nayo pia vilevile iweze kupata kupandishwa hadhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hiyo iko barabara ya Vikindu mpaka Vianzi – Marogoro – Sangatini, upande wa Dar es Salaam kutoka Tundwi - Songani, Pemba Mnazi - Kibada - Mwasonga mpaka Kimbiji inawekwa lami. Upande wetu huku kilomita kama kumi bado ni barabara ya Halmashauri inabeba mzigo mzito. Naomba sasa kwa heshima kubwa na taadhima tuendelee kuthibitisha ya kwamba hii ni Serikali ya Hapa Kazi Tu na akiiona barua ya Engineer Evarist Ndikilo, Mkuu wa Mkoa, Kamanda kabisa basi aitie mkono wake pale Mheshimiwa Waziri, ahakikishe kwamba mambo yanakaa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naomba nichukue fursa hii kuipongeza tena Serikali kwa kazi kubwa inayoifanya ya kulipa madeni ya Wakandarasi. Tunaomba pia iendelee kuhakikisha jambo hili linafanyika kwa ufasaha kwa maana liharakishwe na pesa zinazokwenda katika Halmashauri zetu ziharakishwe, tena nafahamu kwamba Serikali ina mpango mzuri sana wa kuanzisha Agency ya Barabara za Vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wenzangu hapa wamezungumzia jambo la kwamba agency hii ikiwezekana wapewe TANROADS. Sasa sisi hatutaki kurudi nyumba, tunachosema tutakuja kumwambia Waziri wa Fedha aangalie uwezekano ikiwezekana hii Agency ya Barabara za Vijijini ipate pesa na asilimia kubwa zaidi ya ile ya thelathini. Kwa sababu uti wa mgongo wa wananchi wetu ili kuwatoa katika umaskini ni kuwatengenezea barabara zao. Watu wangu wa Mkuranga wakiboreshewa barabara zao vizuri ambacho ndiyo kipaumbele namba moja cha miundombinu, nina hakika kabisa kwamba, watainuka zaidi kiuchumi na watafanya shughuli zao wenyewe. Leo hii mananasi pale yanaharibika ni kwa sababu barabara ni mbovu za vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima kubwa na taadhima naomba nichukue fursa hii kukushukuru sana.