Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, aliyetuwezesha leo tupo hapa, lakini nichukue fursa hii pia kumshukuru sana na kumpongeza Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya, niwapongeze pia nimpongeze Waziri Mheshimiwa Ummy na Naibu Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo mambo machache ya kuzungumza, jambo la kwanza ndani ya Singida Mjini leo tunajenga Hospitali ya Rufaa ya Mkoa. Mheshimiwa Ummy alifika pale na alitoa maagizo na nimshukuru sana. Naomba nisisitize, tunayo changamoto kubwa ya Hospitali ya Wilaya ya Singida Mjini, eneo kubwa ambalo tunalitegemea ni ile hospitali ya Mkoa tuliyonayo iweze kuhamia iende Hospitali ya Rufaa ambayo ipo Mandewa na ile hospitali ya Mkoa iwe hospitali ya Wilaya. Ninamuomba sana Mheshimiwa Ummy wakati ana wind up atusaidie kutoa tamko hili ili tuweze kuharakisha ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mandewa na ile hospitali ya Mkoa iliyopo pale iwe Hospitali ya Wilaya. Tutakuwa tumetatua tatizo kubwa sana Singida Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nizungumzie zoezi la damu salama. Niipongeze Serikali inatumia gharama kubwa leo na katika mpango huu wa damu salama imetusaidia sana. Mkoa wa Singida, tangu Juni , 2016 mpaka Februari, 2017 wamekusanya unit takribani 2,300, bahati mbaya sana Singida Mjini zilikusanywa unit 12 tu, changamoto kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mazingira mengine inaonesha kabisa Singida Mjini tunawanyonya wenzetu wa Halmashauri zingine kwa ajili ya kutumia zile damu salama. Naiomba Serikali ifanye tathmini na iweze kusimamia zoezi hili kikamilifu kwa kila Halmashauri ili tujue tatizo lipo wapi. Kwa sababu kama unakusanya unit 12 maana yake watu waliochangia damu ni watu 12 tu. inawezekana mwamko ni mdogo au yawezekana watendaji wetu Serikalini wanashindwa kufanya kazi hii vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikifanyika tathmini itatusaidi kuweza kupata damu salama kwa wingi, zoezi hili litatusaidia sana. Niombe sana Serikali iweze kulisimamia jambo hili kwenye maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue fursa hii kuishukuru Serikali, imetupatia fedha za dawa na mpaka sasa ni takribani milioni 200 tumepata Singida Mjini fedha za dawa, nimpongeze sana Dada yangu Ummy. Karibu asilimia 93 ya fedha za dawa zilizokuja Singida Mjini, asilimia 93 siyo jambo dogo Serikali inafanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ninayoipata mwananchi anapokwenda kupata huduma na akaambiwa dawa hamna, nami nasimama kwenye majukwaa kuwaambia kwamba Serikali imeleta fedha za dawa asilimia 93, ninakosa ni mazingira gani ninaweza kuwaeleza, matokeo yake itanilazimu sasa na mimi nigeuke kuwa muuguzi au kuwa daktari au kuwa mhasibu ili niweze kusimamia fedha hizi namna zinavyoweza kutumika. Kwa hiyo, niiombe Serikali, tunapotoa fedha na mkatuachia tu tuendelee kuratibu jambo hili sisi wawakilishi wa wananchi mnatupa mtihani mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ninaona kwenye vitabu tumepata fedha na kweli fedha zimefika, lakini hakuna dawa. Mwananchi anapokwenda akakosa dawa huwezi kueleza, utaeleza kitu gani? Tuna kila sababu sasa ya kusaidiana ni namna gani tufanye kuweza kusimamia utekelezaji wa hizi fedha zinazoletwa. Kama dawa zimenunuliwa ni lazima tujue dawa zipo na wananchi wetu wasipate matatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali Watumishi wetu wanapata wakati mgumu sana, leo tumefika mahali call allowance hamna, extra duty hamna, kazi ni kubwa. Daktari anamaliza shughuli zake, nurse anamaliza shughuli zake lakini ataitwa kwa sababu ni wito na atakuja, atakapokuja kufanya ile kazi halipwi, wanayo madeni makubwa sana watumishi wetu.
Ninaiomba sana Serikali iweze kulisimamia jambo hili, hatuna tatizo hilo, tuna tatizo tu la Menejimenti linalosababisha watumishi wasiweze kupata fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itaua morali ya watumishi. Sisi tunapokaa nao, unapozungumza nao, unafanya mikutano unaona kuna mahali wanajitoa wao kufanya kazi lakini sisi tumeshindwa kuweza kutimiza kile ambacho walistahili kupewa ni haki yao. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana.