Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilindi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais na Serikali yake kwa ujumla kwa jitahada kubwa wanazochukua kwa kuleta maendeleo ya dhati hususan katika kujikita katika suala la usafiri wa anga kwa ununuzi wa ndege mpya pamoja na ujenzi wa reli iendayo kwa umeme (standard gauge). Aidha, dhamira ya dhati ya kujenga na kukarabati viwanja vya ndege, ujenzi wa bandari za ndani, Mtwara na mwisho ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami katika maeneo mbalimbali nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie hotuba hii katika maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Handeni – Kibrashi – Kijungu – Njiro – Mrijo Chini – Dalai – Bicha – Chambalo – Chemba – Kwamtoro – Singida (kilomita 460). Barabara hii ni muhimu sana kwa sababu ipo katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi na kwa sababu inapita katika mikoa minne. Nishukuru kwa mwaka huu wa fedha Wizara imetenga kiasi cha sh. 500,000,000/=. Je, kiasi hiki ni kwa ajili ya fidia au jibu gani? Maana ni kiasi kidogo sana kwa ujenzi wa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii kipindi cha mvua inapitika kwa shida sana, barabara hii ina shughuli nyingi za kiuchumi. Wananchi katika maeneo yote yaliyotajwa ni wazalishaji wakubwa wa mazao mbalimbali hususan mahindi. Wananchi hawa hawapati faida ya mazao yao kwa sababu wanalazimika kuuza chini ya bei ambapo kama barabara ingekuwa ya kiwango cha lami, wigo na fursa ya kuuza kwenye masoko watakayokuza ingekuwa kubwa sana. Niiombe Wizara yangu watafute wadhamini wa kutujengea barabara hii au Serikali itoe fedha za kutosha kutujengea barabara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine katika ujenzi wa barabara ni ujenzi wa barabara kwa kilometa tatu kwenye Makao Makuu ya Wilaya. Mwaka wa jana tulitengewa fedha kiasi cha sh. 150,000,000. Kiwango hiki ni kidogo sana.
Nimeshangazwa sana kwa mwaka huu wa fedha hakuna fedha zilizotengwa, hivi Kilindi kuna tatizo gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wa Tanga, Wilaya ya Kilindi ndiyo wilaya pekee ambayo haina kilometa tatu au tano za barabra katika Makao Makuu ya Wilaya ambayo haina lami. Naomba majibu kutoka kwa Waziri mwenye dhamana, ni kwa nini hatujapewa fedha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Songe – Kwekivu – Iyogwe – Gairo. Barabara hii kwanza ni shortcut kwenda Dodoma, ni mto unaotoka Arusha, Tanga kuja Dodoma. Barabara hii ina shughuli za kiuchumi na pia ina wigo wa magari. Naomba Mheshimiwa Waziri barabara hii nayo ingeingia katika utaratibu wa kujengwa katika kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upandishwaji wa madaraja wa barabara kutoka ngazi ya kijiji kwenda wilaya na wilaya kwenda mkoa. Tunazo barabara nyingi ambazo kwa muda mrefu hazijapandishwa hadhi. Mfano katika Jimbo langu la Kilindi tunaomba barabara zipandishwe hadhi kwa sababu zinakidhi sifa na tayari Meneja wa TANROADs alikwisha fikisha maombi Wizarani. Barabara hizi za vijijini ndizo zilizo na shughuli nyingi za kiuchumi, zikijengwa vema na kuhudumiwa ni dhahiri uchumi wa wananchi wetu utakua. Ni vyema Serikali ilipe uzito mkubwa jibu hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.