Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii nami kuweza kuchangia Wizara hii ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. (Makofi)
Awali ya yote nichukue nafasi hii kuweza kumpongeza Waziri wa Wizara hii, kwa kweli anafanya kazi nzuri na kazi yake siyo ya kubeza hata kidogo anastahili pongezi pamoja na Naibu Waziri wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba nijikite sasa katika kuelezea Idara ya Maendeleo ya Jamii. Naomba nielezee kwanza historia, Idara hii ya Maendeleo ya Jamii ni zao la kihistoria la mapinduzi ya viwanda yaliyofanyika katika karne ya 19 katika Bara la Ulaya. Walipojenga viwanda yalijitokeza matatizo mengi ya kijamii hivyo wakaanzisha masomo ambayo yatazalisha wataalam ambao watashughulika na masuala ya mabadiliko katika jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu nchi za Afrika ikiwemo Tanzania haikufanya makosa kuchukua funzo hili na hatimae kujenga na kuanzisha Vyuo Vikuu vya Maendeleo ya Jamii, pamoja na vyuo vya kati ambavyo moja kwa moja vita-deal na mabadiliko ya kijamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana hata ukisoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 87 ameelezea kabisa kwamba vyuo hivyo vitaendelea na udahili wa wanafunzi watakaojishughulisha na masuala ya maendeleo ya jamii, ni vema tukaangalia kwamba tunapoendelea kudahili wanafunzi katika vyuo vya maendeleo ya jamii tuangalie na wale ambao kwa sasa hivi wapo maofisini, hawa Maafisa wa Maendeleo ya Jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mantiki hiyo, ni wazi kwamba kwa sasa hivi ambapo nchi yetu inapiga hatua kuelekea kwenye uchumi wa viwanda hakuna namna yoyote ambayo tunaweza tukaiacha nyuma Idara hii ya Maendeleo ya Jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kusikitisha sana idara hii kwa kifupi imesahaulika. Mwaka jana wakati nachangia Wizara ya Afya, nilizungumzia Idara ya Maendeleo ya Jamii, lakini ni wazi kwamba sijaona mabadiliko yoyote ambayo yamefanyika. Leo hii ukitembea katika Halmashauri zetu nyingi, siyo katika Mkoa wa Songwe tu nchi nzima Idara hizi za Maendeleo ya Jamii ziko hoi. Watumishi wa idara hii ya maendeleo ya jamii hawapelekewi fedha za oc, wala hakuna vitendeakazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye Halmashauri nyingine unakuta idara ya maendeleo imewekwa nyuma ya Halmashauri, nyingine ziko nje kabisa ya Halmashauri kuonesha kwamba siyo part ya Halmashauri zetu. Suala hili linasikitisha sana. Hali hiyo imepelekea sasa hata fedha ambazo zinapelekwa fedha za miradi, miradi mingi katika Halmashauri zetu inakufa haizai matunda, haioneshi mafanikio kwa sababu tumeiacha nyuma idara ya maendeleo ya jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitolea mfano katika Halmashauri yangu ya Wilaya ya Mbozi, kuna miradi mizuri sana ambayo imeanzishwa na Serikali, lakini kwa sababu wananchi hawajashirikishwa, watu wa idara ya maendeleo ya jamii hawajashirikishwa, inapelekea wananchi sasa hawana ile sense of ownership, wanaona kwamba ile miradi siyo ya kwao, wanaona miradi ile ni ya Serikali, kumbe tatizo hawajaelimishwa kuona kwamba ile miradi ina faida hivyo wanapaswa kuitunza, hii yote ni sababu Idara ya Maendeleo ya Jamii imesahaulika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi utaratibu uliowekwa na Serikali wa kutenga asilimia tano ya vijana pamoja na asilimia tano ya wanawake, lengo lilikuwa ni zuri lakini ukiangalia katika Halmashauri idara inayohusika moja kwa moja kufuatilia pesa hizi ni idara ya maendeleo ya jamii lakini hawashirikishwi ipasavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda leo hii katika Halmashauri zetu hususan Halmashauri ambazo zipo katika Mkoa wangu wa Songwe, wanawake hawana kabisa uelewa wa asilimia tano ambayo inatengwa na Halmashauri. Ukienda kwenye makaratasi unaona kabisa kwamba fedha zinatengwa lakini impact kwenye jamii haionekani, swali ukijiuliza ni kwa sababu Idara hii ya Maendeleo ya Jamii ambayo ndiyo inategemewa kwenda kutoa mafunzo kwa vijana pamoja na wanawake wajue namna gani ya kuweza kuzitumia hizo fedha za Halmashauri, wajue namna gani ya kuweza kuzifuatilia fedha hizo ili ziweze kutumika kama ilivyopangwa. Kwa sababu idara hii haishirikishwi, unaona kabisa kwamba fedha hizo hazijulikani zinaenda wapi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi, Wabunge wa Viti Maalum siyo Wajumbe wa Kamati ya Fedha, kwa hiyo unaweza ukaona ni namna gani ambavyo hizi asilimia tano za wanawake na asilimia tano za vijana zinapotea katika mazingira ambayo ni ya kutatanisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la bima ya afya. Katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri amezungumzia kwamba bado mwamko ni mdogo sana wananchi kuweza kujiunga na hii mifuko ya hifadhi ya hifadhi ya jamii, mifuko ambayo ingeweza kuwasaidia pia wanawake ambao wako vijijini, ambao kimsingi wao ndiyo wana matatizo makubwa sana ya kiafya, wanapata matatizo makubwa sana wanapoenda kujifungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanaojiunga na hii mifuko ukiangalia idadi ni ndogo kwa sababu wanachi bado hawajaelimishwa, elimu bado haijawafikia kwa hiyo hawaelewi umuhimu wa kujiunga na hii mifuko ya bima ya afya. Hii yote ni kwa sababu tumepuuza Idara hii ya Maendeleo ya Jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ukiangalia hata katika jamii zetu, masuala ya unyanyasaji wa kijinsia ya wanawake na watoto yamekua kwa kasi kubwa sana. Dada yangu hapa ameongea kwa uchungu, ni masuala ambayo hata katika Mkoa wangu wa Songwe yapo kwa kiasi kikubwa, watoto wadogo wanaozeshwa, hivi ninavyosema nina mtoto ambaye namsomesha sekondari kwa sababu tu mzazi wake alikwishakupokea ng’ombe 60 ili amuozeshe huyo mtoto. Masuala kama haya tunapaswa kama Taifa kuyapinga… (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.