Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hongera Waziri na timu yako yote ya Wizara kwa kuandaa hotuba hii na kuiwasilisha hapa Bungeni. Tunaipongeza Serikali kwa hatua za kuanza kuimarisha reli yetu hapa nchini pamoja na ile ya kati kwa kujengwa kwa viwango vya standard gauge ili kuhakikisha mizigo mizito inasafirishwa kwenye reli na kuokoa barabara zetu zinazoharibika sana. Tunashukuru Serikali kwa kutenga fedha za kumalizia kipande cha barabara ya Nyahua - Chaya kilomita 85.4 kwa mwaka huu ili kuunganisha Mkoa wa Dodoma na Tabora kwa maendeleo ya wananchi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Urambo - Kaliua pamoja na fedha kupatikana tangu mwaka jana 2016 na Bodi ya Zabuni kukaa na kutangaza na Wakandarasi kuomba, mpaka leo haijaanza. Serikali ieleze ni kwa nini kipande hiki cha kilomita 32 ujenzi wake haujaanza mpaka sasa na ni lini hasa utaanza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Kaliua – Kazilambwa, kilomita 56 inayojengwa na CHICO ilitakiwa kukabidhiwa mapema mwaka 2017 kwa maagizo ya Waziri Mheshimiwa Profesa Mbarawa, aliyoitoa alipotembelea mradi huu mwaka jana 2016, mpaka leo ni Mei, 2017 bado haujakamilika pamoja na kuwa kazi inaendelea. Serikali itoe agizo kwa Kampuni ya CHICO kukamilisha ujenzi huu ndani ya muda uliopangwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ile Kazilambwa - Ilunde kilomita 48 ni mbaya sana sana na kipande hiki kinaunganisha Mkoa wa Tabora na Mkoa wa Kigoma. Mpango wa Serikali Kuiunganisha mikoa yote kwa barabara za lami. Pia barabara hii ni muhimu sana kwa uchumi na kusafirisha mazao. Ni lini barabara hii itaanza kujengwa kwa lami?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara ya kuunganisha Mkoa wa Katavi na Tabora, barabara ya Mpanda - Kaliua - Ulyankulu kwenda Kahama. Hii ni barabara muhimu sana kwa kusafirisha mazao na biashara kwa mikoa hii mitatu. Mwaka jana Waziri alilieleza Bunge kuwa inafanyiwa upembuzi yakinifu. Serikali ieleze mchakato wake umefikia wapi na ni lini itaanza kujengwa kwa lami?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na uwepo wa reli katika Wilaya ya Kaliua wananchi wengi wa Kaliua wanakosa fursa ya kusafiri kwa treni kwa sababu ya kukosa tiketi na nafasi chache zinazotolewa kwa siku treni inapopita. Nafasi zinazotolewa ni kumi na tano tu kwa kituo na treni za express haisimami pale Kaliua na wananchi wengi wanakosa tiketi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mabehewa yanayopita Kaliua kwenda Kigoma na Mpanda ni machache sana na hayakidhi mahitaji ya wananchi, pia tiketi zinalanguliwa kwa bei kubwa sana, madalali wanakata tiketi kwa bei ya Serikali wanauza kwa bei ya kuruka na wananchi hawana namna wananunua. Mheshimiwa Waziri aliahidi kuongeza mabehewa mpaka leo bado tabu na adha inaendelea. Serikali ieleze mkakati wa kuongeza mabehewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wastaafu wa Shirika la Reli walioachishwa kazi wakati wa EAC mpaka leo hawajalipwa haki zao, Serikali ilete taarifa kamili za wazee kwa wananchi haki zao mpaka wamechoka na wengine wamekufa bila kupata haki zao. Hii kwa nini hawalipwi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mawasiliano eneo kubwa la Wilaya ya Kaliua na hususani Jimbo langu hakuna kabisa mawasiliano ya redio, wananchi wanaishi bila kujua nini kinachoendelea ndani ya nchi yao pia hakuna minara ya simu. Kata zifuatazo mawasiliano ya redio ni magumu sana mpaka radio zifungwe kwenye miti juu sana:-

Kata ya Igwisi, Kijiji cha Mpanda Mlohoka na Igwisi Center; Kata ya Usimba karibu vijiji vyote havishiki redio; Kata ya Ushokola, Kijiji cha Makubi na Mwamashimba; Kata ya Zugimlole Kijiji cha Igombe na Luyombe; Kata ya Ukumbisiganga, Kijiji cha Usimba na Ukumbi Kakonko; Kata ya Usinge, Kijiji cha Kombe; Kata ya Usonye; Vijiji vya Luganjo mtoni, Shela na Maboha. Kata ya Ugunga Vijiji vya Mkuyuni, Mpilipili na Limbula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji vyote hivi mawasiliano ya simu ni ya tabu sana kwani minara iko mbali na eneo lao pia mawasiliano ya redio ni kwa tabu sana na kwingine hakuna kabisa. Naomba Serikali ieleze ni lini wananchi hawa watapelekewa huduma hii muhimu.