Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafia
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza mtoa hoja, Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa na timu yote iliyofanikisha mchakato wa Makadirio ya Wizara hii.
Mheshimiwa Naibu Mwenyekiti, barabara ya Airport Access Road - Kilindoni mpaka Utende Wilayani Mafia yenye urefu wa kilometa 14 pamoja na kukamilika kwake, lakini kwa masikitiko makubwa imejengwa chini ya kiwango. Ni matumaini yangu Mkandarasi atalazimishwa kuirudia barabara ile na hatua kali za kisheria zichukuliwe kwa kuitia hasara Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mafia kutokana na jiografia yake kuwa ni kisiwa, tunategemea sana Uwanja wa Ndege. Ikitokea dharura hususan nyakati za usiku, ndege haziwezi kuruka kwa kuwa uwanja hauna taa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikitokea dharura ya mgonjwa kukimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili, anaweza kupoteza maisha, kwani ili afike Dar es Salaam, atahitaji kusafiri kwa boti kwa takriban masaa nane hadi kumi ili afike katika Hospitali ya Rufaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, boti ya uokoaji katika Bandari za Kilindoni na Nyamisati ndiyo usafiri wa wengi katika Kisiwa cha Mafia. Ila hatari kubwa iliyo mbele ni kwamba hatuna huduma za uokoaji, yaani Coast guard kutokana na idadi kubwa ya wasafiri kati ya bandari hizi mbili. Tunaiomba sana Serikali iweke Kituo cha Coast guard ili likitokea jambo la dharura waweze kutoa msaada.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu boti ya abiria kati ya bandari ya Nyamisati na Kilindoni Mafia. Wananchi wa Mafia tupo katika wakati mgumu kwenye usafiri wa kuingia na kutoka Mafia. Tumejaribu kushawishi wafanyabiashara waje wawekeze kwenye usafiri wa baharini, lakini mwitikio mpaka sasa umekuwa ni hasi mno. Hivyo tunaiomba Serikali ichukue jukumu la kutuletea kivuko cha kisasa baina ya bandari hizi mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru Serikali kwa kutenga kiasi cha shilingi bilioni 2.5 na tender ya ujenzi imeshatangazwa na ujenzi utaanza muda siyo mrefu. Kwa kuwa ujenzi utachukua zaidi ya mwaka, mazingira ya sasa ya bandari ile siyo mazuri kabisa. Hakuna vyoo, hakuna jengo la abiria na ngazi ya kupanda na kushukia abiria. Niliandika barua kwa Katibu Mkuu wa Ujenzi kuomba ngazi iliyokuwa ya Dar es Salaam ambayo kwa sasa haitumiki ili itusaidie pale Nyamisati. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, wakati wa kujibu hoja, nipate ufafanuzi juu ya ombi hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara kutoka Kilindoni mpaka Rasi Mkumbi yenye urefu wa kilometa 55, Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne aliahidi; na imo katika Ilani ya CCM 2015 -2020. Nimeangalia kwenye kitabu hiki sijaona fedha zozote zilizotengwa kwa ujenzi wa barabara hii. Naomba Mheshimiwa Waziri atupe majibu wananchi wa Mafia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.